3344; Kama umeridhika.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kitu kinachoshangaza kama watu ambao wanataka kupata matokeo ya tofauti, lakini bado wanaendelea kufanya yale yale ambayo wamekuwa wanayafanya mara zote.
Inajulikana kabisa kwamba, ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile, halafu kutegemea matokeo ya tofauti.
Huwezi kupata matokeo ya tofauti kama wewe mwenyewe haupo tayari kubadilika.
Moja ya vitu vinavyowazuia watu kubadilika ni kukosa uhakika.
Huwa wanaendelea kufanya yale waliyozoea kufanya, kwa sababu tayari wana uhakika wa matokeo yake, hata kama ni madogo.
Kufanya mambo mapya ambayo ni kama majaribio kwao, ni kitu ambacho wengi hawapo tayari nacho.
Ni kweli kwamba kufanya vitu vipya hakuna uhakika wa kupata matokeo uliyozoea kupata.
Ni majaribio ambayo yanaweza kuleta matokeo au yasilete. Yanaweza yakafanya kazi au yasifanye.
Swali ni kwa nini uwe tayari kufanya mambo mapya ambayo huna uhakika nayo na kuacha yale uliyozoea na una uhakika nayo?
Kwa nini uache kufanya kile kinachofanya kazi na ujaribu ambacho hujui kama kitafanya kazi?
Jibu ni moja tu, kama huridhishwi na matokeo unayopata sasa, basi huna budi bali kujaribu vitu vya tofauti.
Hata kama huna uhakika na vitu hivyo vipya, bado inabidi uvifanye kwa sababu pale unapokuwa sipo unapokuwa unataka kuwa.
Lakini kama umeridhika na pale ulipo sasa, kama huna msukumo wa kwenda zaidi ya hapo, haina haja ya kuhangaika na usiyokuwa na uhakika nayo wakati yenye uhakika yapo.
Kama pale ulipo sasa ndiyo unapotaka kuwa, ya nini uhangaike na majaribio ambayo yanaweza kupavuruga hapo ulipo?
Japo pia unahitaji tahadhari, kwa sababu mambo huwa yanabadilika. Kinachofanya kazi kwako kwa sasa, baadaye kinaweza kisifanye tena kazi.
Hivyo hata kama umeridhika na pale ulipo, usijisahau sana ukaja kujikuta umeachwa nyuma na mabadiliko yanayokuwa yanaendelea.
Hiyo ina maana hata kama umeridhika, usijisahau na kujiachia sana. Endelea kukagua namna gani unaendelea kuwa mbele zaidi ya pale ulipo sasa ili mabadiliko yoyote yanayokuja yasikurudishe nyuma.
Hata kama umeridhika sasa, unajihakikishiaje kuendelea kuridhika na siku zijazo?
Jibu kitarudi kwenye kuwa mbele ya mabadiliko.
Na hapo utakuja kukuta kwamba njia nzuri ya kuyawahi mabadiliko ni kuendelea kujaribu vitu vipya hata pale unapokuwa unapata matokeo mazuri.
Kwa sababu wakati mzuri wa kufanyia kazi mabadiliko ni pale unapokuwa huyahitaji sana.
Ukishakuwa na uhitaji mkubwa, utaanza kulazimisha majaribio unayofanya yakupe matokeo fulani unayoyataka na hapo utaongeza nafasi ya kushindwa.
Kama hujaridhika na pale ulipo sasa, chukua hatua za tofauti hata kama huna uhakika na matokeo unayokwenda kupata. Utaboresha kila aina ya matokeo yanayokuja mpaka upate kile unachotaka.
Kama umeridhika na pale ulipo sasa, chukua hatua za tofauti ambazo zitakuandaa na mabadiliko yatakayokuja. Huo unakuwa muda mzuri kwako kujaribu vitu tofauti bila ya kulazimisha matokeo na hivyo kujiweka kwenye nafasi ya kupiga hatua kubwa.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, mara zote tunakuwa kwenye hali ya kujaribu vitu vipya.
Kwa popote ambapo tumefika, hatujaridhika nako, kwa sababu tunajua tunaweza kufanya na kwenda zaidi ya hapo.
Tunajua bado tuna uwezo mkubwa zaidi ya ule ambao tumeshautumia, hivyo mara zote tunajisukuma zaidi ya pale tulipo sasa.
Ndani ya jamii hii kila mtu ana malengo makubwa ambayo anayapambania, yanayomsukuma kutoka nje ya mazoea aliyonayo.
Na pale mtu anapofikia malengo hayo siyo ndiyo unakuwa mwisho, bali anayakuza zaidi hayo malengo na kuendelea kuhitajika kufanya kwa utofauti na ukubwa zaidi.
Hata kama hatuna uhakika wa kitu kufanya kazi, hatuachi kufanya majaribio.
Kwa matokeo yoyote tunayoyapata hatuachi kuyaboresha zaidi mpaka kupata kile tunachotaka.
Haturidhiki na kujisahau, tunaendelea na mapambano mara zote.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe