Kila kitu kwenye maisha kina miongozo na miiko yake. Malengo makubwa ni kuhakikisha kunakuwa na standard moja ya utendaji. Pamoja na kutojipa sababu ya kutofanya kitu.

Ni kupitia uwepo wa miongozo watu wanafanikiwa kupata baadhi ya mahitaji yao. Kwa sababu wanachukua wajibu wa kufanya yaliyo muhimu.

Kwenye mauzo pia, ili ufanikiwe kuuza zaidi lazima kuwepo na falsafa ambazo ndiyo mwongozo wako mkuu. Kila unayefanya naye kazi hakikisha anaelewa vema falsafa yenu ili mfanikiwe wote.

Mfano, KISIMA CHA MAARIFA chini ya Kocha Dkt. Makirita Amani falsafa yao inasema, Maarifa +Vitendo= Mafanikio. Ni mengi tumekuwa tunaona na kujifunza kwake, hasa msimamo katika kazi zake.

Elon Musk ambaye ni tajiri duniani moja ya falsafa yake ni “kuamini katika ndoto yako na kufurahia unachofanya”. Ndio ufunguo wa wa mafanikio. Anasema, watu wengi wanasema nina bahati ndiyo ninatajirika. Lakini sio kweli, kuna juhudi kubwa ninaweka katika kazi. Nafanya masaa 120 kwa wiki huku wengi wakiwa wanafanya saa 40 wiki. Hapo utasema nina bahati? Ukifuata mwongozo huu na bahati kidogo lazima ufanikiwe.

Anaongeza kuwa, kuwa na malengo madogo ni changamoto kwa kampuni nyingi hali inayozirudisha nyuma. Wengi wakifia malengo motisha inapungua.

Falsafa inatusaidia kuishi sasa, kutumia vizuri wakati ambao tunao.  Ukiwa na falsafa utapiga hatua kubwa. Utajichunguza na kujiangalia kama kuna hatua gani umepiga na kutojipa sababu ya kuacha kitu.

Kwahiyo mambo ya kujifunza ukiwa na falsafa ni;

Moja; Ung’ang’anizi.
Magumu katika maisha ni suala la kawaida na pengine ndiyo maisha yenyewe. Je, unapokutana na magumu unakata tamaa?

Mafanikio makubwa yapo kwenye  kung’ang’ana bila ya kukata tamaa. Pale unapokutana na magumu unarudi kwenye falsafa. Je, nina maarifa ya kutosha katika hili, nimetumia jitihada zangu zote? Kisha unarudi kwenye utendaji.

Mbili; Kutumia uwezo wako.
Nguvu ya binadamu ipo kwenye akili yake. Je, unaitumia akili yako inavyotakiwa, hasa kufikiria mambo ya msingi na muhimu?

Elon Mask tuliyemuona hapo juu kufikiria ndiyo kanuni yake ya kwanza.  Kila kitu anakifikiria kama hakijawahi kufanyika.

Yaani badala ya kuangalia kitu jinsi kinavyofanyika sasa na kuanza kukifikiria hivyo, unapaswa kufikiria kitu kama vile hakijawahi kufanyika.

Kwa njia hiyo hutazuiwa na fikra au ukomo uliopo, bali utakuwa huru kufikiri na kuja na ubunifu mpya. Je, unafikiria kile kilichozoeleka au kufikiria vitu kwa upya?

Tatu; Matamanio makubwa.
Ukiwa na malengo mengi makubwa, yatakusuma kufanya yale ya muhimu. Ukikwama sehemu unarudi kwenye falsafa yako, je ni kweli kitu fulani nimekifanya vema? Ukiona bado, boresha zaidi ili upate kitu sahihi unachotaka.

Hitimisho; Falsafa inatujenga kiroho na kuyapangilia maisha yetu, kuongoza matendo yetu na kutuonesha nini tunapaswa kufanya na nini hatupaswi kufanya. Bila ya falsafa, hakuna mtu anayeweza kuishi kwa ujasiri au utulivu wa akili.

Unakutana na mambo mengi kwenye maisha yako ya kila siku, ambayo yanakutaka kufanya maamuzi na wakati mwingine maamuzi hayo siyo rahisi. Katika nyakati kama hizi, falsafa inakuwa msaada kwako kufanya maamuzi sahihi, kwa sababu unaijua misingi unayosimamia.

Je, ni falsafa ipi inayokuongoza katika utendaji wako?

Ukiweza kufanyia kazi yote uliyojifunza katika somo hili kuna kitu unaenda kupata katika maisha yako.

Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi.
Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.