3341; Ziada na pungufu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mara zote kwenye maisha yetu, huwa hatupo kwenye hali ya kutosha.
Badala yake tunakuwa kwenye hali ya ziada au pungufu.
Ziada ni pale inapokuwa zaidi ya ulivyopanga na pungufu ni inapokuwa chini ya ulivyopanga.
Wajibu wako mkubwa, kwenye kila eneo la maisha yako ni kuwa na ziada.
Kwenye kipato, kuwa na ziada kuliko kuwa na pungufu. Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kujenga utajiri na uhuru wa kifedha.
Kwenye kazi, nenda hatua ya ziada kwa kila unachofanya kuliko kufanya kwa upungufu.
Ni kwa kwenda hatua ya ziada ndiyo unaweza kutoa thamani kubwa kuliko wengine na kuweza kupata matokeo bora.
Kwenye rasilimali zote unazotumia kwenye kila eneo la maisha yako, unapaswa kuwa na ziada na siyo pungufu. Hiyo ni kuanzia kwa watu unaowaajiri, ni bora kuwa na zaidi ya unavyohitaji kwa sababu itatokea baadhi kushindwa kuendelea kuwepo na hapo wa ziada wanafanya pengo lisionekane.
Ukiwa na idadi unayoona inatosheleza, ni sawa tu na una pungufu. Kwani yeyote anaposhindwa na kutokuwepo, anaacha pengo ambalo ni upungufu.
Muda unaoweka kwenye yale muhimu unapaswa kuwa zaidi kuliko pungufu.
Wengi huwa wanagawa muda wao kwenye vitu vingi na kidogo unaobaki ndiyo wanapeleka kwenye yale muhimu. Wewe unapaswa kupeleka muda mwingi kwenye yale muhimu kwanza na kidogo unaobaki ndiyo unaupeleka kwenye mengine yasiyokuwa muhimu sana.
Hata wateja unaowahudumia, mara zote kuwa na ziada kuliko pungufu. Ni hiyo ziada ndiyo itakusukuma ufanye kwa ubora zaidi. Lakini pia kukufanya uongeze mchujo wa aina ya wateja unaotaka kuwa nao.
Unapokuwa na pungufu ya wateja, unakuwa na tamaa ya kumkubali mteja yeyote hata kama hana zile sifa unazotaka wateja wako wawe nazo.
Japokuwa ziada inaweza kuonekana ni kazi zaidi kuliko pungufu, ndiyo yenye nguvu ya kukupa uhuru kwenye kila eneo la maisha yako.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mara zote tunapambana kupata ziada badala ya kuwa na pungufu. Kwa kila tunachofanya, tunakwenda hatua ya ziada.
Kwa kila lengo tunaloweka, ni kubwa kuliko mazoea na kila tunapolifikia lengo, tunalikuza zaidi.
Ndani ya jamii hii tunafanyia kazi kuwa na ziada kwenye kila eneo la kimafanikio.
Kuwa ndani ya jamii hii inatuonyesha jinsi ambavyo makubwa zaidi tunayotaka yanawezekana, kwa sababu tumezungukwa na watu wanaoyafanya hayo makubwa.
Usijiambie upo kwenye hali ya kutosha. Kama haupo kwenye hali ya ziada, basi jua moja kwa moja upo kwenye pungufu.
Wajibu wako mkuu ni kuwa kwenye hali ya ziada mara zote.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe