3339; Yanayoonekana na yasiyoonekana.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Jiwe la barafu linalokuwa ndani ya maji, huwa linaonekana ni dogo kwa nje.
Lakini kwa ndani jiwe hilo huwa linakuwa ni kubwa zaidi ya linavyoonekana kwa nje.

Kadhalika, mafanikio ya aina yoyote ile huwa yanaonekana ni rahisi kwa nje, hasa pale mtu anapokuwa anayaangalia baada ya kuwa yameshatokea.
Lakini kwa ndani mafanikio ya aina yoyote ile huwa ni magumu na yenye kila aina ya changamoto.

Watu wengi huwa wanafanya maamuzi makubwa ya maisha yao kwa kuangalia yale yanayoonekana kwa nje. Na mara zote maamuzi hayo huwa yanaishia kutokuwa sahihi, kwa sababu kunakuwa na mengi ya ndani ambayo hayakuonekana wala kuzingatiwa.

Kila kitu ni rahisi kwa kinavyoonekana kwa nje.
Ni kwa ndani ndiyo huwa kuna ugumu mkubwa, lakini unaowezekana.
Kinachowakwamisha wengi kupata kile wanachotaka siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu ya matarajio yasiyo sahihi.
Pale mtu anapoingia kwenye kitu akiwa na matarajio ni rahisi, anashtushwa sana pale anapokutana na ugumu.
Ni mshtuko huo ndiyo unaowafanya wengi kukata tamaa na kuacha.

Wewe kuwa tofauti, usifanye maamuzi yoyote kwa yale yanayoonekana pekee. Badala yake jiulize ni yapi yasiyoonekana lakini yana madhara kwenye hicho kitu unachotaka.
Hata kama hutaweza kuona dhahiri, bado unaweza kujiandaa kwa kutegemea kwamba mambo ya ndani kuwa tofauti na yale ya nje.
Tofauti kati ya matarajio na uhalisia ina nguvu ya kuamua kama mtu ataendelea au ataacha.
Pale uhalisia unavyokuwa tofauti sana na matarajio, ndivyo hali ya kukata tamaa inavyokuwa kubwa.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunajua wazi kabisa kile tunachoona kwa nje ni tofauti kabisa na kilicho ndani.
Tunaingia kwenye jambo lolote lile tukiwa na maandalizi ya kukabiliana na zaidi ya yale tuliyotegemea.
Hilo linatuwezesha kudumu kwenye kitu kwa muda mrefu zaidi na hivyo kuzalisha matokeo makubwa zaidi.
Hatukati tamaa pale tunapokutana na uhalisia ambao ni tofauti na matarajio tuliyokuwa nayo.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA hatudharau wala kuchukulia poa chochote kikubwa ambacho mtu amefanya.
Tunajua kuna gharama za ziada ambazo mtu anakuwa ameingia kwenye kukamilisha mambo hayo.
Hilo linatuandaa na sisi kwenda kulipa gharama za ziada ili kupata chochote tunachokuwa tunakitaka.

Kinachotupa matumaini ni kwamba kama wengine wameweza, basi inawezekana na sisi tutaweza pia.
Na hata kama hakuna wengine walioweza, sisi tutakuwa wa kwanza kuweza ili kufungua milango ya uwezekano kwa wengine.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe