Rafiki yangu mpendwa,
Kitu chochote unachotaka kwenye maisha yako, kipo kwa watu wengine. Chukua mfano wa fedha, ndiyo unataka fedha, lakini je unazitoa wapi? Huwezi kutengeneza fedha zako mwenyewe, bali utazipata kutoka kwa watu wengine.
Kuna njia mbili za kupata chochote unachotaka kutoka kwa wengine. Moja ni kuwalazimisha wakupe, hapa unatumia mabavu, hila, wizi na nyingine za aina hiyo. Njia hii inaweza kukupa matokeo, lakini huwa siyo njia ya kudumu na mwisho wake huwa ni mbaya.
Njia ya pili ni kuwafanya watu hao wakupe kile unachotaka kwa ridhaa yao wenyewe. Hapa unawashawishi watu kuwa tayari kukupa kile walichonacho, kwa utashi wao wenyewe, huku wakifurahia kufanya hivyo. Hii ndiyo njia bora ya kupata unachotaka, ambayo ina matokeo ya kudumu.
Ili uweze kuwafanya watu wakupe unachotaka wao wenyewe, lazima uwe na ushawishi mkubwa. Ushawishi ni kitu ambacho tunakihitaji kwenye maisha yetu ya kila siku, lakini tumekuwa hatukipi uzito mkubwa.

Aliyekuwa mwandishi na mkufunzi Dale Carnegie, kwenye kitabu chake kinachoitwa HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE ameshirikisha kanuni za kufanyia kazi ambazo zinakuwezesha kujenga ushawishi mkubwa kwa wengine.
Msingi mkuu wa kitabu ni binadamu ni viumbe wa kihisia, ambapo tunafanya maamuzi yetu kwa hisia kwanza kisha kuyahalalisha kwa mantiki. Huwa tunapenda kujichukulia ni viumbe wa kimantiki, lakini sivyo uhalisia ulivyo.
Hivyo kazi kubwa kwenye ushawishi ni kuweza kwenda vizuri na hisia za watu ili wawe tayari kukupa kile unachotaka. Hilo linahusisha wewe kuwafanya watu wengine wajisikie vizuri pale wanapokuwa na wewe. Pia inahusisha watu kukupenda na kuvutiwa na wewe kwa jinsi unavyojihusisha nao.
Kitabu kimegawanyika kwenye sehemu nne kama ifuatavyo.
Sehemu ya kwanza ni jinsi ya kukabiliana na watu kwa ujumla. Sehemu hii inaeleza misingi ya namna ya kuchangamana na watu kwenye maisha ya kila siku. Kuna vitu ambavyo watu tumezoea kuvifanya na vinatukwamisha sana kwenye ushawishi.
Moja ya misingi muhimu kwenye sehemu ya kwanza ni USIKOSOE, USILAANI WALA USILAUMU. Huu ni msingi wa kwanza na muhimu sana kwenye kujenga mahusiano na ushawishi kwa wengine. Watu huwa hawapendi kukosolewa, hivyo unapochukua hatua ya kufanya hivyo, hata kama ni kwa wema, huwa inapunguza ushawishi. Kitabu kimeeleza njia bora za kuwasaidia watu kubadilika bila ya kuwakosoa.
Sehemu ya pili ya kitabu ni jinsi ya kuwafanya watu wakupende na kukukubali. Sehemu hii inaeleza misingi sita ya kuzingatia ili kupendwa na kukubalika na wengine. Misingi hiyo inahusisha jinsi unavyowachukulia wengine na unavyojiweka wewe mwenyewe.
Moja ya misingi muhimu kwenye sehemu ya pili ni KUTABASAMU. Kutabasamu, kitu ambacho hakina gharama yoyote kufanya kuna nguvu ya kuwavutia watu kwako. Mtu anayetabasamu anakuwa amewakaribisha wengine kwenye moyo wake. Tabasamu linamfanya mtu aonekane ni rafiki na anayejali. Wakati kukosa tabasamu kunafanya mtu aonekane siyo rahisi na hajali. Mara zote kuwa na uso wa tabasamu ni hitaji muhimu kwenye kuwashawishi watu wengine.
Sehemu ya tatu ya kitabu ni jinsi ya kuwafanya wakubaliane na mawazo yako. Sehemu hii inaeleza misingi 12 ya kuwafanya watu wabadili mawazo yao na kukubaliana na wewe. Na hilo halitawezekana kwa kuwalazimisha, bali kwa wao wenyewe kuchagua kufanya hivyo.
Moja ya misingi muhimu kwenye sehemu hii ya tatu ni KUTOKUBISHANA. Mwandishi anaeleza wazi kwamba njia pekee ya kushinda mabishano ni kutokubishana. Anasisitiza ukishaingia tu kwenye mabishano, tayari umepoteza. Kwa sababu hata kama utashinda mabishano hayo, bado utakuwa umempoteza huyo uliyemshinda. Kama unataka watu wakubaliane na wewe, epuka sana mabishano.
Sehemu ya nne ya kitabu ni kuwa na ushawishi kama kiongozi. Sehemu hii ina misingi 9 ya kuzingatia ili uweze kuwa na ushawishi kama kiongozi kwa wale ambao unawaongoza. Kuwa kiongozi kunahitaji sana ushawishi kuliko mabavu. Mabavu yanaweza kuonekana ni rahisi, lakini huwa hayadumu. Ushawishi unahitaji kazi, lakini matokeo yake ni ya muda mrefu.
Moja ya misingi muhimu kwenye sehemu hii ya nne ni KUULIZA MASWALI BADALA YA KUTOA AMRI. Kama kiongozi unaweza kuwa unatoa maelekezo ya nini kifanyike, lakini hilo huwa halipokelewi vizuri, kwa sababu watu huwa hawapendi kupangiwa nini wafanye. Ili kuwa na ushawishi zaidi, waulize watu maswali ambayo majibu yake yanawafanya wawe wamekubali kufanya kitu. Badala ya kuwaambia wafanye moja kwa moja na wakawa wazito, waulize maswali ambayo watayajibu na kupitia majibu yao wanaona wamechagua wao wenyewe kufanya.
Rafiki, kitabu hiki cha HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE ni kitabu ambacho kila mtu anapaswa kukisoma na kukitumia kwenye maisha yake. Kwa sababu kwenye kila kitu unachofanya, unahusiana na watu wengine.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza misingi yote kutoka sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu. Na misingi ya sehemu ya nne nitaielezea kwenye kipindi kingine kinachofuata. Sikiliza kipindi hicho cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ili ujifunze na kuwa na ushawishi mkubwa utakaokuwezesha kupata kila unachotaka.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.