
Ndiyo, nimependa huduma yako na nipo tayari kulipia.
Waoh! Nimependa namna unavyoelezea bidhaa yako. Nipatie mbili tafadhali.
Nipe hii hapa, na hii hapa pesa yako!
Sentensi tajwa hapo juu ni moja ya maneno pendwa kila muuzaji anapenda kuyasikia wakati wa ukamilishaji. Kwa bahati mbaya siyo kila mteja yupo tayari kuyasema.
Sababu ni kwamba, “wateja wanachukia kuuziwa, lakini wanataka kununua”. Ndiyo maana, siyo rahisi na haijawahi kuwa rahisi kupata “ndiyo” ya mteja. Hasa mteja ambaye hujamjua vizuri kwa kina na yeye hajajua vema biashara yako.
Unahitaji ushawishi mkubwa sana katika hilo, iwe kumfanyia ufuatiliaji, utembeleaji au masoko elimishi. Kiujumla kuna mambo mengi unapaswa kuyafanya ili kuipata ndiyo ya mteja.
Tunasema, ndiyo kwa sababu kila mmoja kwenye mauzo anatamani kusikia neno hilo. Namna gani unaenda kupata jibu hilo? Hapa chini nimeweka baadhi ya mambo ya kuzingatia;
Moja; Kuanzisha mazungumzo na mteja.
Hapa unamfanya mteja aongee, akusikilize, akupende na ajisikie vizuri kuwa na wewe. Unachotakiwa hapa ni kumsikiliza, kutumia jina lake, lugha ya ishara na kufungua nafasi ya mazungumzo zaidi na mteja wako.
Mbili; Ainisha mahitaji na maumivu ya mteja.
Hapa ndipo nafasi ya maswali inapata nafasi. Maswali mazuri kuuliza ni ya kujielezea (Open ended questions). Kisha, unakuwa mtulivu wakati mteja anajielezea. Endelea kuonyesha shauku na tabasamu wakati wa mazungumzo yako. Muulize zaidi, unaweza kunielezea kidogo kuhusu hiki? Hii inategemea na kitu alichozungumza.
Tatu; Mpe suluhisho kwa thamani kubwa.
Hapa unamwonyesha mteja kwa kiasi gani bidhaa au huduma yako inaenda kutibu maumivu yake. Hasa kupitia kuonyesha thamani kubwa anayoenda kupata kutokana na matumizi ya bidhaa yako. Ainisha baadhi ya “point” kwamba, utapata hiki au kile ndani ya muda fulani. Malizia kumpatia ushuhuda. Fulani ametumia bidhaa hii na sasa hivi yupo vizuri. “Network marketing” wanatumia sana hii njia.
Nne; Jibu mapingamizi ya mteja.
Mapingamizi ni sehemu ya maisha katika mauzo. Hivyo, yanapojitokeza usiwe na wasiwasi ni sehemu ya mchakato. Unachotakiwa ni kusikiliza vizuri kila aina ya pingamizi na kulitolea maelezo zaidi. Akisema bei ni Kubwa, ubora, kupelekewa, mwenza na lingine sikiliza na mjibu vema.
Mfano, akisema siwezi kumudu bei, mwambie usiwe na wasiwasi. Ukiachana na pesa kuna kitu kingine kinachokuzuia kufanya maamuzi? Akisema hapana. Tayari, pingamizi ni pesa. Mpe punguzo au bidhaa ya kati au chini.
Tano; Kamilisha Mauzo.
Kama ingekuwa ni mpira wa mguu, huu ndiyo wakati wa kufunga goli. Umewapita mabeki wote umebaki na nyavu. Weka mpira golini.
Kama muuzaji hapa ndipo mteja anakupa ndiyo na kuwa tayari kulipia. Japo eneo hili wauzaji wengi tumekuwa hatulitendei haki. Badala ya kulifanya mwishoni, tunalifanya katika hatua za awali. Namna nzuri hapa ni kutumia mauzo ya kudhania, kumpatia uhaba, ofa na njia zingine nyingi lengo ni kumfanya mteja kuchukua hatua na kulipia.
Ukifuta hatua hizi, kuna namna fulani utapata ndiyo nyingi kutoka kwa wateja wako na kukuza mauzo yako.
Kumbuka; Mauzo sio kumlazimisha mteja kulipia, bali ni kumsaidia mteja kufanya maamuzi sahihi ya kulipia.
Je, unakwama wapi katika kupata ndiyo ya mteja? Share na sisi hapa hapa.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz