Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara kwa malengo na mipango isiyo sahihi na hilo limekuwa linachangia wao kutokufanikiwa kwenye biashara hizo.

Kwa mfano kitu kinachowasukuma wengi kuingia kwenye biashara huwa ni kuingiza kipato cha kuendesha maisha yao. Tena huwa wanasema kabisa kwamba wapate hela ya kula. Sasa unadhani wakishapata hiyo hela ya kula nini kinachofuata? Wanaridhika na kuacha kuweka juhudi kubwa.

Ili mtu aweze kufanikiwa kwenye biashara, lazima awe na malengo na mipango sahihi. Na hili halihitaji mtu awe na utaalamu mkubwa sana ndiyo aweze kulifanya. Kinachohitajika ni mtu kujua nini anachotaka na gharama gani anapaswa kulipa ili kukipata.

Pamoja na yote ambayo biashara inafanya, kitu cha kwanza ambacho huwa kinaangaliwa ni mauzo. Hiyo ndiyo namba ya kwanza kupimwa kwenye biashara na ndiyo moyo na uhai wa biashara.

Ili biashara iweze kufanya mauzo, lazima ifanyie kazi lengo lake kuu ambalo ni kutengeneza wateja ambao ni waaminifu kwenye biashara hiyo. Wateja ndiyo lengo kubwa la kufanyia kazi kwenye biashara kwa sababu bila hao hakuna mauzo. Na pia, kikwazo cha kwanza kwa kila biashara ni kutokujulikana. Mara nyingi sana biashara inakuwa na bidhaa au huduma ambazo watu wanazihitaji, lakini watu hao hawajui kama biashara hiyo ipo.

Hivyo biashara ina kazi kubwa ya kuhakikisha wateja wote wanaoweza kunufaika nayo wanajua juu ya uwepo wa biashara hiyo. Na hapo ndipo penye kazi kubwa, kwa sababu wengi huwa hawana mkakati sahihi wa kufanya biashara zao kujulikana.

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kupiga kelele kubwa ili kila anayeweza kunufaika na biashara aweze kujua uwepo wake. Tunasema kupiga kelele kwa sababu kwa sasa tupo kwenye zama za usumbufu, zama ambazo wateja wamevurugwa na mambo mengi yanayoendelea. Katika hizo kelele, ni rahisi sana kupotezewa kama husikiki kwa ukubwa wa kutosha.

Hivyo tunaposema kupiga kelele, tunamaanisha hasa, kwa sababu bila ya kusikika kwa wingi na mara kwa mara, unasahaulika haraka sana na wateja unaowalenga.

Changamoto ya zama hizi siyo tu kujulikana, bali pia kusahaulika. Wateja wanaweza kukujua kwa kukusikia, lakini kama hawataendelea kukusikia, wanakusahau. Kadiri inavyowachukua wateja muda mrefu bila kukusikia, ndivyo wanavyokusahau.

Kelele hazikwepeki kama unataka kufikia wateja wengi, kukumbukwa, kuzoeleka, kuaminika na kisha wateja kununua.

Kuaminika ni kikwazo kingine ambacho kila biashara inapaswa kukivuka ndiyo iweze kufanya mauzo makubwa. Wateja wanaweza kuijua biashara, wakawa na uhitaji na kuweza kumudu, lakini bado wasinunue kwa sababu wanakosa imani. Wateja wa aina hiyo wanachohitaji ni kuendelea kusikia mara kwa mara kutoka kwenye biashara hiyo. Kadiri wanavyosikia ndivyo wanavyozoea na mazoea yanajenga imani.

Kupiga kelele kwenye biashara ni kitu ambacho hakikwepeki, lakini pia siyo tu kuleta usumbufu kwa wateja unaowalenga, maana hilo halitakusaidia. Badala yake ni kuwa na mkakati mzuri wa kuwafikia wateja wengi na kuendelea kuwafuatilia kwa karibu mara kwa mara.

Kuwafikia wateja wapya kwa mara ya kwanza inafanyika kwa njia mbalimbali za usakaji na matangazo kwenye biashara. Njia hizo zinaifikisha biashara kwa wale ambao hawaijui. Ili ziwe na ufanisi, zinapaswa kufanyiwa kazi mara zote na siyo kwa vipindi fulani tu. Yaani zoezi la kuwafikia wateja wapya linapaswa kuwa la wakati wote.

Kuwafuatilia wateja kwa karibu na mara kwa mara ni kuhakikisha wateja waliofikiwa wanaendelea kusikia kutoka kwenye biashara ili wasisahau. Ili ufuatiliaji uwe na ushawishi, haupaswi kuwa wa kuwachosha wateja. Badala yake kila wakati unapaswa kubadilika ili kutoa thamani kubwa kwa wateja.

Kwa ufuatiliaji endelevu unaoufanya kwa wateja wako, wanapaswa kuwa wanasubiria kwa shauku kusikia kutoka kwako kwa sababu wanategemea kupata thamani kwenye kila ufuatiliaji unaofanya kwao. Kwa kufanya hivyo utapata mapokezi mazuri kwenye ufuatiliaji.

Lakini kama utafanya ufuatiliaji unaochosha, wa kupeleka matangazo tu muda wote, utawafanya wateja unaowafuatilia wakukimbie. Wataacha kupokea mawasiliano unayofanya nao na hata kukuzuia usiweze kuwafikia.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina dhana hii ya kupiga kelele kwa ukubwa na uendelevu ili uweze kufanya mauzo makubwa kwenye biashara yako. Karibu ujifunze kutoka kwenye kipindi hiki na ukachukue hatua kunufaika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.