Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi ambao huwa wanaanzia chini na kupambana sana kujijengea mafanikio, huwa wanajisukuma sana wakiwa chini. Ni huo msukumo mkubwa ndiyo unaowafanya wapige hatua kubwa za mafanikio.
Katika kujisukuma huko na kupiga hatua, watu hao huwa wanakutana na fursa nzuri ambayo inakuwa inawanufaisha sana. Na hapo ndipo wanapojikuta kwenye mtego mkubwa ambao wakishindwa kuuvuka wanaishia kuyapoteza mafanikio waliyoyajenga.

Huwa inakuwa hivi, mtu anapokutana na fursa ambayo inamlipa vizuri, anaweka umakini wake wote kwenye kuitumia vyema fursa hiyo na kuhakikisha ananufaika nayo kwa viwango vya juu. Hilo ni jambo jema, kwani mtu anakuwa amepambana sana mpaka kufika kwenye fursa hiyo.
Lakini ambacho mtu anakuwa amesahau ni kwamba mambo huwa yanabadilika, hayabaki vile yalivyo mara zote. Hivyo wakati ananufaika na fursa, kuna mabadiliko yanayokuwa yanatokea na kuleta fursa nyingine kubwa zaidi. Kwa watu kubaki kwenye fursa za awali, wanakuja kujikuta wameachwa nyuma na pale fursa hiyo inapokuwa haifanyi tena kazi, wanapata anguko.
Mafanikio ambayo mtu anayapata yanakuwa yamemweka kwenye mtego kwa sababu anatakiwa ayavune kwa kiasi kikubwa, lakini pia wakati huo huo anatakiwa kuendelea kufanyia kazi fursa mpya ili asiachwe nyuma. Huo ndiyo mtego ambao wengi wamekuwa wanashindwa kuuvuka na kuishia kupata anguko baada ya kufanikiwa.
SOMA; Je unajua gharama ya mafanikio makubwa unayotaka kupata?
Ili kuweza kuvuka mtego huo unapaswa kujua kwamba kile kilichokufikisha hapo ulipo sasa, siyo kitakachokupeleka mbali zaidi. Kilichokufikisha hapo ulipo sasa ni fursa ambazo umeshakutana nazo, wakati kitakachokufikisha mbali zaidi ni fursa ambazo bado hujakutana nazo.
Ukifanyia kazi zile fursa ulizonazo sasa pekee, utaishia kupata matokeo unayoyapata sasa, ambayo hayatakuwa makubwa sana. kupata matokeo makubwa zaidi ya unayoyapata sasa, ni lazima uendelee kuibua fursa nyingine za tofauti na kuzifanyia kazi.
Hilo linakutaka ujipange vizuri ili uhakikishe hushindwi kutumia vizuri fursa uliyonayo sasa, wakati huo huo uwe unafanyia kazi fursa mpya zinazokuja. Hiyo inakutaka ufanye kazi zaidi ya ulivyokuwa unafanya huko nyuma. Na hapa ndipo panapowachanganya wengi, kwa kudhani wanapofanikiwa basi watahitaji kufanya kazi kidogo, wakati uhalisia ni kadiri wanavyofanikiwa ndivyo wanavyokuwa na kazi nyingi zaidi za kufanya.
Ili uweze kujenga mafanikio makubwa na yatakayodumu na kuendelea kukua, mara zote kuwa na njaa ya mafanikio na mara zote kuwa mjinga. Njaa itakusukuma kuchukua hatua kubwa zaidi hata baada ya kuwa umeshafanikiwa. Na ujinga utakufanya uwe tayari kuendelea kujifunza hata unapokuwa juu.
Mafanikio kiasi huwa yanawapeleka wengi kwenye anguko pale wanaposhiba mafanikio na kujiona hawapaswi kujitesa. Pia wanapokuwa na kiburi kwa kuona tayari wanajua kila kitu na hakuna kipya cha kujifunza, hilo huwapelekea kufanya makosa ambayo yanaishia kuwagharimu sana.
Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ujifunze jinsi ya kutumia mafanikio yoyote unayoyapata kuwa ngazi ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa zaidi badala ya kukupoteza. Fungua kipindi hapo chini uweze kujifunza na kuwa bora.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.