3330; Vitu vinavyokuzuia.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Tunaweza kupima ukubwa wa malengo yako na namna ulivyojitoa kuyafikia kwa kuangalia vitu vinavyokuzuia kuyafikia malengo hayo.
Kwa malengo yoyote uliyonayo, lakini ukakubali kuzuiwa na kitu chochote kile kuyafikia, inadhihirisha moja au vyote katika haya mawili.
Moja ni siyo malengo makubwa zaidi kwako, hayana umuhimu kiasi hicho.
Mbili ni hujajitoa vya kutosha kuyafikia malengo hayo. Unatamani ungeyafikia, lakini hujajitoa vya kutosha kuweza kukamilisha hilo kwa uhakika.
Unapoeleza sababu zozote zinazokuzuia kufikia malengo uliyonayo, unachoonyesha ni udhaifu wako binafsi.
Kwa sababu, kuna watu wengine ambao wameweza kufikia malengo makubwa kuliko yako, wakiwa na mazingira magumu kuliko ya kwako.
Hivyo kitu ambacho unadhani kinakuokoa, kinazidi kukuzamisha, kukuanika wazi jinsi ambavyo hujajitoa vya kutosha.
Mara nyingi, ukiwa unapambania malengo yako, hata kama huoni namna utayafikia, watu wanakuona kama tayari unajitambua na upo njia sahihi.
Ni mpaka pale watakapokusikia ukitoa sababu za kuyashindwa malengo hayo ndiyo wanakuja kugundua hukuwa umejitoa kama walivyodhani.
Wanaona kumbe ulikuwa unabahatisha tu.
Kulinda heshima yako, unapoweka malengo yako, hebu yapambanie kwa kila namna mpaka uyafikie.
Kama upo hai, pambana mpaka tone la mwisho.
Muda ambao ungetumia kutoa sababu za kushindwa kwenye malengo uliyojiwekea, unapaswa kuwa umetingwa kuyapambania malengo hayo.
Kila mtu huwa anapitia hali ya kushindwa kwenye maisha yake.
Wale wanaoshindwa wakiwa wanapambana, wanaendelea kuheshimika hata kama bado hawajapata walichotaka, mapambano yao yanakuwa dhahiri.
Wakati wale wanaotoa sababu za kushindwa, wanadharaulika, kwa kuonekana hawakujitoa vya kutosha.
Usikubali kupoteza vyote, malengo yako na heshima/imani ambayo watu wanayo kwako.
Pambana mpaka tone la mwosho na uyafikie malengo yako au hata kama hutayafikia uendelee kuheshimika na kuaminika na wengine.
Asiwepo yeyote mwenye uthubutu wa kukuita wewe ni mvivu au mzembe ndiyo maana umeshindwa.
Pambana uwe mfano dhahiri na kielelezo cha namna sahihi kwa mtu kuyaendea malengo yako.
Uzuri ni kwamba hayo yote yapo ndani ya uwezo wako.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, hatupotezi muda kwenye maelezo ya kwa nini tumeshindwa au haiwezekani.
Kila mwanajamii hiyo ametingwa na kuyapambania malengo yake, haupo muda wa kupoteza kwenye sababu za kushindwa au kutokuwezekana.
Sababu na visingizio ni lugha ambazo hazipo kwenye jamii hiyo.
Kinachokubalika ni uchukuaji wa hatua, kwa mtu kujitoa hasa kwenye kile ambacho anakitaka.
Hivyo ndivyo kila mwanajamii anapata heshima kubwa ndani ya jamii hiyo, kwa mapambano makubwa anayoyaendesha kwenye malengo aliyonayo.
Kuendesha mapambano ya uhakika ndiyo tiketi na heshima kubwa kwenye jamii hii. Hupaswi kuipoteza kwa namna yoyote ile.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe