Habari wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO ambayo yana lengo la kutufanya kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Moja ya masomo tunayopata kwenye mauzo ni ya MAENDELEO BINAFSI ambayo yanatujenga sisi kuwa bora na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yetu kufanya mauzo makubwa.

Huwezi kufanya mauzo makubwa kama wewe siyo muuzaji bora. Na huwezi kuwa muuzaji bora kama wewe siyo mtu bora. Ndiyo maana kauli mbiu yetu ni KUWA MUUZAJI BORA, LAZIMA KWANZA UWE MTU BORA.

Kwenye somo hili unakwenda kujifunza kuhusu kujenga ushirikiano mzuri na watu wengine ili uwe muuzaji bora na ufanye mauzo makubwa. Ushirikiano ni kiungo muhimu kwa mafanikio kwenye mauzo na maisha kwa ujumla.

HAKUNA JESHI LA MTU MMOJA.

Huwa kuna watu wana mtazamo wa mafanikio kama jeshi la mtu mmoja. Imekuwa pia ni kauli maarufu kwamba kuna watu wameyapata mafanikio kwa kujijenga wenyewe (self-made). Lakini kwenye uhalisia mambo hayapo hivyo. Hakuna mtu yeyote anayeweza kujenga mafanikio makubwa yeye peke yake.

Kujenga mafanikio yoyote makubwa kunahitaji sana ushirikiano wa watu wengi. Unawahitaji watu ambao watakusaidia kwenye maeneo mbalimbali ndiyo uweze kufikia malengo makubwa uliyonayo.

Kama muuzaji ambaye unataka kupata mafanikio makubwa kupitia mauzo, futa kabisa mtazamo wa jeshi la mtu mmoja. Jua unawahitaji watu wengi wa kushirikiana nao ili kukamilisha ndoto zako.

Muhimu kujua ni kuhitaji ushirikiano wa wengine haimaanishi kuwategemea wao ndiyo wakupe mafanikio. Bali unahitaji kushirikiana nao, huku wewe ukiweka juhudi kubwa zinazokujengea mafanikio unayoyataka.

MAUZO NI MCHEZO WA TIMU.

Mauzo ni mchezo wa timu na ushindi unapatikana kwa ile timu yenye ushirikiano mzuri kwenye kucheza mchezo huo. Timu ambayo wachezaji wake ni wabinafsi, kila mmoja akitaka ushindi kwa ajili yake mwenyewe, haiwezi kupata ushindi mkubwa.

Kama muuzaji jua unawahitaji watu wengine waliopo kwenye biashara ambao siyo wauzaji. Wanaoandaa bidhaa au huduma unayouza, ni sehemu muhimu ya timu, bila ya wao, ahadi unazotoa kwa wateja hazitatimia.

Lakini pia wauzaji wenzako siyo washindani wako, bali watu unaohitaji kushirikiana nao ili mpate ushindi. Wauzaji ambao mpo kwenye biashara moja mnapaswa kushirikiana na siyo kushindana. Wakati mwingine unaweza kumshindwa mteja wewe, lakini mwenzako akaweza kumuuzia. Hivyo epuka sana ushindani wa kuwadidimiza wengine ili wewe uonekane kuwa juu. Shirikiana vizuri na wauzaji wenzako, hata kama wao watauza kuliko wewe, mchango wako utaonekana tu na kila mtu atakuheshimu kwa hilo.

Muhimu ni hata wauzaji wa biashara nyingine ambao mnashindana nao, unahitaji sana kushirikiana nao kuliko kujenga nao uadui. Licha ya kwamba wote mnauza kitu cha aina moja, bado haikukwamishi chochote kwa kujenga nao ushirikiano mzuri. Wauzaji wa upande wa ushindani wanaweza kuwa hawana bidhaa au huduma na wanataka kumwelekeza mteja mahali pengine pa kwenda kununua, watakuwa tayari kumwelekeza kwako kama mna ushirikiano mzuri.

Tasnia nzima ya mauzo inahitaji sana wauzaji ambao wana ushirikiano hata kama wanafanya biashara zinazoshindana. Si vyema kuwasema wauzaji wengine vibaya au kuwaharibia jina na sifa zao. Kushambuliana huwa kunaishia kuwa na hasara kwa wote, wakati kushirikiana kunawajenga wote. Wateja tarajiwa ni wengi sana, haina haja ya kugombana kwa sababu ya wateja wachache, kila muuzaji afanye kazi ya kujenga wateja wengi zaidi kwenye biashara.

SOMA; Kuwa Mchapakazi Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

JENGA USHIRIKIANO NA WATEJA.

Ili kufanikiwa kwenye mauzo, hupaswi kumchukulia mteja kama mtu anayekuletea tu fedha, bali mchukulie kama sehemu ya timu yako na wewe jichukulie kama sehemu ya timu yake. Kile unachowauzia wateja, jione ukiwajibika kuhakikisha wananufaika nacho na maisha yao yanakuwa bora. Mahusiano yako na wateja yasiishie tu kwenye kuwauzia na kupata fedha, bali yaendelee mpaka kwenye matumizi ya kile ambacho wamenunua na kuendelea kuwanufaisha zaidi.

Wafanye wateja waone wewe ni sehemu muhimu ya maisha yao kiasi cha wao kuwa tayari kukushirikisha mambo hata yasiyohusiana na kile unachowauzia. Kuwa tayari kuwasaidia kwenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wako hata kama hayahusiani na unachowauzia. Juana na wateja wako kwa mambo ya nje ya mauzo na hilo litaimarisha mahusiano yako na wao na kukupa mafanikio.

Kadiri unavyokuwa na mahusiano na ushirikiano mzuri na wateja wako, ndivyo wanavyojiona wakiwajibika kukusaidia ufanikiwe kwenye mauzo. Watakuwa tayari kukupa wateja wa rufaa na hata kuwaeleza watu wengine wengi kuhusu wewe na kile unachouza. Watakuwa tayari kukutetea katika hali mbalimbali kitu kitakachokunufaisha sana wewe.

Kujenga mahusiano na ushirikiano mzuri na wateja ni uwekezaji ambao utakunufaisha sana.

JENGA NA KUZA MTANDAO WAKO.

Kwenye mafanikio huwa kuna kauli kwamba UTAJIRI WAKO = MTANDAO WAKO (YOUR NETWORTH = YOUR NETWORK). Kauli hiyo ikiwa na maana kwamba ukubwa wa utajiri wako, unategemea ukubwa wa mtandao wako. Na mtandao hapo ukiwa ni watu unaowajua na wanaokujua wewe.

Umewahi kusikia kauli inayosema haijalishi unajua nini, bali unamjua nani. Wengi huchukulia kauli hiyo kama watu kupendelewa, lakini ukweli ni kwamba, huwezi kufanikiwa kama hutapata upendeleo fulani. Na upendeleo huo hautakuja tu, bali utatokana na mtandao uliojenga, wa watu unaowajua na wanaokujua wewe.

Kama muuzaji unapaswa kujenga na kukuza mtandao wako kadiri unavyokwenda. Mtandao wako unahusisha wateja wanaokujua, ambao wanapaswa kwenda wakiongezeka kadiri muda unavyokwenda. Lakini pia unapaswa kuhusisha watu wenye nyadhifa mbalimbali ambao kwa ushawishi wao wanaweza kukuwezesha kupata fursa nzuri.

Kujenga mtandao kwa mtu wa mauzo ni rahisi kuliko kwa watu wengine. Kwa sababu wewe tayari unayo sababu ya kuwafikia watu. Unaweza kumtafuta mtu yeyote yule, hata kama ana cheo cha juu au utajiri mkubwa, ukimweleza una fursa nzuri kwake na akawa tayari kukusikiliza.

Katika kujenga mtandao wako, kazana kutoa thamani kubwa kwa watu kiasi cha wao kuwa wanakutegemea zaidi. Epuka njia za kujenga mtandao wako kwa kujipendekeza kwa watu (maarufu kama ‘uchawa’ kwa siku hizi). Uchawa huwa una mwisho mbaya, lakini thamani inadumu mara zote. Utaheshimika kwa kutoa thamani kubwa kwa watu.

Ni kupitia kuwafikia watu wengi ndiyo unajenga na kuimarisha mtandao wako. Na kupitia mtandao mkubwa na imara unaokuwa umeujenga, utaweza kufanya mauzo makubwa na kupata mafanikio makubwa zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

DUNIA NI NDOGO, USIJENGA MAADUI.

Tunaishi kwenye dunia inayoonekana ni kubwa, lakini kwa teknolojia zilizopo, hii dunia ni ndogo sana. Kitu chochote ambacho unafanya kwa mtu yeyote, kinaweza kusambaa dunia nzima ndani ya muda mfupi. Hivyo epuka sana kufanya mambo ambayo yatakujengea uadui na watu wengine. Kwani yatasambaa kwa kasi kubwa na kuwa kikwazo kwako kupata mafanikio unayoyataka.

Mara zote fanya yale yaliyo sahihi na hata kama utashindwa kuelewana na watu wengine, basi isiwe kwa ubaya. Endelea kuheshimiana na watu na hilo litafanya uaminike na kuwa na ushirikiano mzuri na watu wengine na kukuwezesha kupata mafanikio makubwa.

Kila mara fanya mambo ambayo yanakuza mtandao wako na kuimarisha ushirikiano wako na wengine kwa sababu mafanikio unayoyataka, yanahitaji mchango wa wengine ili uweze kuyapata.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.