Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha unafanya kazi kwenye mgahawa wa chakula. Anakuja mteja na kukuomba umpe orodha ya vyakula vilivyopo. Anapotia na kisha kukuambia anataka wali nyama.
Unaondoka kwenda kumwandalia oda yake, lakini kabla hujakamilisha, anakuambia amebadili mawazo, anataka wali samaki. Unasema sawa, wakati unaanza kuandaa hicho, anakuita tena na kukuambia amebadili mawazo, anataka ndizi nyama.
Mpaka kufika hapo utakuwa unajisikiaje? Pamoja na kwamba mteja ni mfalme, bado utapata hasira kwa sababu mteja anakusumbua. Unamwona mteja hajui anachotaka na anaishia kukuchanganya.
Kabla hujamshangaa huyo mteja, napenda nikuambie hivyo ndivyo umekuwa unafanya kwa maisha yako yote na kimekuwa kikwazo kikubwa kwako kupata utajiri.

Umekuwa unabadili mawazo yako mara kwa mara, kitu ambacho kinaichanganya dunia na kupelekea kukosa kile unachokuwa unakitaka.
Picha inaenda hivi, unaamua kwamba unataka kupata utajiri kwenye maisha yako na hivyo kuwa tayari kujituma ili kuupata. Halafu unakutana na watu matajiri na kuanza kuwasema vibaya, kwamba matajiri ni watu wabaya na wasiojali.
Akili yako ilianza kwa kuona unataka utajiri, hivyo kuanza kukuandalia mazingira yatakayokuletea utajiri. Lakini unapoanza kuwachukia matajiri, akili yako inabidi iachane na kukutengenezea mazingira ya utajiri.
Unaendelea tena, wakati mwingine unapata msukumo wa kupata utajiri, lakini haikuchukui muda unaanza kujiambia utajiri haununui furaha, matokeo yake akili yako inazificha fursa zote za utajiri.
Iko hivi rafiki, akili yako huwa inakuonyesha kile tu ambacho unataka kuona. Kwa vitu ambavyo hutaki kuona au huvipendi, huwa inahakikisha huvioni ili visikusumbue.
Hivyo kama kweli unataka utajiri kwenye maisha yako, mawazo yako yanapaswa kuwa ya aina moja tu, kupata utajiri. Usikaribishe mawazo mengine yoyote kwenye akili yako ambayo yanaenda kinyume na mawazo hayo makuu ya utajiri.
Unapaswa kulinda sana akili yako ili kuhakikisha haichafuliwi na mawazo yanayokinzana na mawazo ya utajiri unayokuwa nayo. Ni kwa njia hiyo ndiyo akili yako itaweza kukuletea fursa nzuri za wewe kupata utajiri unaoutaka.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua zaidi hili la kuichanganya dunia kiasi cha kushindwa kupata utajiri ambao upo tayari kwa ajili yako. Fungua kipindi hicho ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi zitakazovunja vikwazo vyote vya utajiri ulivyojiwekea kwenye akili yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.