Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, huwa tunapenda kuwa ndani ya jamii na kukubalika na wale walio kwenye jamii hizo. Hivyo tumekuwa tunatumia muda na juhudi kubwa kutaka kupendwa na kukubalika na wengine.
Lakini pamoja na juhudi kubwa tunazoweka ili wengine waweze kutupenda na kutukubali, bado matokeo tunayoyapata ni tofauti kabisa na tuliyotegemea. Kwani kumekuwa na watu ambao wanatuchukia bila hata sababu za msingi.
Hilo limekuwa linatushangaza, kwa sababu hatuelewi kwa nini pamoja na yote mazuri tunayokuwa tunakazana kufanya, kuna watu wamechagua kutuchukia. Kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, hili na jambo unalopaswa kulielewa na kulichukulia jinsi lilivyo.

Watu wote wanaokuzunguka na kukujua kwenye maisha yako wamegawanyika kwenye makundi matatu.
Kundi la kwanza ni watu ambao watakupenda bila ya kujali umefanya nini. Hawa watakupenda tu, hata kama unafanya mambo mabaya, bado watu hao watakupenda. Hawa ni wale ambao una mahusiano nao ya karibu na wanajali kuhusu wewe.
Kundi la pili ni watu ambao watakuchukua bila ya kujali umefanya nini. Hawa watakuchukia tu, hata kama unafanya mambo mazuri na yenye manufaa. Watu hao watakuwa na kila sababu ya kukuchukia wewe na yale unayoyafanya. Hawa ni wale ambao wana ushindani na wewe kwa namna moja au nyingine.
Kundi la tatu ni watu ambao hawajali sana nini unafanya, hawa hawakupendi na wala hawakuchukii. Kwa kifupi hawa hawana muda na wewe, hawajali sana unafanya nini. Ukiwa nao wanakupa ushirikiano, ukiachana nao wanakusahau. Hawa wanahangaika na mambo yao na hawana nafasi ya kujihusisha na mambo yako.
Makundi haya matatu yanaweza kuwa na idadi sawa ya watu, lakini cha kushangaza, huwa tunaweka uzito kwenye kundi la wale wanaotuchukia na kusahau wengi ambao wanatupenda.
Chukua mfano umezungumza mbele ya watu 100, watu 99 wakakupigia makofi na kukushukuru kwamba umesema mambo ya msingi. Halafu mtu mmoja akakufuata na kukuambia umeongea ujinga mtupu na hakudhani una ujinga kiasi hicho. Utakapotoka hapo utakuwa unafikiria nini zaidi? Utasahau kabisa watu 99 ambao wamekupenda na kumfikiria mmoja ambaye amekuchukia.
Hilo siyo sawa kabisa, unakuwa unajiumiza kwa jambo lisilokuwa sahihi.
Unachotakiwa kujua ni kwamba wapo watu watakaochagua kukuchukia bila kujali umefanya nini. Na watakuchukia siyo kwa sababu yako, bali kwa sababu zao wenyewe. Hivyo usiruhusu hilo likukwamishe kwenye yale unayoyafanya.
Lakini zaidi, unaweza kutumia hali ya watu kukuchukia kwa manufaa zaidi. Kwa sababu kunapokuwa na wanaokuchukia pia kunakuwa na wanaokupenda, unaweza kutumia wanaokuchukia kuwafikia ambao watakupenda.
Hapa unachopaswa kufanya ni kuhakikisha unawaudhi wengi wanaokuchukia. Kwa kile unachofanya na watu wakakuchukia kwa hicho, kifanye kwa wingi na ukubwa zaidi na hakikisha wote wanaokuchukia kwa hicho wanakujua. Kwa kadiri watu wengi wanavyokuchukia ndivyo wanavyosambaza habari zako na hivyo kuweza kuwafikia wengi zaidi.
Wale wanaokuwa wanakuchukia wanakuwa ni watu wazuri sana kukutangaza na ukajulikana na wengi zaidi. Hayo ni matangazo ya bure ambayo huyalipii chochote. Kwani kwa chuki ambazo watu wanakuwa nazo, watasema mambo yako kwa wengi zaidi na kati ya hao kuna ambao watakujua na kukupenda kwa hayo unayofanya.
Kufanya hivyo kunakutaka uwe na ngozi ngumu ya kuvumilia mashambulizi ambayo hao wanaokuchukia watayafanya kwako. Na hilo litakuwezesha kufanya makubwa zaidi.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina jinsi ya kutumia hali ya kupendwa na kuchukiwa ili kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.