Rafiki yangu mpendwa,

Ukifungulia redio nyingi, kuna vitu viwili utakavyokutana navyo. Kitu cha kwanza ni wingi wa vipindi vya michezo, sehemu kubwa ya vipindi vya siku kwenye redio vimekuwa ni vya uchambuzi wa michezo.

Kitu cha pili ni utitiri wa michezo inayoitwa ya kubahatisha, ambayo kiuhalisia ni kamari, ila tu imepewa jina la kupunguza makali yake. Kuna vituo vya redio ambavyo vina hizo kamari kwenye kila saa ya kipindi kwa siku nzima.

Kamari hizo zimekuwa zinapigiwa debe sana na wasikilizaji kuonyeshwa jinsi ambavyo ni rahisi kwao kushinda. Wale walioshinda wanatoa shuhuda zao kwa jinsi walivyocheza mara nyingi mpaka kushinda.

Rafiki, hayo mambo mawili ni ya kushangaza sana, iweje watu wapende sana vipindi vya michezo? Kwa nini watu wacheze sana kamari licha ya kwamba nafasi ya kupata fedha wanazotegemea ni ndogo?

Majibu ya maswali hayo ndiyo ambayo ukiweza kuyatumia vizuri, utaweza kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Ukweli ni kwamba, watu wanapenda ushindi. Hiyo ndiyo asili ya binadamu, kupenda na kufurahia ushindi. Lakini kwa bahati mbaya sana, wengi hawana ushindi wanaoupata kwenye maisha yao. Yaani wengi hawana makubwa wanayopambana nayo kwenye maisha yao na kuwapa ushindi ambao wanaweza kuufurahia.

Sasa kwa kuwa wengi wanapenda ushindi, lakini hawawezi kuupata kwenye maisha yao, basi wanachagua kujihusisha na vitu vingine vyenye ushindi. Hapo ndipo ushabiki wa michezo unapopata nguvu. Kwani mtu akiwa shabiki wa timu fulani na ikapata ushindi, anahesabu ushindi wa timu ile kama ushindi wake binafsi. Utazisikia hata kauli za mashabiki hao, leo tumeshinda, wakati shabiki huyo hakuwa anacheza uwanjani.

Lakini pia watu huwa wanapenda matumaini ya ushindi, hata kama wataukosa ushindi wenyewe. Ile hali ya kuwa na matumaini kwamba wanaweza kupata ushindi, huwa inakuwa na msukumo mkubwa kwao. Hapo ndipo watu wanaponasa kwenye michezo ya kubahatisha na kamari. Inajulikana kabisa kwamba kwenye michezo ya kubahatisha na kamari, ni wachache sana watakaoshinda, wengi wanashindwa na huo ni uhakika. Sasa kwa nini watu bado wanacheza michezo hiyo? Jibu ni yale matumaini kwamba wanaweza kushinda. Kwa kuwa haijulikani nani anashinda na kila mchezaji anayo nafasi ya kushinda, basi mtu anacheza akiwa na hayo matumaini. Hata kama atakosa, lakini matumaini aliyokuwa nayo yanamfanya ajisikie vizuri.

Sasa rafiki, swali ni je unatumiaje hali hii ya watu kupenda ushindi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako? Jibu ni kwa kuanzia kwenye mauzo. Kwa chochote unachouza, waonyeshe wateja unaowalenga jinsi ambavyo kinakwenda kuwapa ushindi mkubwa kwenye maisha yao. Wafanye waone jinsi wanakwenda kupata matokeo makubwa na ya haraka bila ya kuweka juhudi kubwa. Hayo yatawashawishi wateja kununua ili wapate ushindi ambao wamekuwa wanautaka sana.

Jinsi ya kutumia mauzo kuwapa watu ushindi na kuweza kuwashawishi kwa wingi nimeijadili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Angalia kipindi hicho, ujifunze na uanze kuwapa watu ushindi ili nao wakupe kile unachotaka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.