3331; Chanzo cha matatizo yote.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Magumu, changamoto na matatizo yote uliyonayo, yanasababishwa na kitu kimoja tu, uhai.
Unayapitia yote hayo kwa sababu upo hai, siku uhai unapoisha, na yote yanaisha kwako.

Unapata maumivu mbalimbali kwa sababu upo hai.
Siku uhai wako ukiondoka, hakuwezi tena kuwa na maumivu kwako.

Biashara pekee ambazo hazina matatizo ni biashara ambazo zimekufa.
Kitendo tu cha biashara kuwa hai, kunakuwa na matatizo na changamoto mbalimbali.

Kutaka maisha ambayo hakuna matatizo wala changamoto ni kutaka kifo. Hakuna uhai usioambatana na matatizo na changamoto.

Unaweza kudhani una matatizo na changamoto kwa sababu ya ngazi ya chini ambayo upo.
Ukadhani ukipambana na kwenda ngazi ya juu zaidi utayamaliza matatizo na changamoto zote.
Ni mpaka unapofika kwenye ngazi hizo na kukaribishwa na matatizo na changamoto mpya.

Unaweza kuona kama matatizo na changamoto vinakuandama kwa maisha yako yote.
Lakini ukweli ni kwamba hiyo ni sehemu ya maisha, ambayo hakuna namna unaweza kuikwepa kama upo hai.

Namna pekee ya kuwa na maisha tulivu na kufanya makubwa ni kukubaliana na hiyo hali.
Pale unapotegemea magumu na changamoto zitakuwepo kwenye kila hatua ya maisha yako, unajiandaa vyema kuzikabili na kuzivuka.
Na hapo unakuwa umekaribisha matatizo na changamoto nyingine.

Hili ni jambo unalopaswa kukubaliana nalo ili mambo yako yaweze kwenda vizuri.
Kadiri unavyolikataa, ndivyo unavyoyafanya maisha yako kuwa magumu na kuteseka zaidi.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA,  ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, magumu na changamoto ni vitu tunavyojivunia navyo.
Huwa hatulalamiki pale tunapokutana na vitu hivyo, badala yake tunafurahia, kwa sababu ni kiashiria bado tupo hai na tunakua.
Magumu na changamoto zinapoongezeka, tunajionea wazi kabisa kwamba tumepiga hatua.

Kwa kila hatua tunayopiga, tunajua kabisa kwamba tunatoka kwenye magumu na changamoto za chini na kwenda za juu zaidi.
Hivyo tunajiandaa kukabiliana nazo kwa ukubwa zaidi.
Hivyo ndivyo tunavyoenda na mafanikio tunayoyapata na kuzidi kunufaika nayo.

Hatutegemei mambo yawe rahisi, hivyo tunajiandaa kukabiliana na kila ugumu utakaokuja.
Hatutafuti njia za mkato, bali tunafuata mchakato mzima.
Hatulalamiki wala kulaumu, bali tunashukuru kwa yote.
Tunayafurahia maisha pamoja na yote yanayoandamana na maisha hayo.
Wewe kama sehemu ya jamii hii ya kipekee ya KISIMA CHA MAARIFA, yakubali haya na uweze kwenda nayo vizuri ili kujenga maisha ya mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe