Rafiki yangu mpendwa,
Tunaishi zama ambazo zina maendeleo makubwa sana ya teknolojia. Lakini pia ni zama ambazo zina mambo ya kushangaza sana.
Moja ya mambo yanayoshangaza sana zama hizi ni vitu vingi ambavyo vinapatikana bure, wakati hao wanaovitoa bure wanaingia gharama.
Mfano mzuri ni mitandao ya kijamii ambayo tunaitumia, mingi sana tunaitumia bure kabisa bila ya kulipa gharama yoyote. Ukishakuwa tu na mtandao, basi unatumia bila ya ukomo wowote.
Lakini sasa, kitu cha kushangaza ni kwamba makampuni yanayoendesha mitandao hiyo ya kijamii ni moja ya makampuni yenye mafanikio na kuwafanya wamiliki wake kuwa matajiri wakubwa.

Swali la kujiuliza huo utajiri wao unatoka wapi wakati huduma zao zinatumiwa bure na watu? Na hapo ndipo inapokuja siri kubwa ambayo watu hawaijui. Siri hiyo ilitolewa na mmoja wa wamiliki wa mitandao hiyo, Mark Zuckerberg ambaye ni mmiliki wa Facebook na mitandao mingine. Kwenye moja ya mahojiano na baraza la Seneti, aliulizwa kama mtandao wao ni bure kwa kila mtu kutumia, wao wanapataje fedha? Alijibu kwa neno moja tu; MATANGAZO. Na hapo akawa ameeleza mchezo mzima uliojificha kwenye huduma zote zinazoonekana ni za bure. Kwamba ile bure ni kuwakusanya watu wengi watumie, lakini fedha wanapata kupitia watu wanaotaka kutangaza vitu vyao kwa watu hao wengi.
Mfano huo mmoja unatuonyesha jinsi ambavyo kuna rasilimali tulizonazo ambazo watu wapo tayari kulipia ili wazipate. Moja ya rasilimali hizo ni umakini wetu, ambapo huduma nyingi za bure zinanasa umakini huo na kuuza kwa wale wanaotaka kufikisha ujumbe wao kwa wengi zaidi.
Umakini wako ni rasilimali muhimu sana, rasilimali ambayo inawindwa na watu wengi mno. Kila tangazo unalokutana nalo, linawinda huo umakini wako. Kila kelele unayoisikia, ni umakini wako unawindwa. Watu wapo tayari kulipia ili kunasa umakini wa watu wengi zaidi.
Kuelewa hilo vizuri, angalia gharama za kutangaza kwenye vyombo vya habari. Matangazo ya mchana au usiku sana hayana bei kubwa, kwa sababu wakati huo hakuna watu wengi wanaofuatilia. Lakini matangazo ya asubuhi na jioni, muda ambao ndiyo watu wengi wanafuatilia, gharama yake inakuwa kubwa.
Swali ninalotaka wewe rafiki yangu ulitafakari ni hili, kama watu wapo tayari kulipa gharama ili kupata umakini wako, vipi kama wewe utaweza kuudhibiti na kuutumia vizuri? Si utaweza kufanya makubwa sana kuliko unavyofanya sasa? Ndiyo, huo ndiyo uhalisia ambao watu wengi hawajawahi kukuambia, kwa sababu nao hawajui.
Njia kuu ya kuulinda umakini wako ni wewe kuupeleka kwenye mambo muhimu na yenye tija kwako. Kile unachofanya, kipe umakini wako wote na epuka aina yoyote ya usumbufu isikuingilie kwenye kufanya.
Kuna kitu kimoja muhimu kuhusu umakini ambacho kimekuwa hakiongelewi sana, ambacho ni kuchoka haraka pale unapohangaisha umakini wako kwenye mambo mengi. Kwa mfano unapoianza siku yako kwa kufanya maamuzi mengi, ambayo hata hayana tija, unaishia kuchoka haraka na kushindwa kufanya maamuzi muhimu baadaye. Hilo hupelekea iwe rahisi kwako kuahirisha mambo ya msingi.
Hivyo kwenye kulinda umakini wako, jizuie kufanya maamuzi mengi yasiyokuwa na tija mapema. Badala yake ianze kila siku yako na mambo ambayo ni muhimu zaidi na yale yasiyokuwa muhimu yafanye mwisho wa siku. Hata kama utakuwa umechoka na kuahirisha, utakuwa umeahirisha mambo yasiyokuwa na tija.
Umakini wako ni moja ya rasilimali tatu muhimu ulizonazo na unazoweza kuzitumia kufanya makubwa zinazowindwa na wengine. Rasilimali nyingine mbili nimezielezea kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Angalia kipindi hicho na ujifunze ili ukalinde rasilimali zako tatu muhimu zinazowindwa sana na uzitumie kufanya makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.