Rafiki yangu mpendwa,

Kuna mambo ambayo unayafanya, ambapo kwako unaweza kuona ni sawa kabisa, lakini unakuwa unaishangaza dunia. Unakuwa unaishangaza dunia kwa sababu inashindwa kukuelewa kwa nini ufanye mambo ya aina hiyo.

Unasema kwamba unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako na unachagua kabisa eneo ambalo unataka kuyajenga mafanikio yako. Unaweka mipango ambayo utaifanyia kazi kwenye eneo hilo la mafanikio ulilochagua. Na pia unaanza kufanyia kazi mipango yako.

Ni katika kufanyia kazi mipango uliyonayo, ndiyo unakutana na uhalisia, ambao huenda hukutegemea kukutana nao. Uhalisia unaokutana nao ni vikwazo na changamoto ambazo zinakuwa kwenye safari ya mafanikio uliyoichagua. Vitu hivyo siyo kwamba vinatokea kwako tu, bali vinatokea kwa kila mtu aliyechagua safari ya mafanikio.

Sasa basi, mahali unapoishangaza dunia ni jinsi unavyochukulia hizo changamoto unazokuwa umekutana nazo.

Hatua kubwa unayochukua ni kuacha kufanya, kwa kuona kwamba huwezi tena kuendelea. Hapa unaishangaza sana dunia, kwamba wewe ulifikiri njia itakuwa imenyooka tu na utapata kila unachotaka kirahisi? Ulidhani wewe ni nani hasa kwamba uweze kupata kila unachotaka bila kukutana na changamoto? Kwa kweli unaishangaza sana dunia kuacha kile ulichochagua kwa sababu ya kukutana na changamoto.

Kingine ambacho unaishangaza nacho dunia ni kurudia kufanya vitu vingine, wakati hicho ulichochagua bado hata hujakikamilisha. Au unapokutana na magumu, badala ya kupambana kuyavuka, unakimbilia kuangalia vitu vingine rahisi zaidi kufanya. Unaishangaza dunia kwa sababu unatawanya nguvu ambazo ungezikusanya sehemu moja zingefanya makubwa. Lakini wewe unachagua kuzitawanya na kuishia kupata matokeo duni.

Kama unataka kuacha kuishangaza dunia, unatakiwa kujiamini kwenye kile ambacho umechagua na kuendelea kukifanyia kazi kwa uhakika bila kuacha. Usijali umekutana na nini, wewe umeshafanya maamuzi ya kwamba unataka mafanikio makubwa kwenye kitu hicho, basi pambana mpaka upate mafanikio hayo makubwa.

SOMA; JINSI YA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA

Usiruhusu kitu chochote kile kije kati yako na matokeo ambayo unataka kuyapata. Umeshaamua, basi heshimu maamuzi yako na yafanyie kazi kwa uhakika bila ya kukubali kuyumbishwa au kukwamishwa kwa namna yoyote ile.

Kabla dunia haijakupa makubwa ambayo unayataka, kwanza inakupima kuona umejitoa kiasi gani. Inataka kuona kama kweli unajiamini na utaweza kuhimili mafanikio makubwa ambayo unakwenda kuyapata. Ukishindwa kudhihirisha hayo, dunia itakupuuza na kukunyima mafanikio unayoyataka.

Wewe ionyeshe dunia kwamba upo tayari kupokea kile ambacho unakitaka kwa kukipambania bila ya kukata tamaa kwa namna yoyote ile. Fanya kila kinachopaswa kufanyika ili kupata unachotaka. Hayo yote yako ndani ya uwezo wako kama utakuwa tayari kuyafanyia kazi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeelezea zaidi jinsi ya kujitoa na kufanyia kazi kile unachotaka ili kukipata kwa uhakika. Karibu uangalie kipindi hicho hapo chini na uende kuchukua hatua kubwa ambazo zitakupa mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.