Kama Unataka Kupata Mafanikio Makubwa Sana, Zaliwa Upya Kabisa.

Rafiki yangu mpendwa,

Watu kwenye jamii wamegawanyika kwenye makundi haya, ukichukua watu 100;

Asilimia 1 wanakuwa na mafanikio makubwa sana kuliko asilimia 99.

Asilimia 4 wanakuwa na mafanikio ya juu, lakini siyo makubwa sana.

Asilimia 15 wanakuwa na mafanikio ya kati.

Na asilimia 80 wanakuwa hawana mafanikio kabisa, yaani wanakuwa na maisha ya chini.

Kwenye kila jamii, namba zipo hivyo, hata watu wakazane kiasi gani, bado namba zinabaki hivyo hivyo.

Kwa jinsi namba hizo zinavyokuwa na msimamo, inaweza kuonekana kama tayari maisha ya watu yameshaamuliwa, kama watafanikiwa au watashindwa.

Kwamba juhudi anazoweka mtu hazina nguvu kubwa ya kubadili matokeo ambayo anaweza kuyapata.

Hilo ni kweli na siyo kweli.

Siyo kweli kwa sababu juhudi ambazo tunaweka zina mchango mkubwa kwetu kupata matokeo ya tofauti na yale tuliyozoea kupata. Hivyo kuweka kazi kwa juhudi ni hitaji muhimu la kuwa na maisha bora.

Na ni kweli kwamba kupata mafanikio makubwa sana, yaani yale makubwa kuliko wote, kuna vitu huwezi kujifunza au kufundishwa. Vitu hivyo vinakuwa tayari ndani ya mtu. Hivyo anayekuwa navyo anayapata mafanikio hayo makubwa na asiyekuwa navyo hayapati.

Hii ni kuonyesha kwamba kuna namna mtu unaweza kuwa umezaliwa na kuwa umeandaliwa kupata mafanikio makubwa au kuyakosa. Kwa mfano mtu ambaye ni mrefu, ana nafasi kubwa ya kupata mafanikio zaidi kwenye mchezo wa mpira wa kikapu kuliko mtu ambaye ni mfupi.

Lakini sasa, kuna vitu viwili ambavyo unapaswa kuvijua kabla hujakubaliana na hili na kujiona labda wewe upo kwenye fungu la kukosa.

Kitu cha kwanza ni watu wengi wanaishi maisha yao kwa kufuata mkumbo na kuiga wengine. Hawajawahi kukaa chini na kujihoji kisha kujisikiliza wao wenyewe ni nini hasa wanachotaka kwenye maisha. Hawajawahi kujua uimara wao uko kwenye maeneo gani hasa. Matokeo yake wanawaiga wengine na kuingia kwenye vitu ambavyo siyo uimara wao. Hivyo hata waweke juhudi kiasi gani, bado wanaishia kupata matokeo ya kawaida tu. Matokeo makubwa yanakuwa ni kitu kigumu sana kwao kupata.

Kuondokana na hali hii unapaswa kujitambua wewe mwenyewe, kuisikiliza sauti yako ya ndani na kufanya yale ambayo kwako ni kama mchezo wakati kwa wengine ni kazi ngumu. Tumia zaidi uimara wako na puuza madhaifu yako, hilo litakuweka kwenye nafasi ya kuweza kufanya makubwa kuliko wengine.

Kitu cha pili ni sisi binadamu tunao uwezo mkubwa sana wa kubadili kitu chochote kile. Tunaweza kujibadili sisi wenyewe kwa kujifanyia mageuzi ambayo yanatufanya kuwa watu wa tofauti kabisa. Tunaweza kujijenga kuwa watu wapya kabisa na wenye sifa za tofauti kabisa. Kama umewahi kupata au kumwona mtu mwenye ugonjwa wa akili, utakuwa umeona jinsi ambavyo mtu anaweza kubadilika kabisa.

Kuweza kutumia uwezo huo wa kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kujipitisha kwenye ubatizo wa moto. Ubatizo wa moto ni pale unapopitia mateso makali ambayo yanakugeuza kabisa, kukutoa kuwa mtu wa aina moja na kwenda kuwa mtu wa aina nyingine ya tofauti kabisa. Hili ni zoezi gumu na linalokutaka mtu ujitoe hasa, lakini lina matokeo mazuri.

Hivyo basi rafiki, kama unayataka mafanikio makubwa sana, fanya hayo mawili kwa wakati mmoja, jitambue wewe mwenyewe kisha jipe ubatizo wa moto ili uimarike kwenye yale maeneo ambayo una uimara mkubwa.

Na wakati bado ukiwa hapo kwenye kujifanyia mageuzi ili kuweze kupata mafanikio makubwa sana, kuna tabia saba za msingi ambazo unapaswa kujijengea ili ufanikiwe. Tabia hizo walionazo wengi wamezaliwa nazo na zinawapa faida sana. Wewe kama huna, inakubidi upitie ubatizo wa moto kuzijenga.

Jifunze tabia hizo saba na jinsi ya kuzijenga kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Fungua kipindi, jifunze kisha nenda chimbo ukajifanyie mageuzi makubwa na yatakayokuweka kwenye nafasi ya kujijengea mafanikio makubwa sana.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.