3334; Haifanyi kazi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Pamoja na uwepo wa mafunzo na ushauri mwingi wa mafanikio, bado mafanikio yamekuwa magumu kwa walio wengi.
Hiyo ni kwa sababu bado kuna uhitaji wa kufanya maamuzi sahihi kwenye uhalisia.
Na maamuzi mengi huwa hayana machaguo yaliyo wazi, bali yanakuwa yamechanganyana.
Kwa mfano, mafunzo na ushauri mwingi wa mafanikio inaeleza umuhimu wa ung’ang’anizi kwenye kile ambacho mtu anafanya ili kufanikiwa.
Wengi wanaweza kuchukulia ung’ang’anizi kwa namna isiyo sahihi na wakapoteza sana badala ya kupata.
Kama kuna mahali unapita na unagonga kichwa kwenye ukuta, kuendelea kupita na kugonga kichwa siyo ung’ang’anizi, bali ni ukaidi.
Haijalishi utagonga kichwa chako mara nyingi kiasi gani, utaishia kuondoka na maumivu kuliko kupata kile unachotaka.
Sasa basi, ugumu wa mafanikio unakuja kwenye kufanya maamuzi, wapi ni ung’ang’anizi na wapi ni ukaidi?
Haya siyo maamuzi rahisi kufanya na ndiyo maana wengi bado hawafanikiwi.
Wengi wanaishia kufanya maamuzi kwenye kingo mbili za kuacha haraka au kuendelea licha ya maumivu.
Wakati maamuzi sahihi ni mahali fulani katikati ya kuacha na kuendelea.
Na hapo ndipo kinakuja kigezo kingine kwenye ufanyaji wa maamuzi.
Kigezo hicho ni kupima kitu kama kinafanya kazi au hakifanyi kazi kabla ya kuendelea na ung’ang’anizi.
Kigezo hiki cha ufanyaji kazi ni muhimu kwa sababu ndiyo kitakupa mwongozo iwapo uendelee kufanya au uache.
Mafanikio ni pale unapong’ang’ana na kitu ambacho kinafanya kazi. Kitu kinakuwa kwenye misingi sahihi na kinachokuwa kinahitajika ni muda wa kutosha wa kukifanya mpaka kupata matokeo.
Kushindwa ni pale unapong’ang’ana na kitu ambacho hakifanyi kazi. Unachokuwa umekariri ni ung’ang’anizi wa kuendelea, lakini hauna tathmini sahihi ya namba inayokuonyesha uwezekano wa matokeo sahihi. Kinachotokea ni unakuwa unazidi kupoteza kadiri unavyoendelea na ung’ang’anizi.
Kwa chochote unachofanya, ni muhimu uwe unajitathmini na kuona kama bado upo kwenye njia sahihi na kinafanya kazi kabla hujaendelea kung’ang’ana zaidi na zaidi.
Pale hesabu zinapokataa kabisa, yaani kitu hakifanyi kazi, ni wakati wa kufanya maamuzi ya kuacha na kwenda kwenye kitu kingine kinachofanya kazi.
Hapo unakuwa hujakata tamaa au kuishia njiani, bali unakuwa umeiboresha safari yako ili usizidi kupotea.
Kwa mfano kama muundo na mpango wa biashara ni mbovu na hivyo kupelekea kupata hasara, haijalishi utang’ang’ana kiasi gani, utaishia kupata hasara kubwa kama hutabadilika.
Ni lazima uwe unajitathmini, ujionee wazi kama kuendelea kuna namna matokeo yatakuwa bora zaidi. Au kuona kama ni bora kukubali hasara ambayo umeshaingia na kuacha ili usiingie hasara kubwa zaidi.
Watu wasioweza kufanya maamuzi sahihi, hujikuta wakiingia hasara kubwa sana kwa sababu wanakuwa hawapo tayari kukubali hasara ndogo.
Rafiki, kumbuka mafanikio ni safari ya muda mrefu, safari ya maisha yako yote. Haina haja ya kuongeza kasi wakati haupo kwenye njia sahihi.
Sehemu kubwa ya safari yako ni kupima kama upo kwenye njia sahihi na kufanya maamuzi sahihi.
Hilo halitakuwa zoezi rahisi, lakini ni lenye tija kwenye kuzalisha matokeo bora kabisa.
Kukubali kwamba umekosea na kufanya marekebisho mapema ni kuzuia usiingie kwenye hasara kubwa.
Kushupaza shingo na kuendelea na njia ya upotevu ili kuonyesha una ung’ang’anizi ni kutengeneza hasara kubwa ambayo itakupoteza kabisa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kila mwanachama anajijenga na kuwa bora kwenye ufanyaji wa maamuzi kadiri ya anavyokwenda.
Anayatumia maarifa anayopata na hatua anazochukua kujitathmini na kuona ni kipi sahihi kufanya ili kupata kile anachotaka kwa uhakika.
Mwisho wa siku, mafanikio kwa mtu ni yeye kupata kile anachotaka hasa, kufika kule anakotaka kufika.
Hilo linamtaka afanye maamuzi mengi ya kuboresha safari yake nzima kuliko tu kuongeza kasi.
Kuwa ndani ya jamii hii inakusaidia kufanya maamuzi bora zaidi, kwa sababu pia unapata nafasi ya kujifunza kwa wengine ambao nao wapo kwenye safari ya mafanikio kama yako.
Hivyo huhitaji kurudia makosa ambayo tayari wengine wameshayafanya.
Kabla hujaongeza kasi kwenye safari yoyote uliyopo, hakikisha kwanza upo kwenye njia sahihi.
Kwani ukiwa kwenye njia ya upotevu, kila kasi unayoongeza unazidi kupoteza zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe