Rafiki yangu mpendwa,

Ili kupata kile ambacho kwa sasa huna, unapaswa kuwa mtu wa tofauti na vile ulivyo sasa. Hapa ndipo wengi wamekuwa wanakwama na kushindwa kupata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka kwenye maisha yao.

Wengi wanataka waendelee kuwa vile vile walivyo, huku wakifanya yale yale ambayo wamekuwa wanayafanya, halafu wapate matokeo ya tofauti. Hicho ni kitu ambacho hakijawahi kutokea hapa duniani na wala hakitaweza kutokea kwako.

Mabadiliko ya kweli huwa yanaanza na wewe mwenyewe kubadilika. Inapokuja kwenye kubadilika, wengi huwa wanaona ni kitu kigumu kufanya na hivyo kuendelea kubaki vile walivyo. Pale watu wanapoangalia mambo wanayopaswa kubadili kwenye maisha yao, wanaona ni mengi na ya kuwachosha.

Lakini huhitaji kufanya mabadiliko mengi na makubwa kwa mara moja ili kubadili maisha yako. Bali unapaswa kuanza na mabadiliko madogo kisha kwenda ukichukua hatua mpaka kuyabadili maisha yako. Na wala huhitaji kuingia gharama yoyote kwenye kuyabadili maisha yako, kwani sehemu kubwa ya mabadiliko unayopaswa kuanza nayo ni ya kimtazamo.

Sehemu ya kwanza unayopaswa kuifanyia mabadiliko ili uweze kuyabadili maisha yako ni mtazamo unaokuwa nao kuhusu maisha na mafanikio kwa ujumla. Na hapo ndipo kuna zoezi la siku saba ambalo ukilifanya litaweza kuyabadili kabisa maisha yako.

Moja ya vikwazo ambavyo vinawazuia watu kufanikiwa ni tabia ya kulalamika na kuwalaumu watu wengine. Pale ambapo watu wanakuwa wamekosa yale wanayotaka, wanatafuta watu wengine wa kuwalaumu au wanakuwa na malalamiko mbalimbali ya kwa nini wameshindwa.

Kulalamika na kulaumu haijawahi kumsaidia mtu yeyote kufanikiwa. Hivyo ili uweze kujenga mafanikio makubwa, hapo ndipo pa kuanzia.

Katika kuondokana na tabia ya kulalamika na kulaumu, ndipo unapaswa kufanya zoezi la siku saba ambalo lina nguvu ya kubadili kabisa maisha yako.

Kwa zoezi hilo, unaenda kwa siku saba bila ya kulalamika wala kulaumu kwa yeyote au chochote. Kwa siku saba unachukua uwajibikaji wa maisha yako na kwa kila kitu unajiambia wewe ndiye unayehusika. Kila siku unajifuatilia kuhakikisha hutelezi na kurudi kwenye lawama na malalamiko. Na ikitokea umejisahau na kulalamika au kulaumu, unaanza zoezi hilo upya.

SOMA; Hii Ndiyo Njia Ya Uhakika Ya Wewe Kupata Watu Sahihi Kwenye Maisha Yako.

Lengo ni uweze kwenda kwa siku saba bila ya kulalamika wala kulaumu kwa jambo lolote. Ukiweza kufanya hivyo kwa siku saba, mtazamo wako kuhusu maisha utabadilika sana. Jinsi unavyoyachukulia maisha itabadilika kabisa na utaona wapi umekuwa unajikwamisha kufanikiwa.

Ukiweza kufanya zoezi hilo kwa siku saba, maana yake utaweza kuendelea kulifanya kwa kipindi chote cha maisha yako. Hivyo unaanza na siku saba kwa sababu ni lengo dogo unaloweza kulikamilisha. Baadaye unafanya zoezi hilo kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku.

Ukiweza kuachana na tabia ya kulalamika na kulaumu, utayaona maisha yako kwa mtazamo mpya na mzuri zaidi. Utakuwa kama mtu uliyevua miwani ya giza na kuweza kuuona mwanga mzuri. Fanya zoezi hilo na achana kabisa na tabia ya kulalamika na kulaumu.

Kujifunza zaidi kuhusu zoezi hili la siku saba, angalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.