3358; Mchezo usio na mwisho.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Ukishaingia kwenye biashara, maana yake umejiandikisha kwenye mchezo ambao hauna mwisho.
Ni mchezo ambao utaendelea kuucheza kwa kipindi chote cha maisha yako, ila katika ngazi mbalimbali.

Unapoianza biashara, wajibu wako namba moja unakuwa ni kupata wateja ambao ni waaminifu kwenye biashara hiyo.
Hapo utahitajika kufanya kazi ya kuwafikia wateja tarajiwa wengi na kujenga nao mahusiano ili wawe wateja wa biashara yako.
Hii inakuwa ni kazi ngumu kwa mwanzoni, kwa sababu watu wanakuwa hawana imani na kitu kipya.
Na kwa sehemu kubwa, utakuwa unaifanya kazi hiyo wewe mwenyewe.

Ukishavuka hatua hiyo ya kwanza, kwa kuweza kuwa na wateja waaminifu kwenye biashara, ambao wananufaika na hata kuwaleta wengine. Katika ngazi hii, kuwahudumia wateja waliopo na wapya wanaokuja inakuwa ni kazi kubwa.
Hivyo itahitajika kuwa na watu wa kusaidia kwenye jukumu hilo na mengine kwenye biashara.

Hatua inayofuata ni kutafuta, kuajiri, kufundisha na kusimamia wafanyakazi kwenye biashara yako.
Hili ni zoezi linalokuwa gumu mwanzoni kutokana na kukosa uzoefu kwenye kuwapata watu sahihi.
Wengi wataonekana kutaka kazi, lakini wakishapewa kazi wanashindwa kutekeleza kwa namna inavyohitajika.
Hivyo kutakuwa na zoezi pia kwa ajili ya kuwaondoa wafanyakazi wasiokuwa na tija kwenye biashara.

Unapoajiri wafanyakazi wa kukusaidia majukumu mbalimbali kwenye biashara, gharama za biashara zinaongezeka.
Ili kumudu gharama hizo, biashara inalazimika kufanya mauzo makubwa zaidi. Hivyo zoezi la kutengeneza wateja wapya linapaswa kuendelea kufanyika kwa ukubwa zaidi.

Hivyo ndivyo mchezo utakavyokwenda kwa kujirudia rudia bila kuacha.
Mchezo mzima unahusisha watu.
Kupata wateja na kupata wafanyakazi.
Unaanza na kupata wateja, wakishakuwa wengi unaenda kwenye kupata wafanyakazi, ambao watahitaji kuwepo wateja wengi zaidi. Na wateja wengi zaidi watahitaji wafanyakazi wengi zaidi.

Kazi yako kubwa kama mmiliki wa biashara ni kubobea kwenye maeneo hayo mawili.
Na kadiri unavyokwenda unapaswa kujenga mifumo mizuri ambayo inarahisisha utekelezaji wa majukumu hayo muhimu na mengine kwenye biashara.
Kadiri unavyokaa kwenye huu mchezo na kuweka umakini wako wote, ndivyo unavyoziona fursa za kukua zaidi.

Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, kujenga biashara ndiyo kipaumbele cha kwanza kwetu.
Tunaweka juhudi kubwa kwenye kujenga biashara ambayo inaweza kujiendesha yenyewe bila ya kututegemea moja kwa moja.
Kwa lengo hilo muhimu, huu mchezo wa watu unakuwa sehemu ya maisha yetu.

Tunakazana na mchezo huo, licha ya magumu na changamoto zake, kamwe hatukati tamaa na kuacha.
Kila tunapokutana na changamoto kwenye kujenga na kukuza biashara zetu, tunajua chanzo kinakuwa kwenye maeneo hayo mawili, wateja na/au wafanyakazi.
Tunapokijua chanzo kwa uhakika na kukifanyia kazi, tunafungua ukuaji mkubwa zaidi kwenye biashara zetu.

Huu mchezo utaweza kuubobea na kuufurahia kwa kuingia na kuucheza na siyo kuwa mtazamaji wa nje au kuingia na kuucheza kwa juu juu tu.
Itakuwa kazi kubwa kuzama ndani kwenye mchezo huu, lakini ni kazi itakayozalisha matunda mazuri.
Kuwa tayari kuifanya kwa uhakika na utanufaika nayo sana baadaye.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe