Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli maarufu ya Kiingereza inayosema; MIND YOUR OWN BUSINESS, ikiwa na maana ya mtu ujali mambo yako kuliko kuhangaika na mambo ya wengine.

Ni kauli rahisi, lakini iliyobeba ujumbe mkubwa sana ambao mtu ukiweza kuufanyia kazi, utafanya makubwa sana kwenye maisha yako. Ukweli ni kwamba pamoja na malalamiko ambayo tunayo kuhusu muda, bado huwa tunapoteza muda mwingi sana kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

Moja ya eneo ambalo watu wengi tumekuwa tunapoteza muda ni kuhangaika na mambo ya wengine, mambo ambayo siyo tu hayatuhusu, bali pia hayana mchango wowote kwenye kile tunachotaka kupata kwenye maisha.

Tumekuwa ni watu ambao tunafuatilia sana yale yanayoendelea kwenye maisha ya wengine, wakati mambo yetu wenyewe hatuyapi umakini wa kutosha. Mwisho wake ni tunaishia kutokufanya makubwa, siyo kwa sababu hatuwezi, bali kwa sababu tumetawanya sana nguvu zetu.

Yamefundishwa mengi kuhusu kutokuhangaika na mambo ya wengine na mtu kujali mambo yako, lakini bado wengi wamekuwa hawaelewi. Na jambo la kushangaza ni kwamba mambo haya hayajaanza kufundishwa leo, bali yamefundishwa miaka mingi sana iliyopita.

Aliyekuwa mtawala wa Roma na ambaye pia alikuwa Mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha tatu cha Meditations, ameshirikisha namna bora ya mtu kujali mambo yako ili usihangaike na mambo ya wengine na uweze kufanya makubwa. Kwenye kitabu hicho, Marcus ameeleza mengi ambayo mtu ukiweza kuyafanyia kazi, basi utakuwa na muda mwingi wa kuhangaika na mambo yako na kufanya makubwa.

Kitu kikubwa sana ambacho Marcus amesisitiza kwenye kitabu hicho ni muda pekee ambao tuna udhibiti nao, ambao ni muda tulionao kwenye wakati uliopo. Kuhangaika na muda ambao umeshapita, ambao huwezi kuubadili au kuhangaika na muda ujao ambao hatuwezi kuuathiri, ni kupoteza muda ambao tunao. Kadhalika kwa watu, kuhangaika na waliyofanya huko nyuma, wanayofanya sasa au watakayokuja kufanya, haina mchango wowote kwetu kupata kile tunachotaka.

Kujitambua na kujitumia wewe mwenyewe vizuri ni kitu kingine ambacho Marcus amekiongelea kwenye kitabu hiki. Akieleza kwamba tuna sehemu tatu, mwili ambao ndiyo unafanya, akili ambayo ndiyo inafikiri na roho ambayo ndiyo inatoa msukumo. Anaeleza vitu hivyo vipo kwa watu wote, wema na wabaya, hivyo unapaswa kuvitumia vizuri ili uweze kufanya makubwa.

Marcus anasisitiza kama kila mtu angeweka umakini mkubwa kwenye mambo yake kama anavyoweka kwenye mambo ya wengine, angeweza kupiga hatua kubwa sana. Kuhangaika na mambo ya wengine ni upotevu mkubwa wa muda na nguvu kwa sababu huwezi kuathiri chochote kwa wengine. Kwa kuhangaika na mambo yako, una fursa ya kuyafanya kwa ubora zaidi.

Kuna mahangaiko ambayo watu huwa tunajipa na yanazidi kutuchosha na kupoteza muda wetu mwingi. Marcus anatolea mfano wa mtu kuhangaika na mambo ya asili, ambayo yapo kama yalivyo na hakuna unachoweza kufanya kuyabadili. Ni mara ngapi umekuwa unafanya hili, labda ulitaka jua liwake ufanye shughuli fulani lakini mvua ikanyesha na hapo ukaanza kuilalamikia hiyo mvua na kukwama? Ingekuwa vyema kama ungeikubali mvua na kuendelea na mambo mengine yanayowezekana kufanyika kukiwa na mvua kuliko kupoteza muda kulalamikia kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kujali mambo yako kutoka kwenye kitabu hicho cha Marcus Aurelius. Nakualika uweze kusikiliza kipindi hiki, ujifunze na kwenda kuchukua hatua ya kujali mambo yako ili uweze kufanya makubwa. Anza kwa kujipa wewe mwenyewe kipaumbele na utaweza kufanya makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.