Rafiki yangu mpendwa,
Ndoa za Kikristo huwa zina hicho kipengele kwamba watu wameungana pamoja na kuwa mwili mmoja na atakwenda hivyo mpaka kifo kiwatenganishe. Maana nzima ya hilo ni watu kupambania umoja wao kwa sababu hawana njia nyingine. Kila kitu huwa kina changamoto na mahusiano yana changamoto nyingi. Kama watu hawapo tayari kuzikabili changamoto na kuzivuka, mahusiano hayawezi kudumu. Hata wingi wa talaka zilizopo kwenye ndoa kwenye zama hizi, ni kukosekana kwa uvumilivu wa kuzikabili na kuzivuka changamoto.
Tatizo hilo la kuongezeka kwa talaka haliishii tu kwenye ndoa, bali linakwenda mpaka kwenye mafanikio pia. Watu wengi sana wametoa talaka kwenye safari yao ya mafanikio na ndiyo maana hawafanikiwi. Kila wanapoianza safari ya mafanikio, inajitokeza ‘michepuko’ ambayo inanasa umakini wao. Wanasahau kuweka umakini wa kutosha kwenye ndoa yao ya mafanikio na hapo wanaishia kushindwa.

Mafanikio yanakutaka mtu uweke umakini wako wote kwenye kile unachofanya na unachotaka kikupe mafanikio makubwa. Hicho ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako na hakupaswi kuwa na usumbufu mwingine wowote.
Kwa bahati mbaya sana, pale unapochagua kile unachopambania ili kufanikiwa, vitu vingine vya pembeni ambavyo vinaonekana ni vizuri na rahisi vinaanza kujitokea. Hivyo sasa ndiyo michepuko ambayo inakuja kuharibu kabisa ndoa yako ya mafanikio. Uimara wa ndoa yako ya mafanikio unategemea sana uwezo wako wa kushinda vishawishi vya fursa nyingi mpya zinazokuja na kuonekana ni bora.
Ili uweze kujenga mafanikio makubwa kadiri ya unavyohitaji, unapaswa kufunga ndoa moja na kile ulichochagua kufanikiwa na kula kiapo cha kwamba ni mpaka kifo kiwatenganishe. Kwamba hautahangaika na mambo mengine yoyote isipokuwa hilo kuu ulilochagua. Kwamba utapuuza vitu vizuri vinavyoonekana na kuendelea kufanyia kazi njia uliyochagua, hata kama ni ngumu.
Wengi hawana maamuzi ya aina hii na ndiyo maana wamekuwa wanajikwamisha wao wenyewe kujenga mafanikio makubwa. Wanayumbishwa na vitu vipya vinavyoonekana ni rahisi zaidi. Au wanakata tamaa pale wanapokutana na magumu na changamoto.
Wewe epuka hiyo njia, wewe endelea na safari yako ya mafanikio. Endelea kujifunza na kuchukua hatua, huku pia ukiboresha hatua unazochukua kulingana na matokeo unayokuwa unayapata. Ni kwa mwenendo huo ndiyo unaweza kujenga mafanikio makubwa na ya uhakika kwenye maisha yako.
Karibu ujifunze kwa kina zaidi juu ya dhana hii ya kufunga ndoa na mafanikio yako na kuweka kiapo cha mpaka kifo kikutenganishe. Halafu unaheshimu kiapo hicho kweli. Angalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ujifunze na kuchukua hatua ili ujijengee mafanikio makubwa na kwa uhakika.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.