Rafiki yangu mpendwa,
Lengo la kwanza la biashara yoyote ile ni kutengeneza wateja, ambao wanaiamini biashara na kuichukulia kuwa sehemu yao. Kitendo cha biashara kuwa na wateja wanaoiamini hainufaiki tu na manunuzi yao. Bali biashara inaweza kuwatumia wateja ilionao kuwa sehemu ya kupata wateja wengine, tena ambao ni wazuri kuliko wanaopatikana kwa njia nyingine.
Rafiki, huwa wanasema mwanzo ndiyo mgumu kwenye jambo lolote lile. Hiyo ni kwa sababu mwanzoni kunakuwa na vitu vingi ambavyo hujui jinsi ya kuvifanya kwa uhakika, lakini pia unakuwa huaminiki vya kutosha. Lakini unapozidi kuendelea kufanya, ndivyo mambo yanavyoendelea kuwa rahisi.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, mwanzo huwa ni mgumu, kwa sababu unaanza biashara ukiwa huna wateja kabisa. Kuwaaminisha wateja wa kwanza kukubali kununua inahitaji kazi na uvumilivu mkubwa. Wengi huwa wanashindwa kwenye hatua hii na biashara kufa. Lakini wale wanaoweza kuvuka huwa wanakuza biashara zao.

Changamoto kubwa ambayo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakutana nayo ni zoezi la kupata wateja kuzidi kuwa gumu kadiri muda unavyokwenda. Tunategemea kama mwanzo ni mgumu, muda unavyozidi kwenda mambo yawe rahisi. Kama kuwapata wateja wa kwanza ilikuwa vigumu, kupata wateja wanaoendelea iwe rahisi.
Lakini sivyo inavyokuwa kwenye uhalisia, biashara nyingi kila wakati mambo ni magumu. Kupata wateja wa mwanzo ni kugumu na kupata wateja wa mwendelezo ni kugumu pia. Sasa basi, kama upo kwenye biashara na zoezi la kupata wateja linazidi kuwa gumu kadiri muda unavyokwenda, kuna mambo hayafanyiki sawa.
Biashara yoyote ambayo tayari ina wateja ambao wanaiamini, na utajua biashara ina wateja wanaoiamini kama wananunua na kurudi tena kununua, inapaswa kuwa rahisi kupata wateja kadiri muda unavyokwenda. Hiyo ni kwa sababu wateja wanaoiamini biashara ni mgodi wa dhahabu kwenye biashara yoyote ile.
Wateja wanaoiamini biashara ni chanzo kizuri na cha uhakika cha wateja wengine wengi wa biashara hiyo. Hilo litawezekana kama biashara itaweza kuweka mfumo mzuri wa kuwatumia wateja waliopo kupata wateja wapya zaidi kwenye biashara.
Zoezi la biashara kutumia wateja waliopo kupata wateja wapya linaitwa rufaa, ambapo biashara inatumia imani ya wateja waliopo kuaminika na wateja wengine wapya.
Kikwazo cha kwanza cha wateja wapya kununua kwenye biashara ni kukosa imani, kwa sababu hawajawahi kununua kwenye biashara. Wanaweza kuwa na uhitaji na kumudu, lakini kwa sababu hawajawahi kununua, wanakosa uhakika kama watanufaika. Uwepo wa wateja ambao tayari wameshanufaika, inawasaidia kuwa na uhakika na kununua.
Zoezi hili linaweza kutokea bila hata ya biashara kufanya chochote, kwa sababu kuna wateja ambao watakuwa tayari kuwaambia wengine kuhusu biashara ambazo wananufaika nazo. Lakini biashara kusubiri mpaka wateja waambiane wao wenyewe, itakuwa inajichelewesha kunufaika zaidi.
Hivyo basi, kila biashara inapaswa kuwa na mkakati wa kutumia wateja waliopo ili kuwafikia wateja wapya na kuwashawishi kununua. Kwa sababu njia hii ni rahisi zaidi kuaminika, ndiyo ambayo pia ina nguvu kubwa. Hivyo kila biashara inapaswa kutumia njia hii kwa uhakika ili kupata wateja wengi.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha jinsi kila biashara inavyoweza kuweka mkakati kabambe wa kutumia wateja waliopo kupata wateja wengi zaidi. Karibu uangalie kipindi hiki na uende ukaweke mkakati ambao utainufaisha sana biashara. Haijalishi wateja ulionao ni wangapi, kitendo tu cha kuwa na wateja tayari ni fursa nzuri kwako kupata wateja wengi zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.