Rafiki yangu mpendwa,
Maneno mjasiriamali na mfanyabiashara yamekuwa yanatumika kirahisi sana. Kila ambaye anauza vitu kwa watu huwa anajipachika majina hayo, bila hata kujua maana yake kamili.
Kununua na kuuza haitoshi kukufanya wewe uwe mjasiriamali au mfanyabiashara. Wengi wanaofanya hivyo ni wachuuzi, ambao kwa miaka mingi wanakuwa pale pale na hawapigi hatua. Kinachowazuia wachuuzi wasipige hatua ni hawajengi kitu kiwe kikubwa, bali wanachotaka ni kuingiza kipato cha kuendesha maisha yao. Hivyo wakishapata hicho kipato, wanakuwa wameridhika.
Rafiki, leo nitakuambia kuhusu mfanyabiashara na mjasiriamali nitakuambia siku nyingine. Lakini wakati unasubiria nije kukuambia kuhusu mjasiriamali, endelea kupata na kusoma kitabu nilichoandika kinachoitwa MJASIRIAMALI MJANJA ili ujifunze kwa kina. Unakipata kwa kuwasiliana na namba 0678 977 007.

Sawa, turudi kwa mfanyabaishara, je huyu ni mtu gani? Mfanyabiashara ni mtu anayejenga biashara ambayo inajiendesha yenyewe bila ya kumtegemea mwanzilishi au mmiliki moja kwa moja. Yaani biashara inaweza kujiendesha na kuingiza faida hata kama mmiliki wake hayupo moja kwa moja. Na ili kufikia ngazi hiyo, lazima kazi ya kutosha iwekwe.
Kuna vitu vingi vinahusika kwenye kujenga biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila kumtegemea mwanzilishi wake moja kwa moja. Moja ni kuwepo kwa maono makubwa ambayo yanafanyiwa kazi. Mbili ni kuwepo kwa mfumo wa kuiendesha biashara hiyo ambao unafuatwa. Na tatu ni kuwepo kwa timu inayoendesha biashara hiyo.
Kwenye somo hili, tunaenda kuangalia ujenzi wa timu bora ambayo itaiwezesha biashara kuwa na mafanikio makubwa. Hapa ndipo wengi wanapokwama, kwa sababu kupata watu sahihi wa kuweza kujenga biashara imekuwa ni changamoto. Pamoja n hiyo kuwa changamoto, bado watu wazuri wapo na kazi ikifanyika, wanaweza kupatikana.
Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia kwenye kujenga timu ya biashara, ambayo ni kama yafuatayo.
Jambo la kwanza ni mwanzilishi wa biashara kuwa mtu sahihi. Ili upate wafanyakazi sahihi kwenye biashara yako, lazima wewe mwanzilishi na kiongozi uwe sahihi. Kwa sababu hupati watu unaostahili, bali unapata watu unaowavumilia. Hivyo unapaswa kuwa na viwango vya juu kabisa ambavyo wewe mwenyewe unaviishi kwa uhalisia. Na hilo litawafutia wale sahihi kuja kwako. Watu huwa hawasikii yale wanayoambiwa, ila wanaiga yale yanayofanyika, kwa chochote unachotaka timu yako ifanye kwenye biashara yako, lazima wewe uwe mfano wa kwanza kwenye kukifanya.
Jambo la pili ni kujenga utamaduni mzuri kwenye biashara yako. Utamaduni ni namna ya kufanya mambo kwenye eneo husika, ambayo imezoeleka. Ni sheria ambazo kila mtu anazifuata, japo hakuna mahali ambapo zimeandikwa. Kila mahali huwa kuna utamaduni wake, hivyo pia kwenye biashara. Kwenye biashara yako tayari kuna utamaduni, hata kama siyo wewe umeujenga. Na huo utamaduni huwa una nguvu sana kwa watu, kwani hata wakija watu ambao ni wa tofauti, utamaduni huwa una nguvu ya kuwabadili au kuwafanya washindwe kuendelea. Unapaswa kujenga utamaduni ambao unatoa fursa kwa watu sahihi kukua na kuwaondoa wale wasio sahihi. Hili ni zoezi linalohitaji kazi kubwa kufanya na kwa mfano.
Jambo la tatu ni kuchagua watu sahihi wa kuwa kwenye timu yako. Huwa tunaona shule zinazofaulisha sana zikichagua wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kufaulu. Timu zinazoshinda huwa zinachagua wachezaji bora. Halafu wewe unataka ujenge biashara yenye mafanikio makubwa kwa kuokoteza tu watu, hilo haliwezekani. Ni lazima uchague watu sahihi, wenye uwezo na tabia nzuri. Uwezo na tabia ni vitu ambavyo huwezi kuwafundisha watu, hivyo lazima viwepo wakati unawaajiri. Jinsi ya kufanya majukumu ya kazi unaweza kuwafundisha, lakini siyo tabia au uwezo. Hivyo hakikisha hivyo wanavyo kabla hujawaingiza kwenye timu yako.
Haya ni matatu ya msingi kuzingatia kwenye kujenga timu bora ya biashara, yapo mengine matatu ambayo nimeyaelezea kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu ujifunze mambo hayo na ukayafanyie kazi ili ujenge biashara yenye mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.