
Sera ya mauzo ni misingi au miongozo inayokuongoza katika kuwahudumia wateja wako. Sera hii inaainisha mambo muhimu ya kuzingatia ili kuwauzia wateja wengi na kukuza mauzo.
Wauzaji waliofanikiwa wanaelewa dhana za sera ya mauzo na wanazitumia kwa kila mteja wanayekutana naye. Malengo makuu ni kuhakikisha hakuna mteja anayeondoka bila kuridhika au kununua. Sera hizo ni kama zifuatavyo;
Moja; Mauzo ni namba.
Dunia ya sasa ina habari nyingi, karibu kila mtu ni mwanahabari, hivyo tukio lolote linalotokea wapo tayari kulitoa kwa wengine. Hii kwa upande wa biashara ina nafasi ndogo sana. Ni kwa sababu haipimiki.
Namba ndiyo kitu pekee kinachopimika. Kama ni moja ni moja haina mjadala. Tofauti na taarifa. Mara zote ongozwa na namba ili kukuza mauzo yako. Kila unapokwama rudi kwenye namba. Uzuri wa namba zinakusaidia kupima ufanisi wa kila mmoja kwenye timu. Namba hazidanganyi.
Mbili; Mauzo ni mchakato.
Pata picha, wewe ni binti upo zako mtaani unatembea, ghafla unaona kijana anakusimamisha huku akisema amekupenda na anataka akuoe. Utamwambia sawa, au utakataa? Jibu ni utakataa. Sio kwamba hujampenda, ni kwa sababu humjui.
Ipo hivyo kwenye mauzo. Ni nadra sana kumkamilisha mteja siku ya kwanza, hasa mteja asiyekujua. Kuna vitu anahitaji kusikia pengine kuona kutoka kwako. Lengo ni aone kama kweli una nia ya kuuza au mbabaishaji.
Tatu; Mauzo ni uaminifu.
Binafsi nachukulia uaminifu kama mtaji usio na masharti. Ukiwa mwaminifu ni rahisi wateja kukuamini na kuiamini biashara yako.
Kitu muhimu unachotakiwa kufanya ni kutengeneza mazingira ya uaminifu kwa wateja wako. Washirikishe manufaa wanayoenda kupata baada ya kujiunga na huduma au kuchukua bidhaa yako.
Nne; Mauzo ni suluhu
Mgonjwa anapozidiwa na kwenda hospitalini, kitu cha kwanza anachohitaji kutoka kwa daktari ni tiba. Hii ndiyo suluhu ya kuponya ugonjwa au maumivu aliyonayo.
Hata katika biashara yako, utaratibu ni huo huo. Hakuna mteja anakuja kutalii katika biashara yako. Kuna maumivu anahitaji yaponywe. Ni biashara kibao ameziacha na kuja kwako. Hivyo, unatakiwa kutoa suluhisho kwa wateja wako. Waulize maswali sahihi ujue mahitaji yao ya msingi.
Tano; Mauzo ni huduma
Wateja wanataka kuona unawajali muda wote, kuanzia kuwapokea na kuzungumza nao. Mara baada ya kuwahudumia vema, unaweza kujenga uaminifu mkubwa. Na utaongeza nafasi ya kuwauzia zaidi ikiwa watahudumiwa vizuri.
Vitu vya kuzingatia hapa ni uharaka, mwonekano mzuri, uwepo katika eneo la biashara au kujua vema kile unachowahudumia. Hii itawafanya wajisikie vizuri na kuwashirikisha wenzao, habari njema kuhusu biashara yako.
Sita; Mauzo ni thamani
Wauzaji wengi wanashindwa kuwapa thamani wateja wao. Wengi huongelea kuhusu bidhaa na namba kampuni zao zinavyouza. Hali inayowafanya kushindwa kuwauzia wateja wengi.
Kama muuzaji unayetaka kukuza mauzo yako, mpe thamani mteja. Mweleze thamani anayoenda kupata baada ya kutumia bidhaa zako. Hii itamfanya awe tayari kufunguka kifedha pia. Ataona pesa yake haijapotea bure.
Saba; Mauzo ni Maswali.
Tafiti zinaonyesha zaidi ya asilimia 75% madaktari hupata majibu ya mgonjwa kutokana na maswali. Unaweza kuona umuhimu wa maswali katika kumkamilisha mteja.
Kitu muhimu ni kuuliza maswali yanayokupelekea kukamilisha mteja. Maswali yanayomfanya ajielezee zaidi, kuliko wewe kuongea. Mteja akiongea sana uwezo wa kumuuzia upo mkubwa.
Nane; Mauzo ni Ushawishi.
Wauzaji wawili, wanaweza kuwa sehemu moja na kuuza vituvinavyofanana lakini mmoja akauza zaidi ya mwingine. Sio kwamba anasali sana au kuwa na upako. Bali matumizi sahihi ya maneno ya ushawishi.
Habari njema kuhusu maneno ya ushawishi ni kwamba, ni maneno yanayomlazimisha mteja bila kuonekana analazimishwa. Kumuondolea jibu la hapana na kumrudisha kwenye hali ya mazoea. Hivyo, tumia maneno ya ushawishi uwezavyo mbele ya mteja.
Tisa; Mauzo ni majadiliano
Mauzo sio vita. Mauzo ni maelewano baina ya pande mbili. Kwa maana ya mteja na mnuzi. Kuyafanya mauzo kama vita ni kupoteza nguvu zako bure, kwani hakuna mteja anayependa kulazimishwa kuuziwa.
Unapokuwa katika biashara unapaswa kutumia fursa ya kuongea na mteja vizuri, mpe nafasi ya kuongea na kutoa yaliyo moyoni. Hali hiyo itamfanya aone wewe pia, unamjali. Mwishoni atakubali kukamilisha mauzo.
Kumi; Mauzo ni Ushindi.
Hapa ndipo kuna furaha ya kila muuzaji. Maana kupitia mauzo biashara inapata pesa. Pesa hiyo hutumika katika masuala mbalimbali ya kuendesha kampuni.
Kupitia Ushindi au kuuza ndipo muuzaji hupata hamasa na ari katika utendaji wake. Pambana sana kutafuta ushindi huu.
Hitimisho; Ili ufanikiwe kuendana na sera hizi hakikisha unawajua wateja wako, elewa vema biashara yako na uwe na uwasilishaji mzuri. Hakika utauza sana na kukamilisha malengo yako.
Je, ni sera ipi unatumia kama mwongozo katika biashara yako? Share na sisi hapa hapa.
Imeandaliwa na Lackius Robert Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo na mwandishi. Tuwasiliane
0767702659 au mkufunzi@mauzo.tz.