Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye utajiri na uhuru wa kifedha, kuna vitu vya msingi sana ambavyo watu wengi wamekuwa hawavielewi na hivyo vinaishia kuwatesa sana. Moja ya vitu hivyo ni tofauti ya UTAJIRI na UKWASI na kiwango sahihi cha kuwa nacho kati ya vitu hivyo viwili.
Kutokujua tofauti ya utajiri na ukwasi imepelekea kuwepo na watu ambao wana mali nyingi, ambazo kwa thamani yake ni utajiri mkubwa, lakini bado wanakuwa wanapitia manyanyaso sana kifedha. Yaani licha ya mtu kuwa na mali zenye thamani kubwa, bado anakuwa hana uhuru wa kifedha.

Mfano ambao upo kwa wengi ni huu, unakuta mtu ana ardhi na nyumba ambazo thamani yake ni kubwa, mfano milioni zaidi ya 100. Lakini mtu huyo huyo akipata shida inayomtaka awe na milioni kumi ya kuitatua, anashindwa kuipata fedha hiyo kwa haraka.
Licha ya mtu huyo kuwa na mali zenye thamani kubwa, fedha anakuwa hana na hilo ndilo linalonyima uhuru na kumweka kwenye manyanyaso. Kwani katika hali hiyo ya uhitaji atajikuta akiingia kwenye mikopo ambayo inamgharimu au kulazimika kuuza mali zake kwa bei ambayo hata ni ya chini.
Wajibu niliojipa ni kuhakikisha kila mtu anayekutana na kazi zangu anajua kwa uhakika tofauti ya UTAJIRI na UKWASI na kuwa na wastani sahihi kwenye maeneo hayo mawili ili aweze kujenga utajiri unaompa uhuru kamili. Rafiki, wewe ni mmoja wa hao ninaowalenga, hivyo karibu ujifunze kwa kina na uchukue hatua ili kunufaika.
Utajiri.
Utajiri wa mtu unapimwa kwa thamani ya vitu vyote anavyomiliki na kutoa madeni anayodaiwa. Hapo unachukua vitu vyote alivyonavyo na kuvithaminisha kwa bei ya soko kwa wakati husika kisha kutoa madeni yote anayodaiwa. Kwa mfano kama mtu ana nyumba yenye thamani ya milioni 120, ana fedha benki milioni 3, fedha taslimu milioni 2 na ana hisa za milioni 5. Mtu huyo huyo akawa na deni la benki ambalo ni milioni 30. Thamani yake ya utajiri ni Milioni 100 (120M + 3M + 2M + 5M – 30M = 100M).
Ukwasi.
Ukwasi ni kile kiasi cha fedha ambacho mtu anaweza kukipata kwa haraka. Hizi ni fedha ambazo zipo taslimu, benki na uwekezaji kwenye masoko ya mitaji kama hisa, vipande na hatifungani. Unapokuwa na mahitaji ya fedha, unaweza kuzipata kwa haraka, huo ndiyo ukwasi.
Tukiendelea na mfano tuliouanza hapo juu, mtu huyo ana ukwasi wa Milioni 10 (3M + 2M + 5M = 10M). Ina maana mtu huyo, licha ya thamani ya utajiri wake kuwa milioni 100, akiwa na uhitaji wa haraka wa fedha anaweza kupata milioni 10 tu. Kiasi cha zaidi ya hapo atakipata kwa kutumia fedha za wengine au kulazimika kuuza nyumba ambayo ndiyo ina thamani kubwa kwenye huo utajiri wake.
Hiyo ndiyo picha halisi iliyo kwa watu wengi, wanakuwa na mali zenye thamani kubwa, lakini wanalia ukata wa fedha. Wanakuwa hawana uwezo wa kupata kiasi cha kutosha cha fedha kwa haraka. Watu hawa huwa na maisha magumu licha ya kuwa wanamiliki utajiri mkubwa.
Njia pekee ya kuondokana na hayo manyanyaso ya kifedha wakati una mali nyingi ni kuwa na wastani sahihi wa utajiri na ukwasi. Na wastani ninaofundisha mimi ni nusu kwa nusu, yaani asilimia 50. Hiyo ina maana kwamba nusu ya utajiri ambao mtu unakuwa nao iwe kwenye ukwasi, yaani ambao unaweza kupata fedha kwa haraka.
Kupata wastani wa ukwasi kwa utajiri, unachukua ukwasi ulionao na kugawanya kwa thamani ya utajiri kisha unazidisha mara 100. Tukiendelea na mfano tulioanza nao, wastani wa ukwasi na utajiri kwa mtu huyo ni 10% (10/100 x 100%). Mtu aliye kwenye hali hii anapaswa kukazana kufanya uwekezaji kwenye maeneo ambayo yana ukwasi mkubwa ili kukuza kiwango chake cha ukwasi.
Hatua ya kuchukua.
Kokotoa wastani wako wa ukwasi kwa utajiri kwa kujumlisha thamani ya vitu unavyomiliki na kutoa madeni. Kisha gawanya jumla ya thamani ya kwasi wako kwa jumla ya utajiri wako na kuzidisha kwa 100. Baada ya kupata jibu lako pima uko mbali kiasi gani na lengo ambalo ni 50%. Weka mpango wa jinsi unavyokwenda kufikia lengo hilo na fanyia kazi mpango huo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina zaidi dhana hizi muhimu mbili unazopaswa kuzijua na kuzifanyia kazi. Karibu usikilize kipindi kujifunza.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.