Rafiki yangu mpendwa,

Kwa miaka mingi ilikuwa inaaminika kwamba binadamu hawezi kukimbia umbali wa maili moja kwa muda wa chini ya dakika nne. Siyo tu kwamba kitu hicho kilichukuliwa hakiwezekani, lakini pia ilionywa ni hatari kwa afya, ambaye atajaribu kufanya hivyo atakufa kabisa. Madaktari walieleza jinsi ambavyo mwili wa binadamu hauwezi kuhimili mbio hizo za maili moja chini ya dakika nne.

Hivyo miaka na miaka watu waliamini haiwezekani kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Ni mpaka ilipofika mwaka 1954 ambapo mwanariadha Roger Bannister aliweza kuweka rekodi kwa kuwa mtu wa kwanza kukimbia maili moja chini ya dakika nne.

Kwa maelezo hayo, unaweza kuona ni kitu cha kawaida, kwamba jambo liliaminika haliwezekani, lakini Roger akapambana nalo mpaka kuliweza. Hiyo ni kweli, lakini kuna mengi nyuma ya hadithi ya Roger kukamilisha hilo ambayo ukiyajua yatakusaidia sana na wewe kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Hapa nakwenda kukushirikisha mambo hayo, jifunze kwa kina na uyafanyie kazi ili uweze kuvuka vikwazo ulivyowekewa na jamii na utumie uwezo mkubwa ulio ndani yako kufanya makubwa.

Moja; Roger Bannister alikuwa anaelekea kukata tamaa na kuachana na riadha.

Mwaka 1952 kulikuwa na mashindani ya Olympic ambapo Roger alikuwa anategemewa sana kushindwa. Lakini akaishia nafasi ya nne. Jambo hilo lilimuumiza sana na kwa miezi kadhaa alikuwa anafikiria kuachana na riadha. Lakini akaamua kujipa lengo kubwa zaidi la kuwa mtu wa kwanza kuweka rekodi ya kukimbia maili moja chini ya dakika nne.

Somo; hata kama unakwama au kukutana na magumu kiasi gani, usikubali kukata tamaa. Endelea kuweka malengo makubwa na kuyafanyia kazi.

Mbili; siku ya mbio hali ya hewa haikuwa rafiki.

Pamoja na kuweka lengo kubwa na kujiandaa vya kutosha, siku ya mbio ilipofika, hali ya hewa haikuwa rafiki. Kulikuwa na upepo ambapo mkimbiaji alikuwa anakabiliana nao na hilo kufanya mbio kuwa ngumu zaidi. Roger alipata tena mawazo ya kuahirisha mbio kwa siku hiyo, lakini alishawishiwa kushiriki.

Somo; pamoja na maandalizi makubwa unayoweza kufanya, kuna mambo yaliyo nje ya uwezo wako yanayoweza kuonekana ni kikwazo. Usikubali kukwamishwa na chochote, badala yake endelea kama ulivyopanga.

SOMA; Uwezo mkubwa ulio ndani yako wa kufanya makubwa.

Tatu; baada ya Roger kuweka rekodi, wengi waliweza kuvunja rekodi hiyo.

Kabla ya Roger Bannister kuweka rekodi ya kukimbia maili moja chini ya dakika nne, hakukuwa na mtu aliyewahi kujaribu na kufanikiwa kwenye hilo. Lakini baada ya Roger kuweka rekodi hiyo, mwezi mmoja baadaye mwanariadha mwingine naye alivunja rekodi hiyo. Na ndani ya miaka mitatu watu wengine 15 waliweza kuvunja rekodi hiyo.

Somo; unapoweza kufanya kile ambacho kinaaminika kushindikana, unakuwa umefungua milango kwa wengine nao kuweza kufanya. Hivyo endelea kupambania makubwa unayoyataka, siyo tu kwa ajili yako, bali jua kuna wengine wanaokuangalia na kwa wewe kuweza wanapata matumaini ya kuweza pia.

Rafiki, ni ndoto zipi kubwa ulizonazo ambazo watu wamekuwa wanakuambia haziwezekani au huwezi kuzitimiza? Hebu amua leo kwamba utazifanyia kazi ndoto hizo, kwa kuzipambania mpaka uweze kuzifikia. Puuza kabisa ukomo ambao wengine wamekuwekea na wewe zipambanie ndoto zako ukiamini bila ya shaka yoyote kwamba inawezekana.

Ni pale unapoamini bila ya shaka yoyote kwamba kitu kinawezekana, ndiyo kinawezekana kwenye uhalisia. Anzia hapo rafiki yangu na pambana mpaka kufanikisha yale unayotaka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini kuna mjadala mzuri sana kuhusiana na hilo la kuvuka ukomo uliowekwa na jamii. Washiriki mbalimbali wameshirikisha uzoefu wao binafsi kwenye kuvuka ukomo. Karibu usikilize ili uendelee kupata msukumo wa kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.