Rafiki yangu mpendwa,

Jinsi mifumo ya kijamii ilivyojengwa, inakuzuia wewe kupata mafanikio makubwa sana kadiri ya unavyotaka. Jamii itakusaidia uwe na maisha ya kawaida, kwa kuweza kutimiza mahitaji yako, lakini siyo kupata mafanikio makubwa.

Kuna njia tatu ambazo jamii imekuwa inatumia kukukwamisha wewe kupata mafanikio makubwa.

Moja ni kukulinganisha na watu wengine na kuondoa utofauti na upekee wako. Hilo ndiyo limekuwa linafanyika kwa miaka yote ambayo umekuwa shuleni na hata kwenye jamii. Umekuwa unalinganishwa na kushindanishwa na wengine, ambao mna uwezo tofauti. Matokeo yake ni unaacha kuwa wewe na kuanza kuiga wengine. Huwezi kujenga mafanikio makubwa kwa kuiga wengine, kwa sababu unakuwa umeacha uwezo wako mkubwa.

Mbili ni ukosoaji na ukatishaji tamaa wa jamii. Pale unapofanya mambo ya tofauti, unaanza kukosolewa mapema kabisa na kukatishwa tamaa. Kwa sababu jamii inakutaka ufanye yaliyozoeleka na ambayo yana matokeo ya uhakika hata kama ni madogo, kuliko kujaribu mambo mapya ambayo matokeo yake siyo ya uhakika. Na pale mtu anapopuuza ukatishwaji tamaa na kufanya na akashindwa, anakosolewa vibaya na kuonekana amepoteza. Hayo yamekuwa yanakufanya ubaki kwenye mazoea kuliko kufanya mambo ya tofauti.

Tatu ni mtazamo uliojengewa kwenye kukosea na kushindwa. Ukiwa shuleni, mtihani huwa unakuja na jibu moja sahihi, mengine yakiwa siyo sahihi. Na pale unapokosa jibu sahihi unaonekana ni mjinga na wa kushindwa. Lakini kwenye maisha, mambo ni tofauti, kukosea na kushindwa siyo mwisho wa safari, bali ni sehemu ya safari yenyewe. Mpaka ufanikiwe ni lazima utafanya makosa mengi na kushindwa mara nyingi. Kwa kukosea na kushindwa kuonekana ni kitu kibaya, umejengwa kuepuka makosa na kushindwa na hilo kupelekea kujizuia kufanya makubwa.

SOMA; Vyanzo Viwili Vya Vikwazo Vinavyokuzuia Kufikia Mafanikio

Ili uweze kuvuka vikwazo hivyo ambavyo jamii imekujengea na kushindwa kupata mafanikio makubwa, unapaswa kwenda kinyume na hayo matatu.

Kwanza kabisa ni lazima ukubali utofauti na upekee wako, kwa kufanya yale ambayo ni wewe tu unayeweza kuyafanya. Usikubali kulinganishwa au kushindanishwa na mtu mwingine yeyote, kwa sababu hakuna aliye kama wewe. Kila mara jitofautishe na wengine kwa kuwa wewe ili uweze kufanya makubwa ambayo yanawashinda wengine.

Pili usiogope kukosolewa au kukatishwa tamaa. Tambua kwamba unapokosolewa siyo kwa sababu yako, bali ni sababu ya kile unachofanya. Pia ukosoaji ambao wengine wanafanya kwako ni mrejesho mzuri kwako ambao ukiweza kuutumia vizuri utaweza kufanya kwa ubora zaidi. Kama watu wanakuambia utashindwa, angalau wanakuonyesha wapi utashindwa na hivyo kuweza kuchukua tahadhari sahihi ili uepuke kushindwa kwa namna hiyo. Pokea kukosolewa na kukatishwa tamaa kama njia ya kufanya kwa ubora zaidi.

Tatu usiogope kukosea na kushindwa. Jua kabisa kwamba hutaweza kujenga mafanikio makubwa bila ya kukosea na kushindwa. Unahitaji kuwa sahihi mara moja tu ili kujenga mafanikio makubwa. Makosa na kushindwa kote unakopitia kunakusogeza karibu zaidi na mafanikio unayokuwa unayataka. Ni pale unapokata tamaa na kucha ndiyo unakuwa umekubali kushindwa kabisa. Wewe usikubali hilo, pambana kwa uhakika mpaka upate mafanikio unayoyataka.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri juu hilo la jamii kukukwamisha kufanikiwa. Kumekuwa na michango mizuri ya washiriki wa kipindi pamoja na shuhuda zao mbalimbali. Karibu usikilize kipindi hicho hapo chini na kuchukua hatua ili kuvuka vikwazo vya kijamii na kujenga mafanikio makubwa kwako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.