Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya falsafa zetu za mauzo kwenye CHUO CHA MAUZO ni MAUZO NI MCHEZO WA NAMBA. Falsafa hii inarahisisha msingi mkuu wa mauzo ambao ni ukiweza kuwafikia watu wengi zaidi, utaweza pia kufanya mauzo makubwa zaidi.
Tunaposema mauzo ni mchezo wa namba, ni sawa na kurusha matope kwenye ukuta, kadiri unavyorusha matope mengi, kuna ambayo yatanasa. Kwenye mauzo, kadiri unavyowafikia wateja wengi, ndivyo utakavyokutana na ambao wapo kwenye uhitaji wa kununua.

Na hilo linadhihirishwa kabisa na tafiti mbalimbali ambazo zimewahi kufanywa, mojawapo ikiwa ni ya soko kubwa. Utafiti huo unaonyesha kwamba kwenye soko lolote lile, asilimia 3 wana uhitaji wa kununua sasa, asilimia 17 wanafanya utafiti wa kununua, asilimia 20 wana uhitaji lakini hawanunui sasa na asilimia 60 hawana mpango wowote wa kununua.
Matangazo mengi yanayofanywa, huwa yanalenga ile asilimia 3 ambao wapo kwenye uhitaji wa kununua sasa. Hili ndiyo limekuwa linaleta ushindani mkali sokoni, kwa sababu biashara nyingi zinawagombania wateja wachache.
Kuondoka kwenye huo ushindani, unapaswa kuwa na mkakati wa masoko na mauzo ambao unawagusa wateja kwenye makundi yote. Unawagusa wale walio kwenye uhitaji wale walio kwenye hali ya kununua sasa na wale wanaojipanga kununua.
Unaweza kutimiza hilo kama utawafikia wateja wengi zaidi kila siku. Lakini swali la msingi ni je wengi ni kiasi gani? Kwa sababu kwa mtu ambaye hafikii wateja wengi, anaweza kuona ongezeko fulani ni wateja wengi.
Ili kwenda vizuri na namba, kila muuzaji anapaswa kuwafikia wateja wasiopungua 100 kila siku. Ndiyo, namba 100 ndiyo nzuri kwa kila muuzaji kuifikia ili kuwa na ufuatiliaji mzuri wa wateja na wenye ushawishi.
Wengi wanaposikia kuwafikia wateja 100, huwa wanaona ni namba kubwa sana na ambayo haiwezi kufikiwa. Lakini hilo siyo kweli, kila muuzaji anaweza kufikia wateja wasiopungua 100 kila siku kama akiwa na mkakati mzuri wa kufanya hivyo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina jinsi kila muuzaji anavyoweza kufikia wateja hao wasiopungua 100 kila siku. Karibu uangalie kipindi hicho, ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili kufikia wateja wengi na kufanya mauzo makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.