3329; Kipimo ni mauzo.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Wakati wa kuanza biashara, watu huwa wanahangaika na mambo mengi wanayoona yana athiri biashara hiyo.
Wanahangaika kupangilia kila eneo la biashara ili kuhakikisha inakwenda kwa mafanikio makubwa.

Lakini cha kushangaza, eneo moja ambalo ndiyo muhimu zaidi kwenye mipango na utekelezaji wa mikakati ya biashara, limekuwa halipewi uzito.
Eneo hilo ni mauzo, ambayo ni muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara.



Ni kupitia mauzo pekee ndiyo fedha zinaingia kwenye biashara.
Kwa umuhimu huo, mauzo yalipaswa kuwa ndiyo kitu namba moja kwenye maeneo yote.

Kutokana na mchango na umuhimu wa mauzo, yanapaswa kuwa ndiyo hatua ya kwanza kwenye mipango yote.
Wajibu wa kwanza kwenye biashara ni kuhakikisha ipo bidhaa au huduma inayoweza kuuzwa kwa wateja lengwa. Hiyo ina maana kwamba bidhaa au huduma hiyo iwe na thamani kwa wale wanaolengwa.

Baada ya bidhaa au huduma kuwepo, kinachofuata ni kuiuza kwa walengwa. Hapa ni kuhakikisha walengwa wanashawishiwa kweli kufanya manunuzi, kwa kuonyeshwa thamani wanayokwenda kupata.

Hapo sasa ndipo penye mtihani ambao ukiweza kuvukwa, matokeo makubwa yanapatikana.
Kama wateja wataielewa thamani na kununua, tena siyo mara moja tu, bali kwa kurudia rudia, hapo unajua uko pazuri.
Kinachofuata hapo ni kuweza kuuza kwa wengi zaidi na kwa ukubwa zaidi ili kupata matokeo makubwa.

Kama wateja hawajaielewa thamani na hivyo kutokuwa tayari kununua, maana yake hapo kuna kazi ya ziada ya kufanya.
Rudi kwenye meza ya mipango na ufanye maboresho kwenye bidhaa/huduma hiyo kuhakikisha inatoa thamani ambayo imeahidiwa.

Kufanya maamuzi yote muhimu ya biashara kwa kigezo cha mauzo ina manufaa makubwa sana.
Lakini utashangaa jinsi watu wengi wanavyofanya mambo mengi na makubwa kwenye biashara, huku wakiyaweka mauzo pembeni kabisa.

Wewe usiwe hivyo, usikazane na ukuaji zaidi wa kitu wakati bado hujajua kama hata kinahitajika kwa namna unavyodhani.

Kwenye biashara, wacha soko likuambie kipi sahihi na kipi siyo sahihi kupitia mwenendo wa mauzo.
Ukiweza kwenda vizuri na mauzo, biashara nzima itakwenda vizuri.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kazi ya kwanza ya kila mmiliki wa biashara ni mauzo.
Hata kama biashara ina wafanyakazi wengi kiasi gani, mauzo yanasimamiwa moja kwa moja na mmiliki.
Lengo ni kuhakikisha kila mmiliki wa biashara anaelewa kila kinachoendelea kwenye biashara yake na kufanya maamuzi sahihi.

Maamuzi yote unayofanya kwenye biashara, hakikisha yanaanzia kwenye mauzo halisia ili kuweza kuboresha na kuuza kwa ukubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe