3370; Sifa ya kupambania kuwa nayo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa unaanzia chini kabisa na watu wengi hawakujui, safari yako ya mafanikio huwa inakuwa ngumu sana.
Unaweza kuwa na nia njema kabisa na kuwaeleza watu jinsi ambavyo unakwenda kuwapa manufaa makubwa.
Lakini kwa sababu hakuna anayekujua, unaishia kupuuzwa.
Hilo linakuumiza kwa sababu unakuwa unajua kabisa manufaa unayoweza kuwapa wengine, ila wao wanakuwa wazito kukubali kukupa hata nafasi.
Hilo pia lipo sana kwenye mauzo.
Una bidhaa au huduma ambayo ni nzuri na ya uhakika, ambayo inaweza kumpa mtu manufaa makubwa sana.
Unajua kabisa mtu anaihitaji bidhaa/huduma hiyo ili maisha yake yawe bora, na pia anaweza kuimudu.
Lakini kila unapowashawishi wainunue, wanakuwa wagumu kufanya hivyo.
Wanakukatalia kabisa, kitu ambacho kinakushangaza sana, maana ni manufaa makubwa wanayokuwa wanayakataa.
Ni katika hali hii ndiyo watu wengi huishia kukata tamaa na kuona hawawezi kuendelea. Kwa ugumu unaokuwa mbele yao, wanashindwa kujua nini wafanye, hivyo wanakubali kwamba ni kitu kisichowezekana na hivyo kuachana nacho.
Lakini maamuzi sahihi hayapaswi kuwa ni kuacha, badala yake kukomaa mpaka watu wajenge imani kwako na kukubaliana na wewe.
Kama unajua ulichonacho ni sahihi na kina manufaa makubwa kwa watu, unachohitaji ni kuwapa watu muda ili waweze kuelewa
Ukikataliwa na watu na wewe ukakata tamaa, maana yake umewaambia wako sahihi.
Lakini ukikataliwa na ukaendelea kung’ang’ana bila kuchoka, itawafanya baadhi ya watu kutaka kukujaribu waone kwa nini unang’ang’ana sana.
Katika kujaribu kwao wanaipata thamani ambayo ni kubwa sana. Hilo linawafanya waendelee kupata kitu hicho kwako.
Na kadiri wanavyoendelea kupata thamani, ndivyo wanavyozidi kukuamini na kuwa tayari kuendelea.
Hilo halitaishia hapo, bali atazisema habari zako kwa wengine, ambao watakuwa rahisi kuwashawishi nao wapate kile unachotoa.
Kwa kila kitu unachofanya kwenye maisha yako, sifa kuu unayopaswa kujijengea ni ya mtu wa kuaminika, kutegemewa na anayetekeleza mambo.
Hiyo ni sifa ambayo ukishakuwa nayo, mambo yako yanakuwa rahisi sana, unaaminika kwa urahisi na unapewa fursa kubwa na nzuri ambazo mwanzo ilikuwa vigumu kuzipata.
Na jinsi ya kujenga sifa hiyo ya kuaminika, kutegemewa na kutekeleza mambo ni kwa matendo na siyo maneno.
Hutaweza hilo kwa maneno na ahadi, bali kwa matendo yako.
Ni kupitia kuahidi na kutekeleza ndiyo unaijenga sifa hiyo kwa uhakika.
Hivyo basi, wajibu wako mkuu kwenye chochote unachofanya ni kuahidi na kutekeleza.
Yaani ni kusema utafanya kitu, kisha kukifanya kweli kama ulivyosema, badala ya kuja na sababu na maelezo kwa nini umeshindwa kufanya.
Lifanye kila neno lako kuwa sheria, maneno yako yawe dhamana tosha kwenye kila jambo.
Ukiweza kujenga hiyo sifa, ambayo inahitaji kuwa mtu wa vitendo na kwa muda mrefu, utafungua milango mingi ya kukupa mafanikio makubwa.
Yote hayo yatawezekana kwa uhakika kama utabaki kwenye mchezo na kuendelea kucheza kwa uhakika bila kuacha, hata uwe umekutana na nini.
Mwanzo wengi watakupuuza, hata kama una thamani kubwa kiasi gani kwao.
Lakini kama wataendelea kukuona upo, wanashawishika kukujaribu na hapo ndiyo wanakuwa wamenasa kwenye mtego wa kuendelea na wewe milele.
Kwenye jamii ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni jamii ya tofauti tunayoijenga, tumechagua kutoa thamani kubwa na kuisimamia kwa uhakika bila ya kukata tamaa kwa namna yoyote ile.
Tunajiamini kwenye thamani tuliyonayo na mara zote tunaipigia kelele kwa watu wengi zaidi.
Kwa kila nafasi tunayoipata, tunaitumia vizuri kujenga sifa ya kuaminika na kutegemewa kwenye kukamilisha mambo.
Tupo tayari kuumia na kuingia gharama ili kutekeleza yale tuliyoahidi bila ya kutetereshwa na chochote.
Kwa kupambana na kujenga sifa hiyo kuu ya kuaminika, kutegemewa na kukamilisha mambo ndiyo tunafungua milango ya fursa kwetu na kunufaika kwa uhakika.
Lakini tunajua siyo jambo rahisi, bali jambo linalohitaji kazi kubwa na muda mrefu wa kutosha.
Sisi tupo tayari kwa yote, tupo tayari kuweka kazi kubwa na tupo tayari kujipa muda wa kutosha.
Tunajua kwa uhakika, kazi na muda vitatufikisha mbali sana, na hivyo tunabiweka bila kusita.
Tunachopambania ni sifa kuu ya KUAMINIKA, KUTEGEMEWA na KUKAMILISHA MAMBO.
Tukishaijenga hiyo kwa uhakika, mengine yote yanakuwa rahisi sana kwetu.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe