Rafiki yangu mpendwa,

Kila mtu anataka kufanikiwa, lakini ni wachache sana ambao wapo tayari kulipa gharama inayotakiwa kulipwa ili wayapate mafanikio wanayoyataka. Wengi wamekuwa wanataka maisha yao yaendelee kama ambavyo yamekuwa yanaenda, lakini wapate mafanikio makubwa.

Moja ya vitu ambavyo wamezoea kufanya na vimekuwa kikwazo kwao kufanikiwa ni kukwepa kuwajibika. Kwa malezi ambayo tumepata na mazoea ya maisha, pale mambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea, huwa tunatafuta nani amesababisha hilo.

Huwa haitokei tukafika hatua ambayo tunakiri ni sisi wenyewe ndiyo tunaohusika na yote yaliyotokea kwenye maisha yetu. Na kwa bahati mbaya sana, watu au vitu vya kulaumu huwa ni rahisi kupatikana. Wazazi na serikali ni makundi ambayo yamekuwa yanabeba lawama kubwa pale watu wanapokwama kwenye mambo wanayotaka. Halafu hali ya uchumi na hali ya hewa pia ni vitu vimekuwa vinalaumiwa sana.

Msukumo wako wa kufanya chochote unachofanya huwa una mchango mkubwa sana kwenye matokeo ambayo unayapata. Japo kwa nje utaonekana unafanya, ila msukumo wa ndani huwa ni tofauti na hapo ndipo penye breki inayokuzuia kufanya makubwa.

Kuna watu kwa nje huwa wanaonekana wanaweka juhudi kubwa sana kwenye yale wanayofanya, wanaonekana wakichapa kazi sana, lakini matokeo wanayoyapata hayaendani na juhudi wanazoweka. Kwa kuwaangalia kwa nje huwezi kuelewa nini kinawakwamisha na hata wao wenyewe wanakuwa hawaelewi nini kinawakwamisha.

Hiyo ndiyo hali ya breki tunayoizungumzia, kwamba unachochea sana lakini hakuna mwendo, kwa sababu pia unakuwa umeshikilia breki. Ili juhudi unazoweka zilete mwendo, lazima kwanza uachilie breki ambazo umeshikilia.

Moja ya njia za kuachilia breki ni kuwajibika kwa kila kitu unachofanya na matokeo yanayotokea kwenye maisha yako. Na huu uwajibikaji tunaohitaji ili kuachilia breki siyo tu wa kuacha kulalamika na kulaumu, bali wa kubadili kabisa msukumo wa ndani wa kufanya yale tunayofanya.

Huwa kuna misukumo ya ndani ya aina tatu kwenye yale tunayofanya.

Moja na ambao ni msukumo wa chini ni kulazimika kufanya.

Hapa mtu unafanya kitu kwa sababu unaona unalazimika kufanya, kwamba huna namna nyingine bali kufanya. Msukumo wako wa kufanya unatokana na wengine kukulazimisha kufanya. Huu ni msukumo wa chini na ambao hauna kabisa uwajibikaji. Kwani matokeo yoyote ambayo mtu atayapata, ataona siyo yeye anahusika bali wale wanaomlazimisha kufanya. Hapa mtu anakuwa hafanyi kwa ajili yake, hivyo hata juhudi anazoweka, zinakuwa hazitoki ndani yao kweli.

Mbili na ambao ni msukumo wa kati ni kuchagua kufanya.

Hapa mtu unafanya kitu kwa sababu umechagua kufanya, kwamba katika machaguo yaliyopo, hilo ndiyo umechagua kufanya. Hapa kunakuwa na kiasi fulani cha uwajibikaji, lakini bado mtu anakuwa hana msukumo mkubwa sana wa kufanya. Wakati mwingine mtu akipata matokeo fulani, anafikiria kama angechagua tofauti basi mambo yangekuwa tofauti.

Tatu na ambao ni msukumo wa juu ni kutaka kufanya.

Hapa mtu unafanya kitu kwa sababu wewe mwenyewe umetaka kufanya kitu hicho, kwa ridhaa yako mwenyewe, umetaka kufanya. Hapa unakuwa na uwajibikaji wa juu sana kwa sababu hufanyi kwa ajili ya mtu mwingine yeyote na wala huna machaguo mengine. Matokeo yoyote unayoyapata unayapokea kwa sababu unajua ni wewe ndiye umetaka.

Kwa kujifanyia tathmini ya haraka, unajiona ukiwa kwenye ngazi ipi kati ya hizo tatu? Anza na kazi au biashara unayofanya, nini kinakusukuma kufanya?

Je unalazimika kufanya kwa sababu ndiyo inakuwezesha kuendesha maisha?

Je umechagua kufanya kwa sababu ndiyo umeona itakufaa zaidi kwa unachotaka?

Au umetaka kufanya kwa sababu ndiyo kitu unachoweza kutumia kuwa na mchango mkubwa kwa wengine?

Kuwa mkweli kwako na ujipime kiwango chako cha uwajibikaji, ili uweze kuachilia breki zinazokuzuia kufanikiwa.

Baada ya kupata majibu yako hapo, ingia kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ujifunze kwa kina jinsi ya kuwajibika ili uweze kuachilia breki zote ambazo zinakuzuia usifanye makubwa. Sikiliza kipindi hapo chini na ukachukue hatua ili kufanya makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.