Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kwa muda mrefu bila kuacha. Tumejipa angalau miaka 10 (2024 – 2034) ya kwenda na uwekezaji tunaoufanya kwa msimamo bila kuacha au kutoa uwekezaji huo.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza tofauti iliyopo kati ya Uwekezaji (Investing) na Uchuuzi kwenye soko la uwekezaji (Trading).

Watu wengi wamekuwa wanashindwa kutofautisha uwekezaji na uchuuzi, kitu ambacho kinawazuia kupata manufaa ambayo yapo kwenye uwekezaji.
UWEKEZAJI.
Uwekezaji ni pale mtu anapoweka mtaji wake kwenye aina ya uwekezaji aliochagua na kuacha uwekezaji huo ukue thamani kwa kipindi cha muda mrefu. Kwa sababu ukuaji wa thamani ya uwekezaji huwa unakuwa ni mdogo, huwa inachukua muda mrefu kwa uwekezaji kufikia ukuaji mkubwa unaompa mtu manufaa. Nguvu kubwa ya uwekezaji ipo kwenye muda kuliko hata kiasi cha uwekezaji unaofanyika.
Chukua mfano wa watu wawili, ambao wana umri sawa na wamewekeza kwa kipindi cha miaka sawa, ila kwa kutofautiana wakati wa kuanza.
Wa kwanza anaanza kuwekeza akiwa na miaka 30 na anawekeza Tsh laki 1 kila mwezi kwa miaka kumi. Wa pili anakuja kuanza kuwekeza akiwa na miaka 35 na kuwekeza laki 2 kila mwezi kwa miaka 5. Wote watakuwa wamewekeza kiasi kinacholingana, lakini sasa angalia tofauti ya ukuaji wa thamani.
Anayewekeza laki moja kila mwezi kwa miaka 10 atakuwa amefikia thamani ya Tsh;
Wakati anayewekeza laki mbili kila mwezi kwa miaka 5 atakuwa amefikia thamani ya Tsh;
Kwa tofauti hiyo kubwa ya matokeo wakati kiasi ni kile kile, tunaona jinsi ambavyo nguvu kubwa ya uwekezaji ipo kwenye muda.
Faida ya kufanya uwekezaji ni kuwekeza na kuacha, kisha kuendelea na shughuli zako nyingine. Uwekezaji wako unakuwa unaongezeka thamani bila ya wewe kuhangaika nao kwa vyovyote vile. Ni wewe tu kuuacha muda ufanye mambo yake.
SOMA; Dhana Ya Riba Mkusanyiko Na Nguvu Yake Kwenye Uwekezaji.
UCHUUZI (TRADING).
Uchuuzi kwenye uwekezaji ni pale mtu anapovizia uwekezaji na kununua pale bei inapokuwa chini kwa lengo la kuuza pale bei ya uwekezaji huo inapopanda. Ukiangalia kwa haraka haraka, unaweza kuona ni kitu chenye manufaa, kwamba unanunua kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu. Lakini kwenye uhalisia, hilo ni gumu sana kutekeleza.
Pale uwekezaji unapokuwa na bei ya chini, hasa kama bei inashuka, watu wengi huwa wanakimbilia kuuza ili wasipate hasara. Kadiri watu wengi wanavyokimbilia kuuza uwekezaji, ndivyo bei yake inavyozidi kushuka na hivyo wanapata hasara zaidi. Kwa hiyo wengi hawawezi kununua uwekezaji ukiwa na bei ya chini. Kwa kifupi, uwekezaji unapokuwa unashuka bei, watu wanaingiwa hofu na kukimbilia kuuza.
Na pale uwekezaji unapokuwa na bei ya juu, hasa kama bei inapanda, watu wengi huwa wanakimbilia kununua ili wapate faida kwa kutegemea thamani kuendelea kupanda. Kadiri watu wengi wanavyotaka kununua uwekezaji, ndivyo thamani yake inavyozidi kupanda. Na hilo linapelekea watu kununua uwekezaji kwa gharama kubwa. Kwa kifupi, uwekezaji unapokuwa unapanda bei, watu wanaingia tamaa na kukimbilia kununua.
