3340; Kukaa kwenye ufanyaji.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kanuni yetu kuu tunayoifanyia kazi ni MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO.
Kwa kanuni hii, maarifa pekee hayatoshi, ni lazima yafanyiwe kazi.
Ni hapo kwenye kufanyia kazi ndipo changamoto kubwa na mkwamo unapoanzia kwa wengi.
Kikwazo cha kwanza ni utayari wa kuanza. Kuanza huwa ni kugumu na hivyo watu huwa ni rahisi kuahirisha kuliko kufanya.
Wengi hujiambia bado wanaendelea kujifunza na kujiandaa, lakini ukweli ni wanakwepa tu kuanza.
Hakuna wakati ambao mtu atakuwa amekamilisha maandalizi yote anayotaka kuwa nayo.
Dawa ya kikwazo hiki ni kuanza mara moja, mengine utaendelea kujifunza na kuboresha kadiri unavyokwenda.
Kikwazo cha pili ni utayari wa kuendelea kufanya licha ya magumu ambayo mtu anakutana nayo. Unapanga vizuri nini unafanya na matokeo gani unategemea. Unafanya kweli, lakini matokeo yanayokuja ni tofauti kabisa na matarajio.
Hapo wengi hushindwa kuendelea kufanya, wanakata tamaa na kuacha kabisa.
Kuvuka kikwazo hiki, unapaswa kuendelea kufanya kwa kuboresha zaidi hata pale matokeo yanapokuwa tofauti na matarajio. Kuacha kufanya haitabadili hayo matokeo, bali kuboresha kufanya ndiyo kutaleta matokeo bora.
Kikwazo cha tatu ni usumbufu ambao unaingilia ufanyaji wako. Unapanga vizuri nini unakwenda kufanya lakini baadaye yanajitokeza mambo ambayo yanaonekana ni muhimu au ya haraka zaidi kuliko yale uliyopanga. Kama haupo imara, utakimbizana na hayo mapya yanayojitokeza, ukidhani unafanya mambo ya maana.
Kuvuka kikwazo hiki, weka kipaumbele kikubwa kwenye yale uliyopanga kufanya. Kuwa kabisa na orodha ya yote unayopanga kufanya kwenye siku yako. Pale linapojitokeza jambo lolote unaloshawishika kufanya, usikimbilie kuanza kulifanya, badala yake liongeze kwenye orodha ya yale uliyopanga kufanya na utalifanya pale wakati wake unapofika.
Vitu vingi unavyovipa uharaka na umuhimu havina hadhi hiyo.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kufanya ni sehemu ya lazima kwenye safari ya mafanikio.
Kuanza kufanya na kuwa na mwendelezo wa ufanyaji ndiyo njia ya uhakika ya kupata matokeo makubwa.
Kwa kuwa sehemu ya jamii hii, umechagua kuwa mfanyaji wa uhakika. Ni bora ukosee kwa kufanya kuliko ukosee kwa kutokufanya kabisa.
Hupaswi kufurahia tu kujifunza, unapaswa pia kuyaweka yale uliyojifunza kwenye matendo ndiyo yaweze kuleta matokeo ya tofauti.
Na ufanyaji unapaswa kuwa wa uendelevu na siyo kuanza na kuacha au kuishia njiani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe