
Kwenye maisha kila mtu kuna gharama anaingia katika kupata kitu fulani. Hii tunaiona pale tunapotaka kufanya mawasiliano na watu wa karibu yetu kutumia simu. Ili ufanikiwe katika hilo lazima uweke salio.
Katika biashara pia, ili ufanikiwe unatakiwa kuingia gharama za kujifunza, kutafuta mtaji na mengine mengi.
Moja, ya gharama muhimu ya kuweka nguvu katika biashara ni kujenga uaminifu mkubwa. Ukiwa na uaminifu hutowekewa msharti kuwauzia wateja, tofauti na mtu asiye na uaminifu. Salio lako litakuwa linajitosheleza kuwahudumia.
Bilionea Warren Buffet aliwahi kusema, uaminifu ni zawadi ghali, kamwe usitegemee kuipata kutoka kwa watu wa kawaida, au watu rahisi”. Kwenye zama tulizomo sasa, ambazo ni zama za taarifa, uaminifu ni kitu muhimu sana.
Palipo na uaminifu, ndipo palipo na nguvu yetu kubwa ya kufanikiwa. Kwenye ndoa, unahitaji uaminifu. Kazini au kwenye biashara, kupitia uaminifu, ndipo utapata watu sahihi na waaminifu kama wewe.
Asili inaenda na asili. Waaminifu watakutana na waaminifu na waongo watakutana na waongo wenzao.
Kujenga uaminifu kwenye biashara ni kuonyesha viashiria vyote kuwa unaweza kuaminika. Stephen Covey katika kitabu chake cha “The 7 Habits of Highly Effective People ” anasema, kujenga uaminifu ni sawa na kitu alichoita; “Emotional Bank Account”. Ikiwa na maana kwamba kufanya vitu vinavyojenga uaminifu kama;
Moja; Kusema samahani.
Mbili; Kutimiza ahadi.
Tatu; Kuwa msikilizaji.
Kwa mjumuisho wa vitu tajwa hapo Covey anasema, ni sawa na kuingiza pesa kwenye akaunti yako ya benki (deposit). Hivyo, unapoenda kutoa pesa kwenye ATM au wakala hupati shida, pesa unazikuta. Kila unapotimiza ahadi, salio lako linaongezeka.
Anaendelea kusema kwamba kufanya vitu hivi;
Moja; Ukiwadanganya watu.
Mbili; Kutotimiza ahadi.
Tatu; Kuvunja uaminifu.
Mjumuisho wa vitu tajwa hapo juu Covey anasema, hapo umefanya kitu kinaitwa (withdraw) umetoa pesa zako. Pindi ukihitaji pesa hiyo haitakuwemo kwenye akaunti yako ya benki. Kwa lugha rahisi salio ni sifuri(0). Kila unapodanganya salio lako linapungua.
Linapokuja suala la mauzo “salio” lako kubwa la uaminifu litategemea namna gani unavyojiweka karibu na watu. Ikiwa unasaidia watu, unakuwa mpole kwao, utaonyesha utu, upendo na msema ukweli. Basi jua salio lako litakuwa kubwa na watu watakuamini. Utakuwa tayari kuwauzia na wao wataweza kurudi katika biashara yako.
Kama ni simu salio likiwepo unaweza kufanya mawasiliano na watu wako wa karibu.
Ukikosea tu na kuanza kufanya mambo yasiyotakiwa kama uongo, uchonganishi, kuwaingilia watu katikati ya maongezi, kuvunja ahadi, kuwa na ukatili na kukosa usikivu. Salio lako la uaminifu linapungua na watu watakaa mbali na wewe.
Ukigundua salio lako la uaminifu limeanza kupungua, haraka sana omba msamaha na anza kuongeza salio kwa kufanya yale yanayotakiwa. Maana, watu mara zote hupenda kuungana na watu wanaowaamini katika maisha na utendaji wao. Wasalimie watu, kuwa na utu, timiza ahadi na ungana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Uaminifu unaohifadhi kwa watu ndio unaokurudia wakati wa mauzo. Ukimpatia huduma nzuri mteja akafurahia, unawekeza uaminifu kwake. Anapohitaji huduma yako hawezi kwenda pengine bali atakuja kwako.
Bila uaminifu hakuna biashara utafanya na ikafanikiwa. Uaminifu ni msingi wa mahusiano bora kwenye mauzo. Kujenga uaminifu inabidi uwe tayari kuaminika, usivuke hatua.
Hatua za kuchukua; Dhibiti mihemko yako, kaa kwenye mchakato, timiza ahadi na kuwa na nidhamu bora. Watu hujenga urafiki na hununua huduma yako kwa sababu ya uaminifu ulio ndani yako.
Imeandaliwa n Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na Mwandishi. Tuwasiliane 0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.