Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mwendelezo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, masomo yanayotujenga kuwa wauzaji bora kwa kutupa maarifa na hatua za kuchukua ili kukuza zaidi mauzo.

Maeneo makubwa mawili tunayoyafanyia kazi kwa uhakika ili kukuza mauzo ni USAKAJI ambao ni kutengeneza wateja wapya tarajiwa mara zote na UFUATILIAJI ambapo ni kuwafuatilia wateja kwa karibu bila kukoma.

Kwenye usakaji, kauli mbiu yetu kuu ni USAKAJI NDIYO PUMZI YA BIASHARA, UNAPASWA KUFANYIKA MARA ZOTE. Zipo njia mbalimbali za kusaka na kufuatilia wateja, moja wapo ni kwa kutuma jumbe fupi za simu (SMS).

Kuwafikia wateja kwa kutumia jumbe fupi za simu ni njia rahisi ya kuwafikia wateja wengi kwa muda mfupi, lakini ambayo ushawishi wake ni mdogo kuliko kukutana na watu ana kwa ana au kuongea nao kwa njia ya simu.

Lakini bado ni njia ambayo unapaswa kuitumia kwenye kusaka wateja na kuwafuatilia kwa karibu ili waweze kununua.

Kuwafikia wateja kwa kutumia jumbe fupi za simu kupo kwa aina mbili. Moja ni kutuma ujumbe kwa mtu mmoja mmoja na mbili ni kutuma ujumbe kwa watu wengi kwa pamoja.

Kwenye somo la leo tunakwenda kujifunza kuwafikia wateja kwa kutuma ujumbe kwa mtu mmoja mmoja. Na somo linalofuata tutajifunza kutuma ujumbe kwa watu wengi kwa pamoja.

UJUMBE KWA MTU MMOJA MMOJA.

Kutuma ujumbe wa simu kwa mtu mmoja mmoja ni njia ya kuwafikia wateja kwa kuwatumia ujumbe ambao unaenda kwa mtu mmoja anayelengwa. Kwa kuwa ujumbe ni wa mtu husika, unakuwa na nafasi ya kugusa mambo yanayomhusu yeye moja kwa moja na hivyo kuongeza ushawishi.

Njia hii inapofanyiwa kazi vizuri inawafanya wateja kukujua na kuendelea kukukumbuka ili wanapokuwa na uhitaji wakutafute wewe. Pia jumbe unazotuma zinakuwa kwenye kumbukumbu ya simu na mteja anapokuwa na uhitaji anaweza kukutafuta kupitia jumbe ambazo ulimtumia.

Hivyo kila muuzaji anapaswa kutumia njia hii ya kutuma ujumbe kuwafikia wateja wengi zaidi.

SOMA; Usakaji Wa Wateja Kwa Kupiga Simu.

NYAKATI ZA KUTUMA UJUMBE KWA MTU MMOJA MMOJA.

Kuna nyakati mbalimbali ambapo kutuma ujumbe wa simu kwa mtu mmoja mmoja ni muhimu kwenye kuwafikia wateja na kuwashawishi kununua. Zifuatazo ni baadhi ya nyakati hizo na jinsi ya kuzitumia vizuri.

1. Mawasiliano ya mara ya kwanza na mteja.

Pale unapopata namba ya mteja ambaye hujawahi kuwasiliana naye, unaweza kutuma ujumbe mfupi wa simu kujitambulisha na kumfanya awe na shauku ya kutaka kusikia zaidi kutoka kwako. Hii inakuwa na manufaa pale unapokuwa na wateja ambao wanaweza wasiwe tayari kupokea simu yako kwa kuwa hawana namba yako.

Unapopata mawasiliano ya wateja na kuwatafuta ila wasiwe na mwitikio mzuri, wapelekee ujumbe ambao utawapa msukumo wa kutaka kujua zaidi na hivyo kukutafuta au kupokea simu yako.

2. Mara baada ya mazungumzo.

Mara baada ya mazungumzo na mteja, iwe ni ana kwa ana au kwa njia ya simu, unapaswa kumtumia ujumbe wa kushukuru kwa mazungumzo ambayo mmefanya na kumpa muhtasari mfupi wa yale mliyokubaliana. Kufanya hivyo kunahakikisha mpo upande mmoja na mteja na kinachoendelea kinajulikana kwa pande zote.

