Rafiki yangu mpendwa,

Kama hujapata kile unachotaka kwenye maisha, siyo kwa sababu hakuna fursa za kukipata. Na wala siyo kwa sababu huna uwezo wa kukipata. Fursa ni nyingi sana za wewe kupata kila unachotaka. Na uwezo mkubwa sana tayari upo ndani yako wa wewe kupata chochote unachotaka.

Grant Cardone, kwenye kitabu chake kinachoitwa The 10X Rule: The Only Difference Between Success and Failure, ameeleza vikwazo vikubwa viwili vinavyokwamisha watu kufanikiwa. Vikwazo hivyo ni KUFIKIRI na KUFANYA kwa UDOGO.

Watu wanafikiri kwa udogo sana, kitu ambacho kinawapelekea kujiwekea malengo madogo. Kwa kuwa na malengo madogo, watu wanachukua hatua ndogo na kuishia kuwa na maisha ya kawaida.

Njia pekee ya kutoka kwenye huo mkwamo, ambayo Cardone anaifundisha ni kuwa na kiwango sahihi cha kufikiri na kufanya. Kiwango hicho ni kuzidisha MARA 10 ZAIDI (10X) ya vile ambavyo mtu umezoea kufanya.

Kwenye KUFIKIRI, Cardone anasema unapaswa kuweka malengo yako kwa ukubwa wa mara 10 zaidi ya unavyoweka sasa. Hayo yatakuwa malengo makubwa, yanayokusukuma sana na kukufanya ufikiri kwa ukubwa kuliko ulivyozoea kufikiri.

Cardone anaeleza kwamba, hakuna tofauti ya gharama au nguvu kwenye kufikiri kwa udogo na kufikiri kwa ukubwa. Unatumia akili ile ile na nguvu zile vile iwe utafikiri kwa udogo au kwa ukubwa. Sasa kwa nini usifikiri tu kwa ukubwa?

Lakini watu wamekuwa wanaambiwa hawapaswi kuweka malengo makubwa sana ambayo watashindwa kuyafikia, kwani yatawakatisha tamaa. Cardone anasema hayo siyo mafunzo sahihi, watu wanatakiwa kuwa na malengo makubwa hata kama hawatayafikia, kwani wakishindwa kwenye hayo malengo makubwa, bado wataishia kupata matokeo makubwa kuliko ambavyo wangepata kwenye malengo madogo.

Kwenye KUFANYA, Cardone pia anaeleza mtu anapaswa kuchukua hatua kubwa sana, mara 10 ya ambavyo mtu amezoea kufanya. Hiyo ni kwa sababu matokeo makubwa yanatokana na kuchukua hatua kubwa sana. Kwani sehemu kubwa ya hatua hizo hazitafanya kazi.

Kama unapanga kuuzia wateja 10, huwezi kuongea na watu 10 pekee na kutegemea wote wanunue. Badala yake unapaswa kuongea na watu wasiopungua 100 ndiyo uweze kupata kumi watakaonunua.

Kwa matokeo yoyote ambayo mtu unataka kuyapata, lazima uwe tayari kuweka juhudi mara kumi zaidi ya ilivyozoeleka kuwekwa. Na hapo ndipo utakapoweza kujisogeza karibu zaidi na mafanikio makubwa.

Kwenye KUFANYA pia Cardone ameshirikisha ngazi nne za ufanyaji, ambazo ni kama ifuatavyo;

Ngazi ya kwanza ni kutokufanya kabisa. Hapa mtu anakuwa hafanyi kabisa, yaani yupo tu na hakuna hatua anazochukua ili kupata matokeo ya tofauti.

Ngazi ya pili ni ya kurudi nyuma kwenye kufanya. Hapa mtu anakuwa anajitetea na kujipa sababu kwa nini hafanyi. Mtu anakuwa anatumia nguvu nyingi kujizuia kufanya.

Ngazi ya tatu ni hatua za kawaida. Hapa ni pale mtu anapofanya yale aliyozoea kufanya. Hii ni hatua ya hatari zaidi kwa sababu watu huwa wanaridhika na kuona wameshamaliza. Lakini ni hatua ambayo inawaweka watu kwenye mazoea ambayo yanawakwamisha kufanikiwa.

Ngazi ya nne ni hatua kubwa. Hapa mtu anachukua hatua ambazo ni kubwa sana kuliko ilivyozoeleka. Kwa hatua hizo kubwa, mtu anazalisha matokeo makubwa kuliko ilivyozoeleka. Hiki ndiyo kiwango sahihi cha kuchukua hatua ili kuweza kupata mafanikio makubwa.

Kitabu hiki cha 10X RULE kimeeleza mambo mengi ya kuzingatia kwenye KUFIKIRI na KUFANYA kwa ukubwa zaidi. Ni mwongozo muhimu kwa watu wote wanaotaka kupata mafanikio makubwa. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini, nimezielezea sura 21 za kitabu hicho na hatua ya kuchukua kwenye kila sura. Fungua kipindi ujifunze na kwenda kutumia viwango hivyo sahihi vya kufikiri na kufanya ili kujijengea mafanikio makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.