Rafiki yangu mpendwa,
Ushauri maarufu uliopo kwenye tasnia ya mafunzo na ushauri wa mafanikio ni mtu kujifanyia tathmini ili ujue uimara (strength) na madhaifu (weakness) yako. Hili ni zoezi muhimu sana ambalo kila anayetaka kufanikiwa lazima alifanye.
Sehemu ya pili ya ushauri huo ndiyo imewapoteza wengi kuliko kuwasaidia. Kwani sehemu hiyo inasema mtu unatakiwa kukazana kujiimarisha kwenye yale maeneo ambayo una udhaifu ili uondokane na madhaifu yako na uwe imara kwenye maeneo yote.

Ushauri huo hapo, ambapo umeshausikia mara nyingi na kufundishwa maeneo mengi umewapoteza watu wengi na kuwazuia kufanikiwa.
Unajua ni kwa nini? Kwa sababu unapofanyia kazi madhaifu yako ili kuyaondoa na yawe ni uimara kwako, unaishia kuwa na madhaifu ambayo ni imara zaidi. Yaani unayaongezea madhaifu hayo nguvu ya kuwa kikwazo kwako.
Juhudi zozote ambazo mtu ataweka kwenye kubadili madhaifu yake kuwa uimara huwa zinaishia kumkwamisha, kwani anakuwa na madhaifu imara. Na mbaya zaidi ni yale maeneo ambayo tayari alikuwa imara nako anakuwa dhaifu, kwa sababu mtu anakuwa hajayapa nguvu za kutosha.
Hivyo basi rafiki, ushauri unaohitaji siyo wa kufanyia kazi madhaifu yako, bali unapaswa kuyapuuza kabisa madhaifu uliyonayo. Unachopaswa kufanya ni kupeleka juhudi zako zote kwenye yale maeneo ambayo una uimara. Hayo ndiyo maeneo ambayo ukiyawekea nguvu utaweza kuzalisha matokeo makubwa.
Maeneo ambayo tayari una uimara, ukiendelea kuyawekea nguvu, utazidi kuwa imara na kupata nguvu kubwa ya ushindani ambao unakupa mafanikio makubwa. Ukiweka nguvu kwenye maeneo ambayo una udhaifu, unakutana na watu ambao wana uimara kwenye madhaifu hayo na wewe hutakuwa na nguvu ya ushindani.
Nirudie tena kwa msisitizo rafiki yangu, peleka juhudi zako kwenye yale maeneo ambayo tayari una uimara, huku ukiyapuuza kabisa yale maeneo ambayo una madhaifu. Usijaribu hata kidogo kubadili madhaifu yako kuwa uimara, utapoteza hata uimara ulionao.
Swali zuri unaloweka kuwa nalo ni je unayafanyaje madhaifu ili yasiwe kikwazo kwenye mafanikio unayoyajenga? Hilo ni swali zuri sana na ambalo nimeeleza majibu yake kwa kina kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu usikilize kipindi hiki ili ujifunze kwa kina nini cha kufanya kwenye uimara na madhaifu yako ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.