Rafiki yangu mpendwa,

Ukiwauliza wauzaji wengi kwa nini hawafanyi mauzo makubwa, kitu cha kwanza ambacho wengi watakuambia ni ushindani ni mkali. Wengi wanaona wateja wanaowalenga, wanalengwa na washindani wao pia. Na pale washindani wanapokuwa na kitu cha ziada ambacho wao hawana, wanawapoteza wateja hao kwa washindani wao.

Hiyo ni sababu ambayo nimekuwa naikataa mara zote, kwa sababu siyo ukweli. Sababu ya ushindani wa kibiashara kuwa ndiyo inakwamisha mauzo siyo kweli. Au kama ni kweli, basi ni kwa wavivu ambao hawapo tayari kuweka kazi ili kufanya mauzo makubwa.

Nitaanza kukushawishi kuhusu hilo kwa kuanza na KANUNI YA SOKO KUBWA.

Kanuni ya soko kubwa inawagawa wateja wote kwenye soko kwenye ngazi mbalimbali.

Juu kabisa kuna asilimia 3 ya wateja, ambao wapo kwenye hali ya kununua kwenye wakati husika. Hawa ni ambao wana uhitaji na wanataka kununua. Hawa ndiyo wateja wanaolengwa na kila muuzaji. Asilimia TATU TU! Hebu ona hapo rafiki, kelele zote za ushindani, ni kwenye asilimia 3 ya wateja.

Chini ya hapo kuna asilimia 17 ya wateja ambao wanakusanya taarifa kuhusu kile wanachotaka. Hawa wanakuwa na uhitaji, ila bado hawajafanya maamuzi ya kununua. Wanachofanya ni kukusanya taarifa za wapi wanaweza kupata kile wanachotaka na namna bora ya kunufaika. Hawa watakuja kununua siku za karibuni, ila siyo sasa.

Chini ya hapo kuna asilimia 20 ya wateja ambao wana uhitaji, ila hawana mpango wowote wa kuchukua hatua ili kupata kile wanachohitaji. Hawa ni wateja ambao wangeweza kunufaika na biashara yako, lakini hawana mpango wowote wa kununua sasa au siku za karibuni. Hawa hawana chochote kinachowasukuma kuchukua hatua za tofauti, kwa sababu maisha yao yanaenda, hata kama siyo kwa ubora waliotaka.

Mwisho kabisa kuna asilimia 60 ya wateja ambao hawajui hata kama wana uhitaji. Hawa wanaona maisha yao yapo sawa tu na wala hawajawahi kufikiria wanahitaji kile unachouza, japo kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwao.

Sasa ni rudi tena kwako rafiki, je bado unaamini kwamba ushindani ndiyo unakuzuia kufanya mauzo makubwa? Jibu litakuwa ndiyo kama na wewe unaangalia asilimia 3 ya wanaonunua sasa.

Lakini ukiangalia asilimia 17 na 20, utaona wazi kabisa jinsi ambavyo kuna fursa kubwa ya wewe kufanya mauzo makubwa bila ya kusumbuliwa na ushindani.

Kitu pekee unachohitaji kufanya ili kuuza kwa ukubwa bila ya kusumbuliwa na ushindani ni kulenga asilimia 17 na 20 ambayo haipo kwenye kununua sasa. Unachopaswa kufanya ni kujenga mahusiano mazuri na makundi hayo mawili, kiasi cha wao kukuamini kwa manufaa wanayoyapata kwako. Na pale wanapokuwa tayari kununua, wanakufikiria wewe tu na siyo washindani wengine.

Hili linahitaji wewe ufanye kazi kubwa ya kuwapa wateja thamani kabla hata hawajanunua. Na njia bora ya kufanya hivyo ni kuwapa elimu, maarifa na ushauri ambao unakuwa na manufaa kwao. Kadiri wanavyojifunza kupitia wewe na kunufaika, ndivyo wanavyokuamini. Inapofika wakati wa kununua, wanakuwa tayari kununua kwako kuliko kwa wengine.

Ukaribu unaokuwa nao na wateja hao ambao hawapo kwenye uhitaji wa kununua sasa pia unawafanya wapate msukumo wa kununua. Kwa mfano pale unapowaelimisha wateja umuhimu wa kuchukua hatua, inawafanya waone hawana sababu ya kuendelea kusubiri bali kuchukua hatua. Hapo unakuwa umewawahisha kufanya maamuzi ya kununua na kununua kwako tu.

Mauzo yanakuwa magumu pale wauzaji wanapotaka kuvuna kile ambacho hawajapanda, hili linawapeleka kwenye ushindani mkali na unaowaumiza. Kama muuzaji utaamua kupata na kupalilia wateja wako mwenyewe, siku ya mavuno utachekelea wakati wengine wanalia.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza jinsi ya kuwafikia wateja wengi zaidi, hata wale ambao hawana mpango wa kununua sasa ili kujenga nao mahusiano na kuwashawishi kununua. Karibu uangalie kipindi, ujifunze na kuchukua hatua ili kuepuka ushindani kwenye mauzo.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.