Rafiki yangu mpendwa,

Utajiri ni thamani ya mali zote unazomiliki na kutoa madeni unayodaiwa, wakati ukwasi ni fedha unazoweza kuzipata kwa haraka.

Watu wengi wamekuwa wanakazana kujenga utajiri na kusahau kuhusu ukwasi, kitu ambacho kinawaweka kwenye hatari ya kunyanyasika kifedha pale wanapokuwa na uhitaji wa fedha na hawawezi kuzipata kwa haraka.

Ili kuondokana na manyanyaso hayo, tumekuwa tunasisitizana kujenga ukwasi wa kutosha, ambao ni angalau asilimia 50. Yaani nusu ya thamani ya utajiri wako iwe kwenye njia ambayo ni rahisi kubadili kuwa fedha taslimu.

Kwa kuwa na kiasi hicho kikubwa cha ukwasi, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukabiliana na chochote kinachotokea kwenye maisha yako. Lakini pia hilo linakuja na changamoto zake. Kadiri unavyokuwa na ukwasi mkubwa, ndivyo pia unavyojikuta kwenye mitego ambayo inahatarisha kupoteza kabisa ukwasi huo.

Hapa tunakwenda kujifunza kuhusu mtego wa kuwa na ukwasi mkubwa na hatari zake ili tuweze kuepuka na kujenga utajiri ambao unatupa uhuru mkubwa kwenye maisha yetu.

Mtego mkubwa wa kuwa na ukwasi ni matumizi ambayo yanaweza kuwa magumu sana kuyakwepa. Kwa watu wengi, kitu pekee ambacho wanajua kuhusu fedha ni matumizi. Ndiyo maana fedha zinapokuwepo huwa hazikosi matumizi. Fedha huwa zinakaribisha matumizi mpaka pale zinapoisha ndiyo matumizi nayo yanaisha.

Kwa kuwa na ukwasi mkubwa, pale matatizo yanapojitokeza unaweza kushawishika kuyatatua kwa kutumia ukwasi ulionao. Utaona kama ni jambo la msingi unafanya, lakini matokeo yake ni kupoteza ukwasi uliokuwa nao huku matatizo yakiwa hayajaisha.

Mtego mwingine kwenye kuwa na ukwasi mkubwa ni kuchangamkia fursa nzuri zinazojitokeza. Kuna fursa ambazo huwa zinaonekana ni nzuri na hupaswi kupitwa nazo. Fursa hizo zingekukuta ukiwa huna ukwasi, usingehangaika nazo na ungebaki na utulivu wako. Lakini kwa kuwa na ukwasi, unaona hupaswi kupitwa na fursa hizo nzuri. Hapo unajikuta ukishawishika kuingia kwenye fursa, ambazo mara nyingi zinakuwa siyo sahihi kwako.

Watu wengi wamepoteza ukwasi wao kwa kuhangaika na fursa ambazo hawana uelewa wa kutosha. Tamaa ya kunufaika kwa haraka na ukwasi wanaokuwa nao inawaweka kwenye hatari ya kupoteza ukwasi wao.

Watu kushindwa kutulia pale wanapokuwa na fedha huwa pia inawavutia watu wengine kwao, ambao wanawashawishi kutumia fedha hizo. Ukiwa na fedha na watu wasijue unazo, unakuwa na maisha tulivu. Lakini ukiwa na fedha na watu wakajua unazo na unaweza kuzitumia kwa urahisi, unawafungulia milango ya kuja kwako na ushawishi wa kila aina ili kuzipata.

Njia pekee ya kuepuka mtego wa ukwasi na hatari za kuupoteza ni kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana juu ya ukwasi wako. Kwa ukwasi wowote ulionao, sahau kama unao. Kwa sababu una akiba mahali, haimaanishi kwamba unapaswa kuitumia. Au kwa sababu umepata shida fulani, haihalalishi wewe kutumia fedha ulizonazo. Mara zote fikiria kama vile huna fedha ulizonazo na hapo utaona fursa nyingine za kukabiliana na chochote unachokuwa umekutana nacho.

Kama huna nidhamu ya kutosha ya kukuwezesha kutulia na ukwasi unaoujenga, ni bora kufanya uwekezaji kwenye mali ambazo siyo rahisi kuzigeuza kuwa fedha. Hilo litakuweka kwenye hali ya kunyanyasika, lakini angalau unabaki na mali zako. Ukiwa na ukwasi, ni rahisi kuutumia na ukishautumia unabaki mikono mitupu. Lakini ukiwa na mali ambazo siyo rahisi kugeuza kua fedha, ukiwa na uhitaji wa fedha na ukazikosa, utanyanyasika, lakini mwisho wa siku utabaki na mali zako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimefafanua kwa kina mtego huu wa ukwasi na jinsi ya kuuvuka ili uweze kujijengea uhuru wa kifedha na kuepuka manyanyaso ya kifedha kwenye maisha yako. Karibu usikilize kipindi na uchukue hatua ili kujijengea uhuru wa kifedha.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.