Katika hali ya kawaida ya kibinadamu, ni vigumu sana mtu kuweza kununua uwekezaji kwa bei ndogo na kuja kuuza kwa bei kubwa. Wengi hujikuta wakinunua uwekezaji kwa bei kubwa na kuuza kwa bei ndogo, kitu kinachowapa hasara kubwa. Hofu ya kupoteza na tamaa ya kupata ndiyo hisia kuu zinazoathiri maamuzi yetu wanadamu na kutuzuia kunufaika na uwekezaji wa kuvizia soko.
Tatizo jingine la uchuuzi wa uwekezaji ni kujidanganya kwenye uwezo wa kutabiri soko. Sisi binadamu hatuna uwezo wa kutabiri kitu chochote kile kwa uhakika wa asilimia 100. Wapo watu ambao wamewahi kutabiri vitu vikatokea, lakini ilikuwa ni kwa bahati tu na siyo uhakika. Kuchuuza uwekezaji ni kudhani unaweza kutabiri soko kwa usahihi, kitu ambacho hakuna anayeweza kukifanya.
Na mwisho, hata ikitokea kweli umenunua uwekezaji kwa bei ndogo, kisha bei yake ikapanda na ukaona ukiuza unatengeneza faida, huo mchakato wa kuuza na makato ya kodi yanayofanyika kwenye ongezeko la thamani, vinaishia kula sehemu kubwa ya faida ambayo unaona unatengeneza. Muda na juhudi utakazoweka kwenye kufuatilia soko mpaka uone wakati sahihi wa kuuza uwekezaji, hauwezi kufidiwa na faida kidogo unayokuwa umepata, hasa baada ya kukatwa kodi na tozo nyingine mbalimbali.
SOMA; Jua muda unaohitajika kwa uwekezaji wako kukua mara mbili.
WEKEZA NA SAHAU.
Kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU tunawekeza kwa mtindo wa WEKEZA NA SAHAU. Tunafanya uwekezaji kisha tunaendelea na shughuli zetu nyingine. Hatuhangaiki kuangalia bei imepanda au kushuka kiasi gani, sisi tunachojua ni kwa muda mrefu, thamani itakua. Hivyo tunaendelea kuwekeza kwa mpango wetu na siyo kuhangaika kutabiri nini kitatokea kesho.
Kwa mfumo huu wa WEKEZA NA SAHAU tunakuwa na utulivu mkubwa kwenye uwekezaji wetu na kunufaika na dhana ya RIBA MKUSANYIKO na KANUNI YA 72.
Tumechagua kuwa wawekezaji ambao nguvu yetu ipo kwenye muda na siyo wachuuzi ambao wanasumbuka na mambo ambayo hayapo ndani ya uwezo wao kuyadhibiti.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali haya;
1. Eleza tofauti ya Uwekezaji Na Uchuuzi na kipi kina manufaa zaidi.
2. Kwa nini ni vigumu sana kwetu binadamu kuweza kuvizia soko ili kununua uwekezaji kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu?
3. Unapewa nafasi ya kuchagua kati ya kuwekezewa elfu 5 kila siku kuanzia mwaka 2024 mpaka mwaka 2034 (miaka 10) au kuwekezewa elfu 10 kila siku kuanzia mwaka 2029 mpaka mwaka 2034 (miaka 5). Unachagua ipi na kwa nini? Onyesha kwa ukokotozi uchaguzi wako.
4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo la leo au programu ya NGUVU YA BUKU kwa ujumla.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama ishara ya kusoma na kuelewa kuhusu uwekezaji, ambalo ni hitaji muhimu la programu yetu ya NGUVU YA BUKU.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.