3356; Walichozoea kufanya.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Safari ya mafanikio huwa inakuwa ngumu kwa watu wengi kwa sababu ya wale wanaokuwa wanawazunguka.

Wengi wa wanaotuzunguka hawana mafanikio makubwa, na pia hawana mpango wa kupata mafanikio hayo makubwa.
Wameshakata tamaa kwenye hilo na kukubali kile ambacho dunia inawapa.

Watu hawa wasingekuwa na shida kama wangeendelea na maisha yao. Lakini sivyo wanavyofanya, badala yake wanakazana kuwakatisha wengine tamaa ili nao wasipambane kufanikiwa.
Kwa kuwa wao wamekata tamaa, basi wanahakikisha wanawakatisha wengine tamaa ili wasiendelee na safari ya mafanikio.

Unaweza kuwalaumu sana watu hao kwa hicho wanachofanya, lakini haitasaidia.
Kwa sababu wao wanafanya kile wanachoweza, ambacho ni kukata tamaa.
Kwa kuwa wao wameshakata tamaa, watataka na wengine pia wakate tamaa.
Anachojua ni kwamba kama atakata tamaa yeye mwenyewe, ataonekana ni mzembe.
Lakini kama kutakuwa na wengine ambao pia wamekata tamaa, inaonyesha mafanikio hayo ni magumu.

Pamoja na hayo yote ya mtu aliyekata tamaa kuwashawishi wengine nao wakate tamaa, tatizo siyo la anayewakatisha watu tamaa, bali wale wanaokubali kukatishwa tamaa.

Unakuwa umejidharau na kujitukana sana kama utakubali kukata tamaa kwa sababu ya kushawishiwa na wale ambao pia wamekata tamaa.

Watu hao waliokata tamaa huwa hawawezi kung’ang’ana na kitu kwa muda mrefu.
Hivyo hata zoezi lao la kuwakatisha wengine tamaa, huwa wanaishia kukata tamaa pale wanapokutana na watu wasiowakubalia kirahisi.

Usikubali kuwapa ushindi rahisi wakatishaji tamaa, kwa kukubali kukata tamaa kama wao.
Wakatalie na wataishia kukata tamaa, maana ndiyo tabia yao.

Kuwa umetingwa sana na kile unachofanya kiasi kwamba wakatishaji tamaa wanaogopa hata kukusogelea.
Wafanye wakate tamaa kabla hata hawajakufikia.
Na hilo litakuondolea changamoto hizo ndogo ndogo zinazowazuia wengi kufanikiwa.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, waliokata tamaa wanapuuzwa kabisa.
Hakuna chochote kinachosikilizwa kwao, hata kama kinaonekana ni kizuri.
Hiyo ni kuepuka wao kufanya kile ambacho wako vizuri, ambacho ni kuwakatisha wengine tamaa.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA hatuchukui tu ushauri kwa kila mtu. Bali tunawachuja kwanza na kuwaondoa wote waliokata tamaa kwenye orodha ya watu wa kujifunza kwao.
Hakuna kikubwa cha kujifunza kwa waliokata tamaa zaidi ya sisi kutokukata tamaa.
Hivyo hatuhitaji ukaribu wowote na watu hao, zaidi ya kuwaepuka ili wasifanye kwetu kile ambacho wako vizuri kukifanya.

Kukatishwa tamaa na mtu aliyekata tamaa ni uzembe wa hali ya juu sana. Unakuwa umeonyesha wewe uko vibaya kuliko hata wale wanaokukatisha tamaa.
Kwa sababu, kama ungewakazia kidogo tu, wangekata tamaa na kuachana na wewe, kwa sababu ndiyo tabia yao.

Pambania kile ulichochagua na waepuke wakatishaji tamaa wote, hakuna wanachoweza kukusaidia zaidi ya kutaka na wewe ukate tamaa kama wao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe