Habari Wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye masomo ya mauzo, kwenye eneo la ushawishi. Kauli mbiu yetu kuu ni kwenye maisha hupati kile unachostahili, bali kile unachoshawishi.

Na hakuna mahali kauli hiyo inajidhihirisha kama kwenye mauzo. Mfano mzuri, unaweza kuwa na bidhaa au huduma ambayo ni bora sana, na ukawa na bei nzuri kuliko wauzaji wengine, lakini bado wateja wakakataa kununua kwako. Cha kushangaza sasa, wanaenda kununua kwa wauzaji wengine ambao bidhaa au huduma zao siyo bora na bei zao ni kubwa.

Unaweza kutoa maneno mengi uwezavyo kuhusu wateja na wauzaji hao, ukisema hawajielewi na mengine yanayokufanya ujisikie vizuri. Lakini unachotakiwa kujua ni kwamba kwenye haya maisha, wanaopata kile wanachotaka ni wale wenye ushawishi. Hivyo ili uweze kufanya mauzo makubwa, ambalo ndiyo lengo linalotuleta pamoja, lazima uwe na ushawishi mkubwa.

Kwa kifupi, ushawishi ni kupata NDIYO nyingi kuliko HAPANA. Hapo ni watu, kwa ridhaa zao wenyewe, wakupe wewe kile unachotaka, kutokana na namna ulivyowafanya waone hilo ndiyo sahihi kwao kufanya.

Kwenye majadiliano ya aina yoyote ile, anayekuwa na nguvu ya ushawishi na kuweza kupata NDIYO ni yule ambaye anakuwa na machaguo mengi kuliko mwingine. Hii ndiyo kanuni kuu ya majadiliano na ushawishi ambayo unapaswa kuielewa na kuitumia mara zote ili uweze kupata NDIYO nyingi zaidi kuliko hapana.

Kwa kifupi, kuongeza nafasi ya wewe kupata NDIYO, hakikisha unakuwa na machaguo mengi zaidi. Kadiri machaguo yanavyokuwa mengi kwako, ndivyo unavyokuwa na nguvu kubwa ya ushawishi na kuweza kupata kile unachotaka.

Kama muuzaji unapaswa kuongeza machaguo yako kwenye ngazi tatu za mauzo.

Ngazi ya kwanza ni kwenye thamani ambayo unaitoa kwa wateja.

Kwenye ngazi hii, unapaswa kutoa thamani kubwa zaidi kwa wateja wako kuliko gharama ambayo wanaingia. Unapaswa kuwaeleza wateja manufaa wanayokwenda kupata kwa kununua kile unachouza. Eleza manufaa yote, hata yale unayoona ni ya kawaida na kila mtu anayajua.

Kwenye ngazi hii, penda kutumia orodha, mfano; hizi ndizo faida tano za kununua …. Kadiri unavyoorodhesha manufaa mengi ndivyo watu wanavyoona thamani ni kubwa na kuwa tayari kusema ndiyo.

Pale mteja anapokuambia bei yako ni ghali, usikimbilie kwanza kupunguza, bali mkumbushe thamani kubwa anayokwenda kuipata. Mworodheshee manufaa yote anayoenda kupata, ukilinganisha na gharama anayotakiwa kulipa.

Nisisitize sana hili maana wauzaji wengi wamekuwa wanalichukulia poa, wanaona tayari wateja wanajua sifa na manufaa ya kitu, lakini utashangaa wanaenda pengine wanaambiwa hayo mambo na kuona hayapatikani kwingine. Ninachomaanisha ni hata kama akienda kununua kitu hicho kwa wauzaji wengine anapata manufaa hayo hayo, wewe waeleze bila kuacha. Utaongeza sana nafasi ya kupata NDIYO.

SOMA; Jinsi Ya Kutumia Silaha  Ushawishi Ya Uhaba Kuongeza Mauzo Zaidi

Ngazi ya pili ni kwenye huduma unayowapa wateja.

Kila mmoja wetu anajua biashara ambazo zinafanana, zipo eneo moja, zinazua kitu cha aina moja, lakini biashara moja inakuwa na wateja wanaosubiri kwenye foleni kuhudumiwa, wakati biashara nyingine haina watu kabisa. Nini kinasababisha hayo? Jibu ni moja, huduma bora na ya kipekee ambayo wateja wanaipata kwenye ile biashara wanayokuwa tayari kusubiri kwenye foleni.

