Rafiki yangu mpendwa,

Lengo la kupambana na kujenga utajiri kwenye maisha ni kuwa huru. Uhuru unaoupata ndiyo unakuepusha na manyanyaso ya kifedha ambayo yamekuwa yanawaandama watu wengi na kufanya maisha yao kuwa magumu.

Unapokuwa unaanzia chini kabisa, manyanyaso ya kifedha huwa hayakosekani. Kwa sababu unakuwa unawahitaji wengine kwenye kila fedha unayoingiza. Hivyo pale watu unaowategemea wanapokukwamisha, mambo yako yanakwama.

Lakini hilo halipaswi kwenda kwa kipindi chote cha maisha yako. Kadiri unavyojenga utajiri, ndivyo pia unapaswa kujikinga na manyanyaso ya kifedha.

Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa wanaendelea kubaki kwenye hayo manyanyaso ya kifedha licha ya kuwa na mali na thamani kubwa ya utajiri.

Unakuta mtu anamiliki mali zenye thamani kubwa, lakini anapokuwa na shida ya kiasi fulani cha fedha, hawezi kupata kiasi hicho kwa haraka. Matokeo yake ni kuishia kunyanyasika kwa kukosa kile alichohitaji au kupata fedha kwa namna ambayo inamuumiza. Mfano kulazimika kuchukua mikopo ambayo anailipa kwa riba.

Ili kuondoka kwenye hayo manyanyaso ya kifedha, unapaswa kujijengea kiasi cha kutosha cha ukwasi kwenye utajiri unaoujenga. Ukwasi ni kiasi cha fedha unachoweza kukipata kwa haraka pale unapokuwa unakihitaji.

Eneo la ukwasi ndilo ambao watu wengi wamekuwa hawalielewi kwa sababu hakuna mahali linafundishwa kwa uhakika. Watu wanaweza kukazana kujenga utajiri mkubwa, lakini wasiwe na ukwasi. Pale wanapokuwa na uhitaji wa fedha na kuzikosa ndiyo wanashindwa kuelewa wamejikutaje kwenye hali ngumu kiasi hicho.

Lengo langu kubwa ni kuhakikisha kila anayekazana kujenga utajiri basi anakuwa na kiasi cha kutosha cha ukwasi ili aweze kuwa huru kifedha. Kadiri unavyojenga utajiri, ndivyo pia uweze kuepuka manyanyaso ya kifedha ambayo yanawatesa wengi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina tofauti ya utajiri na ukwasi na kiasi sahihi cha ukwasi cha kuwa nacho ili uweze kuwa huru kifedha na kuepuka manyanyaso ya kifedha. Karibu uangalie kipindi hiki na ukachukue hatua ya kujijengea ukwasi utakaokuweka huru kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.