Kila baada ya mazungumzo na mteja mtumie ujumbe mfupi, itakutofautisha sana na watu wengine na utakuwa umeweka sawa kitakachoendelea.

3. Unapomkosa mteja kwenye simu.

Ukimpigia simu mteja na kumkosa, iwe ni hakupokea simu, hakupatikana au amekata simu, mtumie ujumbe mfupi wenye maelezo ya kile ulichotaka kuwasiliana naye huku ukimpa shauku ya kukutafuta au kupokea simu yako. Mara nyingi wateja wanaweza kukukwepa kwenye simu kwa mtazamo wa tofauti wanaokuwa nao, unapowatumia ujumbe unawafanya waone kuna kitu hawakuwa wamekijua wakati wanakukwepa.

Kila unapomkosa mteja kwa mawasiliano ya simu, mwachie ujumbe mfupi wa simu wenye ushawishi wa kumsukuma akutafute au awe tayari kupokea mawasiliano yako.

4. Kutuma taarifa mbalimbali.

Unaweza kutumia ujumbe mfupi wa simu kuwatumia wateja taarifa mbalimbali ambazo unataka wawe nazo. Pia kuwataka wateja wakutumie taarifa mbalimbali unazohitaji. Kuna taarifa mnaweza msielewane kwa mazungumzo ya simu, lakini kwa kuandika ujumbe, zinaeleweka vizuri.

5. Kutuma salamu mbalimbali.

Ujumbe mfupi wa simu ni mzuri kwa kutuma salamu mbalimbali kwa wateja. Salamu za sikukuu, salamu za pongezi, pole na nyingine unaweza kuzituma kwa ujumbe mfupi wa simu.

Pale unapokuwa na salamu za kutuma kwa wateja, fanya hivyo kwa kuwatumia wateja ujumbe mfupi wa simu.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMA UJUMBE KWA MTU MMOJA MMOJA.

1. Taja jina la mteja.

Mwanzo wa ujumbe taja jina la mteja, hilo linanasa umakini wake na kumfanya awe tayari kusoma kujua nini kinamhusu kwenye ujumbe huo.

2. Ujumbe uwe na mtiririko mzuri.

Ujumbe unaotuma kwa wateja uwe na mtiririko wa kunasa umakini, kujali maslahi, kuibua tamaa na kumpa hatua ya kuchukua. Mtiririko huo unafanya ujumbe kuwa na ushawishi zaidi kwa mteja kuliko ukiwa hauna mtiririko mzuri.

3. Ujumbe uwe na ushawishi wa mtu kujibu.

Ujumbe ukiwa tu ni wa taarifa, mteja anaweza kusoma na kusahau. Lakini unapokuwa na kitu ambacho kinamtaka ajibu, inamsukuma kujibu. Pale mteja anapojibu ujumbe, anakuwa ameufikiria kwa kina na hivyo kuukumbuka zaidi.

4. Usitume jumbe nyingi na zinazofanana.

Lengo la kutumia ujumbe mfupi kwa mtu mmoja mmoja ni kufanya yaonekane ni mawasiliano ya kawaida. Ukituma jumbe nyingi na zinazofanana, inamfanya mteja asiyape uzito mawasiliano hayo na hivyo ushawishi kupungua zaidi.

5. Andaa jumbe za kutuma mara kwa mara.

Huhitaji kuwa unaandika ujumbe upya kila wakati. Kwa zile jumbe unazotuma mara kwa mara, ziandae na kuzihifadhi, kisha wakati wa kutuma kwa wateja, zihariri ili ziendane na wateja unaowatumia. Zoezi hilo linarahisisha mawasiliano kwa sababu tayari jumbe zinakuwa zimeandaliwa kwa mtiririko mzuri.

Kama muuzaji, kutuma ujumbe mfupi kwa mteja mmoja mmoja ni moja ya njia muhimu ya kuwafikia wateja unayopaswa kuifanyia kazi. Unapofanyia kazi njia hii kwa usahihi, unaweza kuwafikia wateja wengi na kuwafanya waendelee kukukumbuka kitu kinachoongeza ushawishi kwao kununua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.