
Kwenye maisha kuwa na furaha, kukutana na changamoto ni suala la kawaida. Na hayo ndiyo maisha yenyewe. Siku inaweza kuanza ngumu ikaisha vizuri au kuanza vizuri na kuisha vibaya.
Kwa kuwa kila mtu kuna hali anapitia, suala la kuomba ushauri limekuwa na kawaida. Mtu pekee wa kukimbilia linapokuja suala la kuomba ushauri ni kwa rafiki yake wa karibu. Sio tu rafiki bali msiri wake. Mtu anayeamini hawezi kwenda kusambaza habari zake mahali pengine nje yake.
Maana tupo kwenye dunia ya sayansi na teknolojia. Jambo unalifanya na mtu mmoja lakini ndani ya muda mchache linawafikia wengi.
Siku hizi washauri wa biashara wamekuwa wengi, lakini sio kila mmoja anaweza kukushauri. Kadhalika na wauzaji ni wengi lakini sio kila mmoja unaweza kumshauri lazima kuwepo na bond fulani. Hasa urafiki. Maana watu wengi wanapenda kuomba ushauri kwa marafiki.
Ili ujenge urafiki na mteja unahitaji kuwa mashauri wake. Ushauri unaopaswa kufanyia kazi hapa ni wa kimauzo zaidi. Lakini ikitokea kuna changamoto nyingine ambazo unaweza kumsaidia kupata utatuzi usimuache nazo. Mwelekeze namna nzuri ya kuzitatua.
Sifa za mshauri mzuri;
Moja; Asiwe anajiona
Mbili; Awe mkweli
Ukweli unapanda ngazi lakini uongo unapanda lift. Utamuuma lakini atafurahia baadaye.
Tatu; Ajue kile anachokushauri.
Nne; Taarifa sahihi
Tano; Namna sahihi ya kufikisha ujumbe. Ajue mpokeaji ataupokeaje. Modality iwe nzuri na kuvutiwa.
Katika kumshauri mara zote, epuka kuwa mtu wa kwanza au kuwa na kimbelembele. Yaani unaona mtu anafanya hiki haraka unaanza kusema; oh! unajua hapa ukifanya hivi utafanikiwa. Kumbuka, ni wengi anakutana nao wanamwambia hivyo. Unachotakiwa ni kuangalia namna nzuri kumweleza juu ya kufanya kitu.
Mambo ya kuzingatia wakati wa kumshauri mtu;
Moja; Mazingira.
Siyo kila sehemu unaweza kutoa ushauri angalia mazingira rafiki.
Mbili; Maandalizi
Rejea mitihani kwa wanafunzi, wanapewa muda wa kujiandaa ili kufanya vema mitihani. Ipo hivyo kwenye kumshauri mtu. Mpe nafasi ya kujiandaa vema na wewe kujiandaa kwa ajili ya uwasilishaji.
Tatu; Mada.
Lazima iendane na huduma yako. Wakati wa uwasilishaji epuka kuzunguka. Nenda kwenye point, maneno yasiwe mengi.
Nne; Mhusika.
Sio kila mtu unaweza kumshauri. Lazima uangalie mtu mzuri kumshauri ili afanyie kazi unachomshauri.
Pale unapotaka kumshauri mtu neno zuri la kutumia ni mapendekezo. Mfano, “sina uhakika kama itakufaa, lakini kuna bidhaa zingine ukiwa nazo zitakusaidia kuongeza mauzo”. Neno lakini linamfanya afikirie zaidi sentensi ya mwisho ya kuongeza mauzo. Na kusahau maneno yaliyosemwa mwanzoni.
Chukulia upo kazini, bosi wako akakuita na kuanza kukwambia; hivi unajua bwana Lazaro umekuwa unafanya vema katika kampuni yetu. Sifa zako na utendaji wako hakuna mtu anapinga, kwa namna unavyopambana. Lakini, kitu fulani kinapaswa kubadilika.
Anapomaliza kuongea hivyo, simu inaita anaipokea na kuondoka. Huku akisema, mtaonana siku inayofuata au baada ya masaa kadhaa. Nini kinabaki kinakuwazisha? Jibu ni neno lakini. Kwa hiyo ipo hivyo kwa mteja wako.
Hili ni neno la ushawishi kwa mteja huyo linahusika na kutoa mapendekezo. Unaweza kuona katika neno hilo hakuna mahali tumezungumza ni lazima ufanye kitu hiki au uongeze bidhaa hii. Bali nimesema sina uhakika.
Hii ina maana hujatoa ushauri wa mwisho, wewe mwenyewe unaonekana kama huna uhakika hali inayomfanya mtu afanyie kazi ushauri wako ka kina. Anapopata matokeo makubwa ni rahisi kukufikiria wewe na kuomba uendelee kumshauri zaidi.
Ni watu wangapi wanakuomba ushauri? Fanyia kazi yote uliyojifunza katika somo hili.
Imeandaliwa la Lackius Robert, Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.