Rafiki yangu mpendwa,
Ndani yako tayari unao uwezo mkubwa wa kujenga mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka wewe mwenyewe. Huo ndiyo ukweli ambao wengi hawaujui na hata wale wanaoujua hawauamini na ndiyo maana hawafanyii kazi.
Lakini uwezo na matokeo ni vitu viwili tofauti, licha ya kuwa na uwezo mkubwa, matokeo unayoyapata hayaendani na uwezo huo. Na siyo kwamba huweki juhudi, unaweza kuwa unaweka juhudi kubwa sana, lakini bado matokeo yanakuwa siyo sawa na uwezo ulionao.
Kikwazo kinachokuzuia usipate mafanikio licha ya kuwa na uwezo na kuweka juhudi ni breki ambazo umezishikilia. Kama ambavyo ukiendesha chombo chochote kikiwa na breki hakiwezi kuwa na kasi, ndivyo pia breki binafsi unazokuwa nazo zinavyozuia uwezo wako na juhudi zako visikupe mafanikio.

Zipo njia mbalimbali za kuachilia breki ambazo zinakukwamisha na moja ya njia hizo ni kutumia ubunifu. Ubunifu ni kitu kingine ambacho kila mtu anacho, lakini wengi wamekuwa hawakitumii. Wewe hapo tayari unao ubunifu mkubwa ndani yako, ambao ukiweza kuutumia utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Licha ya kila mtu kuwa na ubunifu, bado wengi wanashindwa kutumia ubunifu huo kufanya makubwa. Na hiyo ni kwa sababu kuna vikwazo vitano ambavyo watu wamekuwa wanajiwekea kwenye ubunifu, ambavyo wakiweza kuvivuka, watafanya makubwa sana.
Kikwazo cha kwanza ni hofu ya mabadiliko.
Watu huwa wanapenda kufanya vitu walivyozoea kufanya kwa sababu tayari wana uhakika na matokeo wanayoyapata, hata kama ni madogo. Kujaribu vitu vipya ambavyo vinaweza kuwapa matokeo makubwa zaidi huwa wanahofia kwa sababu ya kukosa uhakika wa matokeo. Watu wengi huwa wana hofu ya kubadili yale wanayofanya na bila mabadiliko hakuna ubunifu.
Kuondokana na kikwazo hiki, yapende mabadiliko, kila wakati chukua hatua ndogo ndogo za mabadiliko ambazo zitakuweka kwenye ubunifu na kupata matokeo ambayo ni ya tofauti. Jilazimishe kubadilika hata pale matokeo yanapokuwa ni mazuri, kwani ukisubiri mpaka unapolazimika kubadilika, unakuwa umeshachelewa.
Kikwazo cha pili ni kujiona siyo mbunifu.
Watu hudhani ubunifu ni kitu ambacho kuna watu wanacho na wengine hawana. Kwamba kuna watu walizaliwa wakiwa wabunifu na wengine wakazaliwa siyo wabunifu. Hili siyo sahihi, kila mtu ni mbunifu, tofauti ni kwenye matumizi ya ubunifu huo. Kila mtu anajua kupangilia mavazi yake ili asiwe kituko. Kila mtu anajua kutafuta njia za mkato pale anapotaka kuwahi mahali. Hivyo vyote ni viashiria vya ubunifu ambao upo ndani ya kila mtu.
Kuondokana na kikwazo hiki, jua kwamba wewe tayari ni mbunifu. Kubali kwamba ndani yako unao ubunifu na wajibu wako ni kuutumia ili kufanya makubwa. Angalia mambo mengi ambayo umeshayafanya kwa utofauti na utaona wazi jinsi ambavyo umekuwa unatumia ubunifu kwenye maisha yako.
Kikwazo cha tatu ni kuona kitu ni kigumu au hakiwezekani.
Mtazamo unaokuwa nao kuhusu kitu unaathiri sana uwezo wako wa kutumia ubunifu katika kukifanya. Ukishasema kitu ni kigumu au hakiwezekani, unakuwa umefunga kabisa fikra zako juu ya kitu hicho. Unakuwa umehitimisha kwamba hakiwezi kufanyika na hivyo hakuna haja ya kuhangaika nacho.
Kuondokana na kikwazo hiki, jua kila kitu kinawezekana. Hata kama huoni ni jinsi gani ya kufanya kitu, kamwe usijiambie hakiwezekani. Badala yake jiulize kinawezekanaje na hapo utafungua fikra zako ili kutafuta njia ya kuweza. Hapo ndipo ubunifu unapochochewa na mtu kuweza kufanya makubwa.
Kuna vikwazo vingine viwili ambavyo vinawazuia watu kutumia ubunifu wao, na pia kuna hatua 20 za kuchukua ili kuchochea na kutumia ubunifu ulio ndani yako kuweza kufanya makubwa na kufanikiwa kwenye maisha yako. Hayo yote yapo kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambacho kipo hapo chini. Fungua kipindi hicho na ujifunze ili utumie huo ubunifu ulionao kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.