Tunapozungumzia maslahi tunamaanisha mahitaji ya mtu. Yaani, kile anachohitaji kutoka kwenye huduma yako. Mfano, unafanya kazi ili upate pesa. Kwenye kazi, pesa ndiyo maslahi yako, ndiyo hitaji lako kuu.

Unauza ili upate pesa, ikiwa mteja anakuja na pesa ndogo tofauti na unachouza unasema; kwa kiasi ulichonacho maslahi hayapo, hakuna maslahi ninayopata. Kinachofanya useme hivyo ni kwa sababu unaona utapata hasara.

Weka akilinini kuwa, kila mtu kuna kitu anapenda zaidi. Mfano hapo umeshika simu yako, ambayo umenunua kwa taabu. Halafu mtu aichukue na kuidondosha chini. Kuna ugomvi utaibuka hapo, hutotaka hata kumsikiliza. Unajua kwa nini? Kwa sababu simu yako unaipenda na kuijali zaidi. Maana kupitia simu unapata mambo mengi zaidi.

Ipo hivyo hata kwenye maisha, kila mtu kwenye maisha yake kuna vitu ambavyo anavipenda na kuvijali zaidi. Hilo ni jambo ambalo lipo kwa kila mtu, ambalo linaweza kuchochewa na mazingira, imani na mitazamo ambayo watu wanakuwa nayo. Watu huwa tayari kufanya chochote kwa ajili ya yale wanayoyapenda na kuyajali kwa sababu ndiyo yanajenga maana kwenye maisha yao.

Uwepo wa vitu ambavyo watu wanapenda na kujali ndiyo unayafanya maisha yao kuwa na maana. Ndiyo maana watu huwa tayari kuvipigania vitu hivyo, kwa sababu visipokuwepo, maisha yao yanaonekana kukosa maana. Wajibu wako mkubwa kwenye mauzo ni kujua mtu anapenda na kujali nini zaidi ambacho kinahusiana na kile unachouza.

Hii ni kazi inayohitaji uwe msikilizaji mzuri kwa wateja na kuwahoji maswali. Ili kujua maslahi ya mteja kwanza jua kabisa unayeongea naye, ni mfanyakazi, fundi, meneja, au mkurugenzi. Kisha yazingatie haya;

Moja; Mfanye aongee zaidi.
Kupitia kuongea ni rahisi mtu kufichua yaliyo katika moyo wake. Hali inayofanya ujue mahitaji yake na kumshawishi ili kumfanya kwa rafiki. Naamini unalijua pembe la ng’ombe, huwa halifichiki. Hata jua literemke, ng’ombe avae kofia ngapi, pembe litaonekana tu.

Hivyo, ukizungumza na mtu kwa muda na kuweka umakini mkubwa kumsikiliza, huku ukimuuliza maswali, kile anachopenda na kujali kitajidhihirisha wazi kabisa. Hali itakayokusaidia kumsogeza karibu yako na kujenga naye urafiki na hatimaye kumuuzia.

Mbili; Ongea na wateja kupitia lugha yao.
Hapa unaangalia mteja wako anaongea kuhusu nini. Inaweza kuwa faida, hasara, delivery, kulijua soko na mengine mengi.

Hii utajua kupitia mazungumzo kwenye mazungumzo anayofanya, utasikia anasema; ninakwama katika kukamilisha mauzo, kuendana na kasi ya soko au gharama ni kubwa ukilinganisha na kinachoingia.

Maelezo yako yanapitia humo na mteja anaona mpo pamoja. Sisi binadamu ni viumbe wa hisia, tunapenda kuwa karibu na watu wanaotujali na kutusikiliza.

Tatu; Kuwa Mwalimu na siyo muuzaji.
Kwa kawaida wateja hawataki kuuziwa. Wanapenda kuona wanafikia maamuzi ya kununua wao wenyewe. Kwa lugha nyingine, wateja wanapenda kujifunza vitu vipya. Wajibu wako ni kuwasaidia wateja kuiona dunia katika mwanga tofauti. Kuona uwezekano wa kitu na mengine mengi.

Nne; Tumia hadithi na mifano.
Kwenye biashara na maisha kiujumla “Vitu husahaulika haraka, lakini hadithi inakumbukwa”.  Hadithi inaleta urahisi wa mteja kuelewa zaidi na kuwa msikilizaji mzuri.

Lengo kuu la hadithi ni kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha. Hapa unaelezea kiufupi mambo machache uliyopitia hadi kufika hapo. Madhumuni makuu ni kumfanya mteja aone uwezekano wa kitu. Wakati mwingine unaongea na mteja anayeona mambo magumu, ukimpa hadithi anaona umemjali zaidi na kufanya achukue hatua zaidi.

Baada ya kuyajua maslahi ya mteja, kinachofuata ni wewe kukamilisha au kumpa hatua zinazofuata. Muhimu zaidi ni kuendelea kuwa karibu naye(keep in touch) pamoja na kuongeza thamani katika biashara yake.

Je, unajali na kugusia maslahi ya wateja wako?

Imeandaliwa na Lackius Robert, Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.