Rafiki yangu mpendwa,
Safari ya mafanikio ina vikwazo vingi sana. Wengi wanayataka mafanikio makubwa, lakini wamekuwa hawayapati. Na kwa ambao wanapambana na kuyapata, wanakuja kujikuta hawana furaha licha ya kuwa na mafanikio. Hali hizo zimekuwa zinawachanganya watu wengi na hata kuwakatisha tamaa kwenye kuyapambania mafanikio.

Wajapani wana dhana wanayoiita IKIGAI, ambayo inamaanisha maana ya maisha ya mtu hapa duniani. Kwa dhana hiyo, mtu anapaswa kuwa na kitu ambacho anakifanya na kinayafanya maisha yake kuwa na maana. Kwa mtu kufanya kitu hicho, anapata ridhiko kubwa ndani yake, lakini pia anapata mafanikio.
Kwa mtu kujua IKIGAI yake, anakuwa amejihakikishia mafanikio makubwa na furaha ya kudumu. Hapa tunakwenda kujifunza dhana hiyo na jinsi unavyoweza kuifanyia kazi ili ufanikiwe na kuwa na furaha ya kudumu.
SABABU 4 ZA KUFANYA.
Dhana ya IKIGAI inaanza na sababu kubwa nne za mtu kufanya kitu. Yaani msukumo unaompeleka mtu kwenye kufanya kitu anachokuwa anafanya.
Sababu ya kwanza ni KUPENDA kufanya.
Hapa ni pale mtu anapofanya kitu kwa sababu anapenda kukifanya. Hapa mtu anakuwa tayari kufanya hata kama hakuna mtu anayemlipa. Hivi ni vile vitu ambavyo vinatoka ndani ya mtu hasa, kulingana na mapenzi yake binafsi.
Mfano hapa ni vipaji ambavyo mtu unaweza kuwa navyo na kupenda kufanya.
Sababu ya pili ni UJUZI wa kufanya.
Hapa ni pale mtu unapofanya kitu kwa sababu unajua jinsi ya kukifanya. Yaani mtu unakuwa vizuri kwenye kufanya kitu hicho, kulingana na elimu uliyopata na/au uzoefu ambao umejijengea. Kwenye vitu hivi, mtu anakuwa vizuri kwenye kuvifanya kuliko wengine wanaofanya.
Mfano hapa ni ujuzi ambao mtu unakuwa umejifunza na kujenga uzoefu.
Sababu ya tatu ni KULIPWA kufanya.
Hapa ni pale mtu unapofanya kitu kwa sababu watu wengine wanakulipa kwa kukifanya. Kwa kuwa kuna watu wapo tayari kukulipa kwenye kufanya kitu hicho, unakuwa na msukumo mkubwa wa kukifanya. Na kama tunavyojua umuhimu wa fedha, hivyo msukumo huwa ni mkubwa.
Mfano hapa ni kazi za kuajiriwa au biashara ambazo watu wanafanya na kulipwa.
Sababu ya nne ni MAHITAJI ya dunia.
Hapa ni pale mtu unapofanya kitu kwa sababu dunia ina uhitaji mkubwa wa kitu hicho kufanyika. Hapa unasukumwa na kutoa mchango wako kwa ajili ya kuifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.
Mfano hapa ni vitu ambavyo watu wanajitolea kwa ajili ya wengine.
AINA 4 ZA KAZI.
Kwa kuleta pamoja sababu mbili kati ya nne za kufanya, tunapata aina nne za kazi ambazo watu wanafanya.
Aina ya kwanza ni MISHENI.
Misheni ni kazi inayotokana na vitu unavyopenda kufanya na mahitaji ya dunia. Unakuwa unapenda kufanya kitu, lakini pia kwenye kukifanya unatoa mchango kwa dunia.
Hii ni kazi ambayo inamridhisha mtu anayeifanya, lakini haiwezi kumpa utajiri kwa sababu hawezi kuingiza kipato kikubwa kwa kazi ya aina hiyo.
Mfano ni uanaharakati wa aina yoyote ile. Mpaka mtu kuwa mwanaharakati kuna kitu anakuwa anapenda na kuona dunia inataka mchango wake kwenye kitu hicho. Mfano haki za binadamu, mazingira, usawa n.k.
Aina ya pili ni MAPENZI.
Mapenzi ni kazi inayotokana na vitu unavyopenda kufanya na vile ambavyo una ujuzi wa kuvifanya. Hapa unakuwa vizuri kwenye kufanya kile unachofanya na unapenda sana kufanya.
Kazi hii inampa mtu hali ya kuridhika, lakini anakosa maana kwa sababu inakuwa haina mchango mkubwa kwa wengine. Pia kunakuwa hamna njia ya mtu kuingiza kipato kikubwa kwa kazi hii, hivyo mtu hawezi kujenga utajiri.
Mfano ni vipaji ambavyo mtu anapenda kuvifanyia kazi, lakini havina mchango kwa wengine wala havimwingizii kipato.
Aina ya tatu ni WITO.
Wito ni kazi inayotokana na kike ambacho mtu analipwa kufanya na kina uhitaji kwa dunia. Hapa mtu analipwa kwa kufanya kitu ambacho kina mchango mzuri kwa watu wengine.
Kazi hii huwa inampa mtu shauku kubwa kwenye kufanya, lakini huwa inamweka kwenye hali ya kutokuwa na uhakika, kwa sababu anakuwa hana ujuzi mkubwa kwenye kuifanya.
Mfano ni kazi za kujitolea ambazo zinatoa mchango kwa wengine na mtu analipwa.
Aina ya nne ni TAALUMA.
Taaluma ni kazi inayotokana na ujuzi ambao mtu anao na kulipwa kwa kile anachofanya. Kwa taaluma, mtu anakuwa vizuri kwenye kitu na kulipwa kupitia kitu hicho.
Kazi hii huwa inampa mtu hali ya kuridhika, lakini inamfanya ajione ni mtupu kwa kazi hiyo kukosa mchango kwa watu wengine. Hapa ndipo mtu anaweza kufanikiwa sana lakini bado asiwe na furaha kwa sababu haoni maana ya kile anachofanya.
Mfano hapa ni kazi zinazowalipa watu fedha nyingi, lakini hazina manufaa makubwa kwa wengine, kama michezo ya bahati nasibu na kamari.
IKIGAI.
IKIGAI, ambalo ndiyo lengo, inapatikana pale unapoleta pamoja sababu zote nne na aina zote nne za kazi.
IKIGAI inakuwa ni kazi ambayo unapenda kuifanya, uko vizuri kuifanya, unalipwa kufanya na ina mchango kwenye dunia.
Ukiweza kuleta vitu hivyo pamoja, unapata kitu chenye maana kubwa kwenye maisha yako, ambacho kitakupa mafanikio makubwa na furaha ya kudumu.
HATUA YA KUCHUKUA.
Anzia hapo hapo ulipo sasa na kwa kazi au biashara unayofanya kisha jiulize maswali haya manne;
1. Nini napenda sana kwenye hiki ninachofanya?
2. Ni wapi niko vizuri kwenye hiki ninachofanya?
3. Nalipwaje kwenye hiki ninachofanya?
4. Nina mchango gani kwenye dunia kwenye hiki ninachofanya?
Tafakari kwa kina mpaka upate majibu ya maswali hayo manne na uyatumie kwenye ufanyaji ili ujenge mafanikio na furaha. Kama hupati majibu, jiulize unawezaje kutengeneza majibu kupitia hicho unachofanya au unawezaje kuhusisha na kitu kingine ili upate majibu hayo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeelezea kwa kina dhana hii ya IKIGAI na hatua hizi za kuchukua. Karibu usikilize kipindi na uendelee kujifunza ili ukachukue hatua sahihi na kujenga mafanikio pamoja na furaha ya kudumu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.