3345; Siyo wewe, bali wao.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwa asili, sisi binadamu huwa ni wabinafsi.
Kwa kitu chochote tunachofanya, huwa tunaanza kujiangalia sisi wenyewe kwanza.
Tunaangalia ni kwa namna gani tunanufaika na kitu kabla ya kujihusisha nacho.
Hata pale tunapowajibu wengine, huwa tunajiangalia sisi wenyewe nini tunafikiria na kutaka.
Hatujihangaishi sana na wengine wanafikiria au kutaka nini.
Hivyo ndivyo tunavyofanya mambo yetu, halafu tunashangaa pale tunaposhindwa kupata matokeo mazuri.
Unapoenda kuvua samaki na kuweka chambo kwenye ndoano, siyo kwa ajili yako, bali ni kwa ajili ya samaki.
Na hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye mahusiano yetu na watu wengine.
Tunapaswa kuwafikiria wao zaidi kuliko sisi wenyewe.
Tunapaswa kujiuliza hao wengine wananufaikaje na siyo sisi tu.
Jua nini ambacho wengine wanafikiria na kutaka kisha utumie hayo kuwashawishi wafanye kile unachotaka wafanye.
Kama kila mtu anajifikiria zaidi yeye mwenyewe, utaweza kuwashawishi wengi zaidi kwa kufikiria kuhusu wao na siyo wewe pekee.
Unapoweka maslahi ya wengine mbele, wanakuwa tayari kushirikiana na wewe.
Na zaidi kwenye kuongea na wengine, haijalishi sana ni nini wewe unafikiria au kutaka, bali wao.
Ongea na watu kuhusu kile wanachofikiria na kuwapa yale wanayotaka na utakuwa na ushawishi mkubwa kwa watu wengine.
Unaweza kuona kama ipo kinyume, kwamba vitu unataka wewe, lakini inabidi uhangaike zaidi na mambo ya wengine.
Hivyo ndivyo mambo ya watu yalivyo.
Siyo sisi tulioamua yawe hivyo, bali ndivyo tumekuta yalivyo.
Hivyo badala ya kubishana nayo kwa kulazimisha kile tunachoona ni sahihi, ni bora kwenda nayo kama ilivyo ili tuweze kupata kile tunachotaka.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tunakazana kutoa thamani kubwa kwa wengine kwanza kabla ya kutaka kupata au kujinufaisha.
Ni kupitia utoaji wa thamani kubwa ndiyo tunajiweka kwenye nafasi ya kupokea thamani zaidi.
Ni thamani ipi kubwa unayokazana kutoa kwa wengine kabla hata hujapata chochote kutoka kwao?
Hicho ndiyo kipimo cha ni mafanikio makubwa kiasi gani unayoweza kuyajenga.
Mara zote fikiria kwa upande wa wengine kabla ya kufikiria upande wako.
Hilo litakupa fursa kubwa kwenye zama hizi ambazo kila mtu anajifikiria yeye mwenyewe zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe