Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio ni kitu kinachopendwa na kila mtu, japo wachache sana ndiyo wamekuwa wanayapata. Mafunzo mengi kuhusu mafanikio ambayo tumekuwa tunayapata yamekuwa yanaangalia sana mchango wa mtu binafsi kwenye kufanikiwa au kushindwa kwake.

Ni sahihi kwamba mtu binafsi ana mchango mkubwa kwenye matokeo anayoyapata kwenye maisha yake, iwe atafanikiwa au atashindwa. Lakini mchango binafsi siyo kitu pekee kinachoathiri mafanikio anayopata mtu.

Mazingira yamekuwa na athari kubwa kwenye mafanikio ambayo watu wanapata au kukosa. Na kwa bahati mbaya sana, athari ya mazingira imekuwa haionekani wazi wazi. Hiyo ni kwa sababu mazingira yanakuwa yamezoeleka kiasi kwamba yanaonekana ni sehemu ya maisha. Kwa kuwa mtu anakuwa kwenye mazingira husika kwa muda mrefu, anakuwa ameyazoea na kuona ni sehemu ya maisha ya kawaida, hivyo haiwi rahisi kwake kuona athari za mazingira hayo kwenye mafanikio yake.

Kuna mambo mengi yanayoathiri mafanikio kutoka kwenye mazingira, lakini matano makubwa ndiyo yamekuwa na athari kubwa zaidi. Tunakwenda kujifunza hayo hapa na hatua za kuchukua ili mazingira yasikukwamishe kufanikiwa. Uweze kuyatumia vizuri na kufanya makubwa.

Moja; Kupata Mahitaji Ya Msingi.

Mtu kuweza kutimiza mahitaji yake binafsi ina athari kubwa sana kwenye mafanikio ambayo anaweza kuyapata. Watu wengi ambao wanaanzia chini kwenye umasikini wamekuwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu muda wao mwingi wanautumia kwenye kutimiza mahitaji ya msingi kama chakula na malazi.

Wale ambao wameshavuka hatua hiyo ya kutafuta mahitaji ya msingi ndiyo wanaoweza kupeleka fikra zao na muda wao kwenye kufikiria na kufanya mambo makubwa zaidi. Kama hujui unapata wapi hela ya kula kesho, ni vigumu sana kufikiria mambo makubwa. Fikra zako zote zinakuwa kwenye kupata mlo unaofuata au mahitaji mengine ya ngazi hiyo.

Hatua ya kuchukua ili hili lisiwe kikwazo kwako ni kuhakikisha unapambana kujiwezesha kutimiza mahitaji yako ya msingi hata kama huna kipato cha moja kwa moja. Mfano kuwa na akiba ya kuweza kuendesha maisha yako kwa kutimiza mahitaji ya msingi kwa kipindi cha miezi 6 mpaka 12 ijayo. Hapo utaweza kuwa na utulivu kwenye kufikiria na kuchukua hatua kwenye mambo makubwa zaidi.

Mbili; Watu Wanaokuzunguka.

Huwa kuna kauli kwamba maisha yako ni wastani wa watu watano unaotumia nao muda wako mwingi, yaani wale unaokaa nao sana. Na hilo limekuwa linajidhihirisha wazi, kwani huwa ni vigumu sana kufanikiwa kuwazidi wale ambao unakuwa nao muda mwingi. Kiwango cha mafanikio unayoyapata kinategemea sana mafanikio ya watu wa karibu yako. Kila utakapojaribu kufanikiwa kuliko wao, watakurudisha nyuma ili ubaki kama wao.

Hatua ya kuchukua ni kutumia muda wako na watu ambao wana mafanikio makubwa kuliko wewe au wanapambana kupata mafanikio makubwa zaidi ya pale walipo sasa. Waepuke sana watu ambao wamesharidhika na pale walipofikia kwenye maisha. Huna haja ya kugombana nao, wewe acha tu kutumia muda mwingi na wao. Na kama huna watu waliofanikiwa wa kuwa nao, chagua mashujaa ambao utajifunza kwao kupitia kusoma vitabu vyao na kufuatilia maisha yao, iwe wapo hai au walishakufa.

Tatu; Viwango Vya Kijamii.

Kila jamii huwa ina viwango vyake vya mafanikio, ambavyo mtu akifikia anasifiwa na kuonekana amefanya makubwa. Kwa jamii za chini, kiwango cha mafanikio kinakuwa chini pia, hivyo wale wanaokifikia kiwango hicho wanaridhika haraka. Mfano mzuri ni jamii za vijijini, utakuta wanaohesabiwa kufanikiwa, hawajafanya makubwa sana ukilinganisha na wa mjini. Lakini kwa kujilinganisha na wengine kwenye jamii, wao wanaonekana kufanya makubwa. Wakati kwenye jamii za mijini, viwango vya mafanikio ni vikubwa hivyo watu wanajisukuma zaidi.

Hatua ya kuchukua ni kwenda kwenye jamii ambazo zina viwango vikubwa vya mafanikio ili kila hatua unayopiga unakuta kuna wengine wamepiga zaidi. Hilo linakupa msukumo wa kufanya zaidi. Na kama unachagua kubaki kwenye jamii yenye viwango vidogo, basi usijilinganishe na wale walio kwenye jamii hizo, badala yake weka viwango vyako juu sana na vipambanie hivyo.

Nne; Rasilimali Zilizopo.

Kila eneo huwa lina rasilimali zake za kipekee, ambazo zikiweza kutumika vizuri zinakuwa na mchango kwa mafanikio ya watu walio kwenye eneo hilo. Mfano maeneo yenye madini, uchumi wake mkubwa utakuwa kwenye eneo la madini, kadhalika kwa kilimo na shughuli nyingine. Rasilimali zilizopo zinaathiri shughuli gani za uchumi zinakuwa na nguvu.

Hatua ya kuchukua ni kufanya shughuli ambazo zinatumia rasilimali zilizopo vizuri ili kukupa mafanikio makubwa. Usihangaike na mambo ambayo yanakuwa magumu kimazingira, badala yake nenda na yale ambayo tayari ni rahisi, ila wewe yafanye kwa ubora zaidi na kwa namna ambayo wengine hawafanyi. Kwa mfano kama kuna mgodi mpya wa madini umegundulika na kila mtu anakimbilia kuchimba madini, wewe usiende kuchimba madini kama hao wengi, bali wauzie vifaa vya uchimbaji, utafanikiwa bila ya ushindani mkali. Ukiwa mbunifu kwa kuyaangalia mazingira vizuri na rasilimali zilizopo, utaweza kufanya makubwa sana.

Tano; Uongozi Na Sera.

Uongozi na sera zilizopo vimekuwa na athari kubwa kwenye mafanikio ambayo watu na jamii kwa ujumla inaweza kupata. Maeneo yanayopata mafanikio makubwa yamekuwa na uongozi mzuri na wenye sera nzuri ambazo zinavutia mafanikio. Wakati maeneo yanayoshindwa, yanakuwa na uongozi mbaya na sera mbovu.

Hatua za kuchukua, kwa kuwa uongozi na sera siyo kitu ambacho kipo ndani ya udhibiti wako wa moja kwa moja, tafuta nafasi ya kwenda kwenye maeneo ambayo uongozi na sera zake zinachochea mafanikio. Kuna mataifa na miji ambayo imepata mafanikio makubwa kwa uongozi na sera zake. Kama hilo litakushinda basi zijue vizuri sera za eneo ulipo na kuona njia bora ya kuzitumia ili kufanikiwa. Kwa kujua kuzitumia vizuri sera zilizopo unakwepa kufanya makosa ambayo yatakugharimu na kukuzuia usifanikiwe.

Haya ni maeneo matano ya mazingira ambayo yamekuwa na athari kubwa kwenye mafanikio ambayo tunayapata kwenye maisha yetu, kwa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeyafafanua haya zaidi pamoja na mifano ya kila eneo. Karibu usikilize kipindi hicho na uzidi kujifunza, upate msukumo wa kwenda kuchukua hatua na kuyatumia vizuri mazingira yako kujenga mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.