Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli ya Kiswahili inasema; mwanzo ni mgumu. Ni kauli inayobeba ukweli mkubwa kwa sababu mwanzo wa kitu chochote kile, mtu unakuwa huna uelewa wa jinsi kinavyopaswa kufanyika. Na hata kama mtu umejifunza, bado unakuwa huna uzoefu wa kufanya kitu chenyewe. Hiyo ni kwa sababu nadharia na uhalisia ni vitu viwili tofauti.

Mwanzo wa biashara yoyote huwa ni mgumu sana kwa sababu inakuwa haina wateja na hivyo mauzo kuwa magumu. Tunajua bila wateja hakuna mauzo na biashara inapoanza, inakuwa haina wateja. Na hata baada ya biashara kuanza, siyo kwamba wateja watakimbilia kuja kununua, bado itachukua muda kwa wateja kujengeka kwenye biashara.

Kinachofanya ichukue muda kwa biashara kujenga wateja ni imani. Kikwazo cha kwanza kwa wateja kununua ni imani. Wateja huwa hawanunui kama hawana imani. Na kwa biashara ambayo ni mpya, ambayo wao wenyewe hawajawahi kununua wala hawawajui watu wao wa karibu ambao wamewahi kununua, imani inakosekana.

Kundi kubwa la wateja huwa linasubiri kwanza kuona kama biashara itadumu kwa muda mrefu ndiyo waamini na kununua. Hiyo ni kwa sababu tayari wanakuwa wananunua mahali pengine na iwapo wataacha kununua huko na kwenda kununua kwenye biashara mpya, kama biashara hiyo haitadumu, watakuwa wameharibu uaminifu wao kule walipokuwa wananunua.

Hapo ndipo unapojikuta unapoanzisha biashara mpya au biashara ile ile kwenye eneo ambalo ni jipya. Wateja wanaweza kuwa na uhitaji, wanakuwa wanamudu kabisa kununua, lakini kwa kuwa bado hawana imani, wanasubiri waone namna utakavyokwenda.

Kwa bahati mbaya sana, wafanyabiashara wengi huwa wanakata tamaa haraka kwa kuona hakuna wateja, kumbe wateja wapo ila wanasubiri wapate imani. Na pale mfanyabiashara anapokata tamaa na kuacha, wateja wanaona walikuwa sahihi kutokununua kwa haraka.

Leo tunakwenda kujifunza njia rahisi na ya uhakika ya kupata wateja kwenye biashara mpya. Njia hiyo inahusisha kutumia imani ambayo tayari umeshajenga mpaka sasa kwa watu ili kupata wateja.

Tumeona kinachowazuia watu kununua ni kukosa imani, kwa sababu biashara ni mpya na hakuna wateja ambao wameshanunua. Unachofanya hapa ni kuwatumia watu ambao tayari wanakuamini kwenye maisha yako ya kawaida ili kupata wateja kwenye biashara yako mpya.

Zungumza na watu wako wote wa karibu ukiwaeleza biashara uliyoanzisha na kuwaomba wakupe mtu wanayemjua ambaye anaweza kunufaika na biashara yako. Ukifanya hivyo kwa watu wote ambao wanakujua na kukuamini, utapata wateja unaoweza kuanza nao.

Mpango huu unapaswa kuufanya kama ulivyo, usiwatake wao wanunue, bali waombe wakupe watu wanaowajua. Kwa kuwaomba wakupe watu, kama wao wenyewe pia wana uhitaji, watakuambia hata wao wanataka. Inabidi ufanye hivi ili kuondoa majuto ya kuwafanya watu wanunue. Watu wengi wanapoanzisha biashara mpya huwa wanawataka watu wao wa karibu wanunue na kuwafanya wajisikie vibaya kama hawatanunua. Hivyo baadhi wanaweza kununua siyo kwa sababu wana uhitaji, bali tu kukuridhisha.

Watu kununua kwenye biashara yako ili kukuridhisha haitakusaidia kitu, wewe unachotaka ni kujenga wateja wenye uhitaji ambao utawauzia kwa muda mrefu. Hivyo usiwafanye watu wanunue kwako kukuridhisha, bali waombe wakupe watu wenye uhitaji na kama wao wenyewe wana uhitaji, watakuambia.

Tayari unaaminika na watu wengi, tumia hiyo imani kupata wateja kwenye biashara mpya unayoanzisha. Na kwa kila wateja wanaonunua, wahudumie vizuri na uwatumie hao kuendelea kupata wateja wengine wengi.

Njia nyingine za kutangaza na kuwashawishi wateja utaendelea kuzifanyia kazi, kwa sababu hizo matokeo yake huwa yanaonekana baada ya muda mrefu. Ila njia hii ya kutumia wanaokuamini kupata wateja matokeo yake ni ya haraka, ifanyie kazi kwa uhakika.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeelezea njia hii kwa kina zaidi, karibu uangalie kipindi hapo chini, ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kujenga biashara yenye mafanikio.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.