Hilo ni eneo ambalo wewe unapaswa kulifanyia kazi ili kuongeza nafasi ya kupata NDIYO nyingi zaidi kutoka kwa wateja kuliko kupata HAPANA. Nenda hatua ya ziada katika kuwajali na kuwahudumia wateja wako kiasi cha wao kuwa tayari kurudi kwako mara zote. Na siyo tu kurudi, bali pia kuwaambia wengine nao waje kupata huduma.

Jitoe hasa kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na ambayo inawashangaza, waahidi mambo mazuri, halafu kwenye kutekeleza nenda zaidi ya ulivyoahidi. Wafanye wateja waone kama wana deni kubwa kwako kutokana na huduma ya kipekee ambayo unawapatia.

Unapotoa huduma bora na ya kipekee kabisa, unakuwa wa kipekee, hivyo wateja wengi wanakuwa wanakutaka wewe, kitu kinachoongeza NDIYO kwa upande wako. Lakini ukitoa huduma mbovu au ambayo ni ya kawaida, unakuwa sawa na wafanyabiashara wengi na hivyo mteja kuwa na machaguo mengi, kitu kitakachokupa wewe HAPANA nyingi zaidi.

Chagua kuwa upande wa kipekee, ili wateja wengi wawe wanataka kufanya biashara na wewe, badala ya wewe kuwa ndani ya kundi la wafanyabiashara wengi ambapo mteja anachagua anunue kwa nani na aache kwa nani. Ukishawekwa kwenye kundi kubwa la wafanyabiashara wengi, nafasi ya NDIYO inakuwa ndogo na HAPANA kuwa kubwa.

Ngazi ya tatu ni kwenye wingi wa wateja unaokuwa nao.

Hapa tunarudi kwenye falsafa yetu ya mauzo ni mchezo wa namba. Kama una wateja wachache na wote wakasema HAPANA, unaishia kukosa mauzo. Lakini unapokuwa na wateja wengi, haiwezekani wote wakasema HAPANA, kuna ambao watasema NDIYO na hapo utapata mauzo.

Hivyo basi, kuongeza nafasi yako ya kupata NDIYO zaidi kwenye mauzo, hakikisha mara zote unakuwa na wateja wengi zaidi. Ni wajibu wako kila wakati kama muuzaji kuwa unatengeneza wateja wengi zaidi. Kamwe usifike mahali na kuona tayari una wateja wa kutosha na huhitaji kutafuta wengine.

Zoezi la kutafuta wateja wapya ni la kufanya mara zote. Lengo ni uwe na wateja wengi sana kiasi kwamba hauwezi kukosa kabisa mauzo. Kuna nyakati ambazo mauzo yanaweza kuwa chini, nyakati ambazo wateja wengi watashindwa kununua. Hizo ndizo nyakati ambazo kuwa na wateja wengi zaidi kutakuokoa, kwa sababu kuna wachache watakaonunua.

Unaweza kuwa unajiuliza ni wateja wengi kiasi gani unaopaswa kuwa nao. Na jibu ni mara 10 ya wale unaoona ndiyo kikomo kwako kuweza kuwahudumia. Mara zote hakikisha unakuwa na wateja wengi zaidi ya unavyoweza kuwahudumia ili usikose mauzo.

Hilo litakupa kazi ya ziada, kwa sababu umeshajifunza kwamba inabidi uwape wateja wako huduma bora zaidi. Sasa ukiwa nao wengi utawezaje kuwahudumia? Hiyo ndiyo kazi yako kama muuzaji, kuwa na wateja wengi na wahudumie vizuri kama ambavyo umewaahidi.

Rafiki yangu muuzaji, hayo ndiyo maeneo matatu ya wewe kuongeza nafasi ya kupata NDIYO zaidi ili kukuza mauzo. Toa thamani kubwa, toa huduma ya kipekee na kuwa na wateja wengi zaidi. Ukifanyia kazi hayo matatu, utakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi na wateja watakuwa wanakugombania wewe badala ya wewe kuwagombania wateja.

Utajisikiaje pale wateja wanapokuwa wanakugombania wewe? Vizuri sana, si ndiyo? Basi habari njema hilo lipo ndani ya uwezo wako, fanyia kazi mambo haya matatu uliyojifunza hapa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.